by Devis | 6 May 2025 08:46 pm05
Jina la Mwokozi YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze Biblia Neno la MUNGU wetu, lilio taa na mwanga wa njia yetu.
Unapofika wakati MUNGU wetu wa UPENDO, anapotaka kututoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa kuondoa matatizo makuu yanayotishia maisha yetu, basi huo haondoi tu chanzo cha tatizo bali pia na mkondo wake wote anauondoa.
Ili tuende pamoja, hebu turejee wakati Bwana YESU anazaliwa, maandiko yanasema Herode alitafuta kumwua mtoto YESU, lakini Yusufu na Mariamu kupitia onyo la Malaika wa Bwana waliambiwa wakimbilie Misri ili Herode asimwue mtoto.
Lakini jambo la ajabu ni kwamba baada ya Herode kufa, biblia inatuambia hakufa peke yake bali na wengine waliokuwa na nia kama ya kwake ya kumwangamiza mtoto, ambao biblia haijawataja majina yao.
Mathayo 2:19 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20 akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana WAMEKUFA WALIOITAFUTA ROHO YA MTOTO”.
Hapo anasema “WAMEKUFA”..na si “AMEKUFA” Maana yake hakuwa mmoja bali wengi, maana yake si Herode peke yake, walikuwepo na wengine waliokuwa na nia kama ya Herode…huenda wakuu wa majimbo waliofanya kazi na Herode, au makuhani au raia wa kawaida.
Kwahiyo waliokuwa wanaitafuta roho ya mtoto, hawakuwa wachache, bali wengi (ulikuwa ni mkondo) na wote walikufa..Herode alikuwa tu ni kichwa cha pweza, lakini mikia ilikuwa mingi!.
Endapo Yusufu na mtoto wangeendelea kubaki Bethlehemu walikuwepo wapelelezi wengi hivyo taarifa kuhusu mtoto zingemfikia Herode haraka, hata baada ya yale maangamizi kupita bado hatari ilikuwepo, kwahiyo suluhisho ni wote wafe kwanza ndipo usalama uwepo wa Bwana YESU kurudi Israeli.
Sio hilo tu, utakumbuka pia ile habari ya Malkia Esta, wakati Hamani, adui wa wayahudi alipoandika waraka wa wayahudi wote kuuawa, katika siku moja!.. kama ni mwanafunzi wa Biblia utagundua kuwa si Hamani peke yake aliyekuwa adui wa waisraeli kwa wakati ule!, bali walikuwepo wengine wengi katika kila jimbo la mfalme Ahasuero, Hamani yeye alikuwa ni kichwa tu cha pweza kama alivyokuwa Herode!.
Ndio maana mambo yalivyoharibika kwa Hamani, hakufa peke yake bali na maadui wote wa wayahudi katika ufalme wote.
Esta 9:1 “Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile ADUI ZA WAYAHUDI walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia;
2 siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa hofu yao imewaangukia watu wote. …….
5 Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia.
6 Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza…………
16 Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, WATU SABINI NA TANO ELFU; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono”.
Watu zaidi ya Elfu 75 walikufa pamoja na HAMANI, ingawa kwa haraka tunaweza kuona kama aliyekuwa adui wa wayahudi alikuwa ni Hamani peke yake, kumbe hakuwa peke yake bali ulikuwa ni mkondo mkubwa ibilisi alioutengeneza kwa muda mrefu!.
Hivyo ukiona mtu mmoja mashuhuri anafanya vita na wewe katika vitu vilivyo sahihi unavyovifanya basi fahamu kuwa hayupo peke yake bali upo mkondo wa ibilisi nyuma yake!, na wakati wa MUNGU ukifika huwa anakiondoa chanzo na mkondo wake, ili amani irejee..
Na MUNGU anapokiondoa chanzo na mkondo wake si lazima awaue maadui zako kama inavyodhaniwa na wengi, La! Kifo chaweza kuwa njia ya mwisho kwa MUNGU wetu dhidi ya tunaowaona kama maadui zetu,
Lakini badala yake MUNGU anaweza kuwahamisha na kuwapeleka mbali au kukuhamisha wewe ukae mbali nao sehemu salama, au anaweza kuwabadilisha na kuwafanya watu wazuri (wakamrudia MUNGU)..na lile tatizo likawa limeondoka, na hambadilishi yule chanzo tu peke yake, bali na mkondo mzima, Ndio hapo unashangaa watu waliokuwa wanakuchukia na kukupiga vita sasa wanakupenda, waliokuwa maadui zako sasa mnaishi kwa amani n.k
Swali: Niombe maombi gani ili Mungu aondoe chanzo cha matatizo na mkondo wake?
Badala ya kufikiri namna ya kuomba, fikiri kuzitengeneza njia zako mbele za MUNGU, njia zako zinaponyooka mbele za MUNGU (kwa kuishi maisha ya kumpendeza MUNGU), basi MUNGU anashughulika na vyanzo vyote na mikondo yake, kwa kukurejeshea amani..
Mithali 16:7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye”.
Lakini usiponyoosha njia zako kwa MUNGU, na ukategemea maombi tu peke yake, bado safari itakuwa ndefu, Maisha yetu yanajalisha sana katika kuelezea vyanzo vya matatizo tuliyonayo, yakizidi kuwa safi mbele za MUNGU ndivyo matatizo yatakavyozidi kuwekwa mbali.
Je umempokea YESU?.
Unao uhakika Bwana YESU akirudi leo unakwenda naye?
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Ni kwa namna gani Bwana YESU alikula Siagi na Maziwa? (Isaya 7:15)
Kuonja ni kufanya nini? (Kutoka 15:25).
NI NANI TUNAPASWA TUMWONE ZAIDI KILA TUSOMAPO BIBLIA?
Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?
NIONYESHE MARAFIKI ZAKO, NIKUAMBIE TABIA ZAKO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/05/06/mungu-wetu-huondoa-chanzo-pamoja-na-mkondo-wake/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.