MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

Maombi(uombaji) ni nyenzo namba moja ya kumfikisha mtu uweponi mwa Mungu kwa haraka sana. Na kama tunavyofahamu sikuzote mtu yeyote aliyepo mbele za uso wa  Yehova mwenyewe, uwezekano wa yeye kujibiwa mahitaji yake yote upo. Hivyo shetani kwa kulijua hilo hataki, mtu wakati wowote mtu afike huko hivyo anachofanya ni kumletea tu saikolojia za kipepo ili zimfanye asidhubutu kutaka kwenda kusali wakati wowote.

Na baadhi ya saikolojia hizo ni hizi:

  1. Nimechoka:

Siku zote Kabla ya mtu hajafikiria tu kwenda kuomba, mawazo ya kwanza yanayomjia kichwani pake ni “nimechoka”..Ataanza kufikiria Nimekuwa kazini siku nzima, sijapata muda wa kupumzika, hata kidogo, hapa nilipo usingizi wenyewe umenikamata, najisikia homa homa, hivyo wacha leo nipumzike nitaomba siku nyingine..

Mwingine atasema nimefanya kazi ya Mungu siku nzima, tangu asubuhi hadi jioni hata sasa bado wapo watu wananitegemea nikawafundishe, nina mialiko mingi ya mikutano hivyo wiki hii nimechoka wacha nisiende kusali..

Lakini Bwana wetu Yesu Kristo yeye alikuwa anachoka kuliko hata sisi kwa utumishi mgumu kwa kuzunguka huko na kule, Utaona upo wakati baada ya kuwahubiriwa makutanao siku nzima mpaka imeshafika jioni badala awaage aende akapumzike kidogo, kinyume chake aliwalazimisha mitume wake watangulie mashuani,  yeye akabaki nyuma kwenda kusali mlimani, alikaa kule masaa mengi, akisali, sio kwamba hakuwa amechoka hapana. Lakini alijua umuhimu wa maombi.

Mathayo 14:22  “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.

23  Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

24  Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.

25  Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.”

Sisi pia, kwanini Neno “Nimechoka” linataka kuchukua nafasi ya maombi yetu?.Kwamwe tusikiendekeze hicho kigezo cha nimechoka kuchukua nafasi yetu ya maombi.

    2. Sina Muda wa kuomba:

Neno lingine shetani analoliwekwa kwenye vichwa vya watu ni hili “sina muda wa kuomba”..kwani nimetingwa na mambo mengi, na shughuli nyingi nipo bize sana…Nimekutana na Watu wengi wakiniambia maneno haya, wanasema wanashindwa kwenda ibadani au kuomba kwasababu ya kukosa muda….Wapo pia watumishi wa Mungu wanaosema mimi nipo bize sana na huduma hivyo sina muda wa kuomba binafsi muda mrefu, ninamialiko mingi ya semina, sehemu mbali mbali..

Lakini nataka nikuambie pia tunaye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ndiye kielelezo cha utumishi wetu, yeye alikuwa bize kuliko hata sisi, muda mwingine makutano walikuwa wanamsonga, muda wote wanataka awafundishe lakini biblia inatuambia..alijieupua, akaenda kutafuta mahali pa utulivu akaomba huko..

Luka 5:15 “Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao.

16  Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba”.

Alifanya vile kwasababu alijua hata ile huduma aliyokuwa anaifanya ilihitaji maombi ili iweze kusimama, ni jambo la kushangaza kama tutasema sisi ni watumishi wa Mungu halafu tunakosa muda wa kuomba…Nasi pia tujiepue tupate muda wa kuomba binafsi.

  1. Mbona ninaweza kuishi bila maombi:

Jambo lingine ni hili shetani analileta kichwani,.. mbona ninaweza kuyamudu tu Maisha yangu bila maombi?..Ni kweli utayamuda Maisha yako ya kidunia, lakini sio Maisha yako ya wokovu.

Utamudu kwenda disko, utamudu kuendelea kuwa mlevi, utamudu kuiba, utamudu kuwa mwasherati na utamudu kuwa bize na kazi zako kuliko hata hata kumtafuta Mungu  na mambo mengine yanayofanana na hayo utayamudu kwasababu hayo yote hayahitaji maombi.

 Lakini ukisema umeokoka halafu sio mwombaji, basi ujue hutaweza kuyashinda majaribu ya aina yoyote ile, Bwana Yesu mwenyewe alisema..Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni..Unadhani alikuwa anatania, unadhani shetani ataufurahia wokovu wako, ustarehe tu, halafu mwisho wa siku uende mbinguni?. Atakutafuta tu na kama wewe sio mwombaji basi huwezi kuchomoka,..na ndio maana taamaa za mwili unashindwa kuzitawala, kwasababu huombi, unashindwa kuwa na kiasi kwasababu muda wa maombi huna, hauuhisi uwepo wa Mungu maishani mwako, kwasababu wewe sio mwombaji..

Yakobo 4:1  “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?

2  Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa HAMWOMBI!”

Maombi ni Mafuta ya wokovu, kama vile gari lisivyoweza kwenda bila Petrol vivyo hivyo, wokovu wako hauwezi kupiga hatua yoyote bila kuwa maombi..

  1. Sina uhakika wa kujibiwa maombi yangu:

Saikolojia nyingine ya ki-shetani ni hii ya kudhani kuwa  maombi yako hayawezi kujibiwa. Unaona kama ukiomba utapoteza muda bure,.Nataka nikuambie, Maombi yote yanasikiwa ikiwa utaomba sawasawa na mapenzi yake, lakini sio jambo la kufanya siku moja halafu basi Kesho unaendelea na mambo yako mengine, maombi ni sehemu ya Maisha ya mkristo ni mwendelezo, majibu ya maombi mengine yanakuja kwa kuomba tena na tena, leo, Kesho, Kesho kutwa n.k…lakini katika kuomba huko Bwana Yesu ametupa uhakika kuwa Ombi lolote la namna hiyo mwisho wa siku ni lazima lijibiwe tu..haliwezi kuachwa..

Luka 18:1  “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa”.

Mathayo 7:7 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; 8  kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa”.

Mwisho, nataka nikuambie Wapo watu wanadhani wanaweza kuvumbua njia nyingine ya kuwasiliana na Mungu kirahisi au watapata suluhisho la matatizo yao Zaidi ya maombi..Fahamu kuwa Bwana wetu Yesu ameshatusaidia kufanya utafiti, sasa usitafute utafiti mwingine wa kwako wewe au wa kwangu mimi mbali na ule aliouthibitisha Yesu wa maombi..Yeye alikuwa hana dhambi hata moja, alikuwa ni mtakatifu sana, lakini katika utakatifu wake wote huo hakutupilia mbali suala la maombi alilifanya kama nyenzo ya yeye kufikia malengo yake, alifanya maombi kuwa sehemu ya Maisha yake..

Na wakati mwingine alikuwa anaomba kwa jasho na machozi mengi, na hata damu ilimtoka, akisihi mpaka akawa anasikilizwa…

Vinginevyo asingepokea kitu, Je mimi na wewe ambao si wakamilifu kama Bwana Yesu tunapaswaje?..tunaona raha gani kuishi Maisha ya kutokuomba halafu tunajiita bado ni wakristo..?

Waebrania 5:7  “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu”;

Hivyo tusitafute njia ya mkato..Kama tunataka tumwone Mungu akitembea katika Maisha yetu kwa ukaribu Zaidi na sisi, huu ndio wakati wa kuanza upya tena kwa nguvu za Maombi. Bwana alituambia walau saa moja kwa siku..Hivyo tujitahidi, tupambane, tushindane, tusiruhusu uongo wa shetani utuvurugie uombaji wetu, tusiruhusu, kukosa muda kutuvurugia ratiba yetu, tusiruhusu kutegemea nguvu zetu na akili zetu kutuharibia uombaji wetu..

Tuombe, tuombe, tuombe..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

https://wingulamashahidi.org/mafundisho-ya-ndoa/

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!

UJIO WA BWANA YESU.

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

AMEFUFUKA KWELI KWELI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments