LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

Shalom, kila mahali biblia inatuasa juu ya kujiweka tayari, wakristo wengi tunadhani wokovu ni suala la kuotea tu kwamba nitaokoka au tutaokoka siku yoyote, au baada ya kuokoka leo basi hakuna haja ya kuyakamilisha yale mapungufu niliyonayo..Hatujui kuwa wokovu ni process, ni mchakato endelevu,. ni jambo lenye maandalizi, maana yake ni kuwa mpaka unyakuliwe ni lazima uwe umekidhi vigezo vyote vya kuwa bibi-arusi kamili wa Kristo, na sio suria.

Kama tunavyoijua ile habari ya wanawali 10 katika Mathayo 25. Ni habari ambayo inatupa picha halisi ya kitakachotokea muda mfupi kabla ya Yesu kurudi, ambapo tunaona 5 wao walikuwa werevu na 5 wao walikuwa wapumbavu, Lakini wote hawa walikuwa wanadai wanamngojea Bwana wao aje waende karamuni, mfano tu makundi yaliyochanganyikana ya wakristo leo kanisani, kila mtu anadai anamngojea Bwana, hata Yule mzinzi kanisani naye pia madai yake ni hayo hayo.. Lakini tunasoma wale werevu walikuwa wamejiandaa kwa kila kitu, mpaka na mafuta ya ziada katika chupa zao, lakini wale wengine hiyo kwao haikuwa na umuhimu hata kidogo, japokuwa walijua kuwa taa zao hazitadumu, lakini hawakulizingatia hilo, waliendelea kubahatisha hivyo hivyo tu, wakidhani maadamu wameshafika mahali pa kumsubiria Bwana basi hiyo inatosha..Lakini kilichotokea ni kwamba, ghafla tu usiku wa manane, pakawa na kelele..

Wote wakashtuka kuna nini? Wakaambiwa Bwana wao anakuja,..wale werevu wakawasha taa zao, lakini wale wengine ndio wakaanza mchakato wa kuzichochea taa zao, wakawa wanaona zinazima, wakaanza kuwaomba wenzao wawapunguzie kidogo, Lakini hilo halikuwezekana ikabidi wakajinunulie ya kwao (kwasababu Roho Mtakatifu hatolewi kwa mwanadamu bali kwa Mungu..Na waliporudi wakakuta mlango umeshafungwa..

Mathayo 25:6 “Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.

11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.

12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi”.

Ni jambo gani nataka tuone hapo; kabla mlango haujafungwa, palitangulia  kwanza na sauti za kelele ili  kuwaamsha wote..Yaani maana yake ni kuwa wote walipewa muda mfupi sana wa neema kutengeneza mambo yao kabla Bwana hajawasili.. Lakini muda huo haukuwa si muda wa kwenda tena kununua mafuta, ulikuwa ni muda wa kuwasha tu taa.

Ndivyo ilivyo katika siku hizi za mwisho,.Tunapozidi kuukaribia ule mwisho, wakati wa unyakuo, kabla parapanda haijalia, kutatangulia kwanza sauti za kelele, sauti hizo zitakuwa ni mahubiri maalumu ambayo yatahubiriwa katika ulimwengu mzima, hayo ni mahususi kwa ajili ya kuwaweka tayari watakatifu wote waliomwamini Yesu kwa ajili ya tukio la unyakuo ambalo linakwenda kutokea ndani ya kipindi kifupi sana.

Lakini wakati huo ukifika, na wewe ulikuwa hauuthamini wokovu wako, ulikuwa unaishi hoe hae tu, vuguvugu, mguu mmoja nje, mwingine ndani..usidhani siku hiyo itakuwa ni ngumu kuivuka.. Hata iweje, Ni kweli utajua kabisa Unyakuo umefika, na utaanza michakato ya kuyatengeneza mambo yako kwa Mungu, lakini hilo halitakamilika, ghafla tu utashangaa wenzako uliokuwa unashiriki nao kanisani hawapo ndipo utakapokuwa katika kilio cha kusaga meno.

Wokovu ni maandalizi..Kwenda katika unyakuo, ni kukamiliza vigezo vyote, sio kusema tu nimeokoka, halafu basi, wale wanawali wapumbavu nao pia walikuwa wameokoka, lakini kumbuka kwa Mungu hatufiki kwenye muda wenyewe tuliopangiwa, hapana bali tunafikia ndani ya Muda….Kwa mfano mtu akikuambia tuonane saa 8 kamili..na wewe ukafika pale muda huo huo wa saa 8, hapo ni sawa na umefika kwenye muda wenyewe..Lakini ukifika saa 7 na nusu, hapo umefika ndani ya muda, na ndio Mungu anachotaka kwetu.. Kwa Mungu ukifika saa 8 umeshachelewa..

Kwasababu, kabla haujamfikia huwa kunakuwa na maandalizi rasmi. Na ndio maana hata ukisafiri huwa unawekewa kabisa muda wa kuwasili(reporting time) na Muda wa kuondoka(departing time), Kama ukisema mimi nitafika ule muda wa kuondoka..Ujue tayari umeshachelewa, kwasababu zipo hatua za kufuata ambapo mpaka ukamilishe zote, tayari ule muda wa kuondoka utakuwa umeshapita..

Hivyo, katika hichi kipindi cha mwisho, wewe kama mkristo unaishi ukristo wa kubahatisha, ule wa kusema tu mimi nimeokoka, halafu, hakuna mabadiliko katika maisha yako, siku zinakwenda siku zinarudi haujiweki sawa kwa ajili ya kurudi kwa pili kwa Kristo. Ndugu yangu nataka nikuambie, Unyakuo utakupita, mbele ya macho yako hivi hivi ukiona ikiwa wakati huo utakuwa hai. Na kama utakuwa umekufa hutafufuliwa, kuungana na walio hai kwenda mbinguni.

Huu wakati wa mwisho ni wa ajabu kwasababu biblia inatoa maelezo kuwa kutakuwa na makundi mawili ya wakristo wakristo wanaomngojea Bwana, na sio kundi moja kama inavyopaswa  iwe, ndio hao wanawali werevu na wapumbavu. Sasa swali la kujiuliza mimi na wewe je!  tupo katika kundi lipi?

Sio kila staili unayoiona kwa watu Fulani wanaoitwa wakristo  ni ya kuiiga..

Sio kila maisha unayoona anaishi mtu Fulani anayejiita mkristo ni ya kuyaiga.

Sio kila mahubiri na mafundisho ni ya kuyasikiliza, ni lazima uyachuje.

Sio kila sauti inayosema ndani yako ni ya kuifuata.

Huu ni wakati wa kuitengeneza taa yako wewe mwenyewe binafsi, na kuwa na uhakika kuwa hata leo mambo ya kibadilika ghafla ninaweza kwenda kumlaki Bwana mawinguni.

2Wakorintho 13:5 “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa”.

Naamini sisi sote tutaanza kuishi kama wanawali werevu. Na Bwana atusaidie.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312. Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments