by Devis | 30 April 2025 08:46 am04
Swali: Katika kitabu cha Mathayo 17:4 Mtume Petro na wenzie waliwezaje kufahamu kuwa wale ni Musa na Eliya?
Jibu: Turejee habari hiyo kuanzia ule mstari wa kwanza..
Mathayo 17:1 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani;
2 akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru.
3 Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.
4 Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”.
Biblia haijaeleza kama Musa na Eliya walijitambulisha katika maono yale, ikiwa na maana kuwa kuna njia nyingine iliyowafanya Petro na wenzie kujua kuwa wale ni manabii Musa na Eliya na si wengine.
Sasa njia Pekee iliyomfanya Petro na wenzie kufahamu kuwa wale walikuwa ni Musa na Eliya na si wengine, ni UFUNUO WA ROHO MTAKATIFU.
Kama vile ufunuo wa Roho Mtakatifu ulivyomjia Petro kumhusu YESU.
Mathayo 16.15 “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?
16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”.
Umeona hapo?, aliyemwambia Petro kuwa YESU ni KRISTO tena ni MWANA WA MUNGU aliye juu sio YESU mwenyewe!, bali ni ufunuo wa alioupokea kutoka kwa Baba.
Na hiyo sio ajabu kwani walikuwa wameenda mlimani kuomba.. ni kawaida kwa watumishi wa MUNGU kupokea mafunuo ya mambo yaliyopo, au yajayo wanapokuwa katika maombi, hususani kama hayo ya mlimani.
Kwahiyo Mtume Petro na wenzie walipata ufunuo wa ujio au uwepo wa manabii hao wawili wakiwa katika maombi, utaona jambo kama hilo lilishatokea tena kwa Petro wakati yupo kwa Yule Simoni mtengenezaji wa ngozi wa kule Yafa, wakati ambapo Roho Mtakatifu alimfunulia alipokuwa katika maombi kuwa kuna watu watatu wanamwulizia, hivyo aende nao asiogope!, na kweli ikawa hivyo..
Matendo 10:17 “Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango,
18 wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
19 Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.
20 Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.
21 Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
Kwa namna hiyo hiyo, huenda Petro na wenzake walipokea ufunuo kuwa wale ni Musa na Eliya, labda walipokea ufunuo huo muda mchache kabla hawajawatokea, au wakati ule ule walipotokea.
Kikubwa tunachoweza kujifunza ni kuwa tuwapo katika uwepo wa MUNGU kama katika maombi, ni rahisi kupokea ufunuo wa Roho Mtakatifu kwani tunakuwa tupo katika roho, na mtu anapokuwa katika roho anayatambua mambo yote ya rohoni pasipo kuambiwa!
Hivyo ni muhimu sana kuwa waombaji, na wasomaji wa Neno la MUNGU, endapo akina Petro wangekuwa si watu wa kusoma maandiko, ni dhahiri kuwa wasingemjua Musa wala Eliya na hiyo ingezuia Roho kuwafunulia watu hao, kwani Roho Mtakatifu anamfunulia mtu kitu ambacho kinahusiana na Neno la MUNGU.
Je na wewe ni mtu wa kudumu uweponi mwa MUNGU? Je KRISTO YESU?..Je unao uhakika kwamba akirudi unaenda naye?
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Kwanini Eliya afunge Mbingu miaka mitatu na nusu? (1Wafalme 17:1)
TUKIO LA MUSA NA ELIYA KUMTOKEA BWANA, LIMEBEBA UJUMBE GANI?
Je! Tutatambuana tukifika mbinguni?
Je Mariamu alikuwa na umri gani alipochukua mimba ya Bwana YESU?
Kwanini Mungu alimchagua Musa, na si mtu mwingine?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/04/30/je-petro-na-wenzie-walitambuaje-kuwa-wale-walikuwa-ni-musa-na-eliya/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.