Kwanini Roho Mtakatifu amzuie Paulo kuipeleka injili Asia? (Matendo 16:6-7).

by Devis | 5 June 2025 08:46 am06

Jibu: Turejee Matendo

Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, WAKIKATAZWA NA ROHO MTAKATIFU, WASILIHUBIRI LILE NENO KATIKA ASIA.

7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,

8 wakapita Misia wakatelemkia Troa”.

Biblia haijataja sababu za moja kwa moja kwanini Roho Mtakatifu awazuie wasiingie Asia kuhubiri injili lakini zifuatazo zinaweza kuwa sababu za Roho Mtakatifu kuwazuia Paulo na wenzake wasiingie hiyo miji kuhubiri injili.

   1. WAKATI WA INJILI KWA HIYO MIJI ULIKUWA HAUJAFIKA.

Kila mahali pana wakati wake wa kuhubiri injili kulingana na mapenzi ya Mungu, kwamfano kuna wakati ambao injili ilikuwa haijaruhusiwa kuhubiriwa kwa watu wa mataifa isipokuwa wayahudi tu peke yao, na kipindi hiko ni kile ambacho Bwana YESU alikuwa yupo bado duniani.

Mathayo 10:5 “Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Maneno hayo ya Bwana Yesu yanaonyesha kuwa wakati wa injili kwa watu wa mataifa ulikuwa haujafika, lakini haikumaanisha kuwa Mataifa hawakuwa katika mpango wa Mungu wa kupokea Injili, walikuwepo lakini muda wao ulikuwa bado haujafika.

Na hapa katika Asia ni hivyo hivyo, huwenda muda wao wa kufikishiwa injili ulikuwa bado.

    2. WATUMISHI WENGINE WALIKUWEPO WAKIHUBIRI INJILI.

Kama muda wao wa kupokea Injili ulikuwa umefika na bado Roho Mtakatifu akawazuia akina Paulo kufika miji hiyo, sababu nyingine ni kwamba labda walikuwepo watumishi wengine wakihubiri katika hiyo miji, hivyo hakukuwa na haja ya akina Paulo kwenda huko tena wasije wakajenga juu ya msingi wa wengine kama Neno la Mungu linavyosema katika Warumi 15:20.

Warumi 15:20 “kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine”

    3. WATUMISHI WENGINE WAMEKUSUDIWA KWENDA KUHUBIRI KATIKA HIYO MIJI.

Na kama hakukuwa na watumishi wengine waliokuwa wanahubiri katika miji hiyo, basi sababu nyingine ya Roho Mtakatifu kumzuia Paulo na wenzake kufika huko Asia huwenda ni kwasababu Roho Mtakatifu alikuwa amepanga/kusudia watumishi wengine ndio wakahubiri kwenye hiyo miji mbali na Paulo na wenzake.

Kikawaida Roho Mtakatifu ndiye anayepanga watu na mahali watakapokwenda..Paulo asingeweza kwenda miji yote peke yake, ni wazi kuwa ipo miji mingine ilikusudiwa kupelekewa injili na watumishi wengine/mitume.

    4. WALIIKATAA INJILI.

Hii yaweza kuwa sababu ya mwisho ya Roho Mtakatifu kuzuia injili isiingie Asia kupitia Paulo na wenzake… Inawezekana Roho Mtakatifu alishatanguliza watu huko waliohubiri Neno la Mungu lakini wakaikataa ile injili.. na matokeo yake ni kufungiwa dhambi sawasawa na  Yohana 20:22-23..

Yohana 20:22 “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.

23 Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

Kufungiwa dhambi kunakuja pale ambapo Neno la Mungu linahubiriwa kwa watu na wale watu wanalikataa kwa makusudi na hata kuwaua au kuwafukuza watumishi wa MUNGU, inapotokea wale watumishi wanakung’uta mavumbi kwenye miguu yao na kuondoka hapo wanakuwa wameufungia dhambi ule mji au mtaa, matokeo yake ni kwamba Roho Mtakatifu hawezi tena kupeleka wahubiri hapo mahali, wale watu watabaki vile vile kwasababu walishamkataa Roho Mtakatifu.

Mathayo 10:14 “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, KUNG’UTENI MAVUMBI YA MIGUUNI MWENU.

15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule”.

Tunachoweza kujifunza ni kuwa Injili sio kitu kinachoweza kupatikana kila wakati, upo wakati ambapo Neema ikishaondoka mahali hairudi, au hata ikirudi yaweza kuchukua muda sana, hivyo hatuna budi kuiheshimu sana Neema ya Mungu.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Paulo, alihimiza kusikiliza nyimbo za kidunia kulingana na Matendo 17:28

Paulo aliwapaje watu karama ya rohoni?

Je ni sawa kuukubali udhaifu kama mtume Paulo alivyojisifia kwa huo? (2Wakorintho 12:9-10)

Kwanini Paulo, alihukumu wakati hukumu hairuhusiwi?

Paulo alikuwa anamaanisha nini kusema “Mnatenda vema kuvumiliana naye” (2Wakorintho 11:4).

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/05/kwanini-roho-mtakatifu-amzuie-paulo-kuipeleka-injili-asia-matendo-166-7/