JIEPUSHE NA UNAJISI.

JIEPUSHE NA UNAJISI.

Jina La Bwana wetu Yesu libarikiwe. Karibu tuyatafakari maandiko tena siku ya leo.

Kuna mtafaruku mkubwa sana katika ukristo kuhusu vyakula, wapo wanaoamini kuwa vipo vyakula najisi na wapo wanaoamini kuwa vyakula vyote ni halali kuliwa. Na hivyo kusababisha mashindano yasiyoisha.

Kama tukiyasoma maandiko tutaona kuwa vyakula haviwezi kumtia mtu unajisi. Ingawa hatuwezi kusema kwamba vyote vinafaa, hapana si vyote..huwezi kula mbao, au chuma, au sumu au pombe na kusema vinafaa…hapana hivyo havifai kwasababu vinauharibu mwili badala ya kuujenga.

1Wakorintho 10:23 “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo”.

Kwahiyo kama umehakiki hicho ulacho hakina madhara katika mwili wako, basi kula! Si dhambi..lakini kama umehakiki kwamba kina madhara basi usile. Na pia kama unawasiwasi na mashaka kwamba hicho ulacho kinaweza kuwa na madhara basi usile kabisa. Kwasababu hata usipokula hutendi dhambi!!

Warumi 14:22 “ Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali.

23 Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi”.

Sasa leo hatutaingia sana kujifunza juu ya vyakula, kama utahitaji somo juu ya hilo, basi utatujuza inbox..Lakini tutajifunza namna ya kuepukana na unajisi, kwa kupitia maandiko yafuatayo ambayo ni maarufu sana.

Tusome…

Marko 7:5 “Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?……………………………..

14 Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu.

15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu.

16 Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.]”

Sasa maneno haya Bwana wetu Yesu aliwaambia makutano, ambao pengine idadi yao ilikuwa ni mamia au maelfu, na ndani ya mkutano huo walikuwepo pia wanafunzi wake wale 12, Na kwa Pamoja wakasikia maneno hayo…kwamba hakuna kimwingiacho mtu kimtiacho unajisi bali kimtokacho..sasa baada ya maneno hayo kama umefuatilia kwa makini Bwana hakuendelea kuongea zaidi. Hivyo kila mmoja akatoka na tafsiri yake kichwani…naamini wengi walifiki kwamba ni kimwingiacho mtu ni chakula na kimtokacho ni matapishi au kinyesi na mkojo..na kwamba hivyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi..Lakini ule mkutano wote ulitawanyika ukidhani umemwelewa Bwana vizuri kumbe hawakumwelewa hata kidogo..

Baadaye ndipo wanafunzi wake wakahisi kuna kitu hawakukielewa na hivyo wakaamua kumfuata wakiwa peke yao kumwomba awafafanulie zaidi..

Tusome..

“17 Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. 18 Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi;

19 kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.

20 Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

21 Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

22 wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

23 Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi”.

Umeona hapo?. Wanafunzi wamepata ufafanuzi vizuri, lakini makutano hawakupata!..Makutano wameondoka wakidhani unajisi ni majasho, matapishi, haja kubwa na haja ndogo…Kumbe sivyo!. Vitu najisi ni vile vinavyotoka moyoni na si mwilini…

Unapopita barabarani na kwa bahati mbaya ukasikia matusi yakitukanwa… yale yanaingia moyoni mwako, na kwenda kwenye hazina ya kumbukumbu zako, (hapo hakuna unajisi)..lakini unapopitia hali ya kuudhiwa siku za mbeleni na kwenda kuifungua ile hazina na kisha kuyatumia yale matusi uliyoyasikia huko nyuma na kumtukana mwingine hapo ndipo unapokuwa najisi.

Unapoona mauaji yamefanyika ambayo sio wewe umeyafanya kwamfano mauaji ya utoaji mimba..Jambo lile linakwenda kwenye hazina ya moyo wako, hapo hujawa najisi, lakini siku moja ukapata ujauzito na ukaenda kuutoa au mwingine akapata ujauzito na ukamshauri akaitoe, hapo tayari umekuwa najisi. Na mambo mengine yote ni hivyo hivyo.

Na mtu najisi mbele za Mungu ni mtu mchafu..Katika agano la kale mtu najisi alikuwa haruhusiwi hata kuingia katika kusanyiko la Mungu, anatengwa mpaka atakaposafishika…Na hata sasa bado unajisi upo!..Ukiwa mlevi tayari umejitia unajisi, ukiwa mwasherati, mzinzi, muuaji, mtukanaji, mlawiti, mtazamaji picha za tupu, msengenyaji n.k tayari wewe ni najisi mbele za Mungu, hustahili kuwepo katika kundi la Mungu, haijalishi umeshakuwa mkristo kwa miaka mingapi, bado ni najisi mbele za Mungu, kwamba unahitaji kutubu..Na kujitenga na hayo mambo.

Tito 1:15 “Vitu vyote ni safi kwa hao walio safi; lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia. Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai”.

Kama hujaokoka! Kristo anakupenda na alikufa kwa ajili yetu..Wokovu unapatikana bure leo, unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kupiga magoti binafsi, na kutubu mbele zake kwa dhati kabisa..Kama umemaanisha kweli pale utakaposema tu Amen, basi tayari ameshakusikia na kukusamehe..na utaona amani ya ajabu imeingia moyoni mwako, baada ya hapo nenda katafute ubatizo sahihi wa kimaandiko, ambao ni ule wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo, ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19, Matendo 2:38)..Kwa kuyatii maagizo hayo machache na mepesi utakuwa utakuwa umeihakikishia mbingu kuwa kweli umeanza umegeuka na hivyo Mungu atakuheshimu zaidi. Na utakaso halisi wa Kristo utakuja ndani yako.

Bwana akubariki.

Kama umeokoka usisahau kuliombea Kanisa Pamoja na wakristo wote na watumishi wa Mungu kila siku..

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

 Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?

LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

Mkatale ni nini katika biblia? (Matendo 16:24)

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Winfrida damian
Winfrida damian
2 years ago

Amen amen