Nini maana ya huu mstari “sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”

Nini maana ya huu mstari “sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”

Swali: Bwana Yesu alikuwa na maana gani kusema.. “sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”? Ni kwa namna gani atatupwa nje? Na ni kwanini atupwe nje na sio chini?


JIBU: Tusome huo mstari…

Yohana 12:31 “Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.

32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. ”

Kama ukichunguza vizuri hapo utaona anatumia neno “ATA” na si “ALI”.. yaani atatupwa na sio alitupwa au anatupwa..Ikionyesha kuwa ni kitendo kijacho ambacho bado hakijatokea..

Kumbuka tena hapo anasema atatupwa NJE, na sio atatupwa CHINI.. Shetani alishatupwa chini zamani sana, Kile kitendo cha yeye kuasi kule mbinguni biblia inasema kilimsababishia atupwe chini yeye pamoja na malaika zake (soma Ufunuo 12:7-10), Hivyo akawa ameganda tu hapa duniani kwenye giza nene, bila shughuli yoyote, wala tumaini lolote, akisubiria siku yake ya maangamizo ifike,apotee.. Mpaka sisi tunakuja kuumbwa, yeye alikuwa bado yupo hapa hapa anatazama tu, mwanadamu akimilikishwa kila kitu..

Lakini Adamu alipoasi, ndipo shetani akapata nafasi ya kuingia ndani ya ufalme ambao ulikuwa ni milki ya mwanadamu tu, Adamu akaiuza ile hati yake ya umiliki kwa shetani..Na tangu huo wakati shetani akapata nguvu akawa na mamlaka juu ya mambo mengi sana katika huu ulimwengu, akawa na uwezo hata wa kuwaendea wafu waliokufa(ikiwemo watakatifu) na kuzungumza nao kama alivyofanya kwa Samweli, akawa na uwezo hata wa kuzuia maombi ya watakatifu, yasimfikie Mungu …Yaani kwa ufupi japo watakatifu walikuwa wanalindwa na Mungu..lakini bado shetani alikuwa na uwezo fulani juu yao..

Sasa wakati ulipofika wa Mungu kuirudisha ile hati ya umiliki kwake, Ndipo akamletea mwanadamu aliyefanana na Adamu, ndiye Bwana wetu YESU KRISTO.. yeye alikuja kufanya kazi moja, na kazi yenyewe ilikuwa ni KUMFUKUZA SHETANI atoke ndani ya milki ya wanadamu..

Lakini si kwa wanadamu wote, bali wale tu watakaomwamini na kumpokea..

Na ndio maana sasa utaona Bwana Yesu anasema hapo.. sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”? Ikiwa na maana bado kitambo kifupi tu atakwenda kutupwa nje ya milki ya utawala wa watakatifu..Na tukio hilo lilikuja kutimia siku ile, pale KALVARI Bwana Yesu alipokufa na kuchukua funguo zote za uzima, pia na za kuzimu na mauti (Ufunuo 1:18).

Sasa tangu huo wakati hali yake shetani ikarudia kama mwanzoni alipokuwa pale Edeni kabla ya Adamu kuasi, akawa hana nguvu yoyote kwa wale watu waliomwamini Yesu na kuoshwa kwa damu yake, akawa hawezi kujiamulia tena kitu chochote juu yao, hawezi kuwaendea wafu na kuzungumza nao tena, hawezi kumdhuru mtu yoyote wa Mungu, ikiwa Mungu hajaruhusu.

Hivyo leo hii mtu aliyeokoka, hahitaji kuogopa wachawi, hahitaji kuogopa mapepo au majini, hahitaji kuwa na wasiwasi labda shetani atamuua, hahitaji kuwa na hofu labda maombi yake yamezuiliwa sehemu fulani hapo juu ya wakuu wa anga kama Danieli.. Sasa hivi shetani hawezi kufanya hivyo kwa mtu aliyeokoka kweli kweli.

Lakini kama upo nje ya Kristo..basi Maisha yako yapo hatarini..Wewe unapaswa uwe na hofu ya kila kitu, hukosei kuwaogopa wachawi, au majini, au wanadamu..kwasababu huna ulinzi wowote wa Mungu na shetani bado yupo ndani ya maisha yako, kila siku akikupangia njama za kukuangamiza..hivyo upo sahihi kabisa kuwaogopa kikweli kweli.

Ni neema za Mungu tu zinakushikilia ili utubu ndio maana upo hai.. Mpe Kristo Maisha yako kama hujampa, Uwe salama.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789 001312. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments