by Devis | 1 July 2025 08:46 am07
Bwana Yesu alitutahadharisha kuwa karibia na kurudi kwake, tabia za watu zitabadilika na kukaribia kufanana na zile za watu wa Nuhu na Lutu.
Luka 17:26 “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.
27 Walikuwa WAKILA NA KUNYWA, walikuwa WAKIOA NA KUOLEWA, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.
28 Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa WAKILA NA KUNYWA, walikuwa WAKINUNUA NA KUUZA, wakipanda na kujenga;
29 lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote.
30 Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu”.
Sasa ishara hii ya watu kununua na kuuza, kuoa na kuolewa na kula na kunywa ilikuwa inalenga makundi mawili, kundi la kwanza ni WATU WASIOMJUA MUNGU, na kundi la pili ni WATU WANAOMJUA MUNGU, hetu tuanze tathmini ya kundi moja baada ya lingine.
1. WATU WASIOMJUA MUNGU.
Kipindi cha Nuhu na Sodoma na Gomora walikuwa wakila kwa anasa, na kunywa kwa kulewa, na wakamsahau Mungu, lakini pia walikuwa wakioa na kuolewa kwa ndoa haramu (maana yake za watu waliocha waume zao au wake zao, au wa jinsia moja) vile vile walikuwa wakinunua vitu haramu na kuuza vitu haramu kwa njia zisizo halali, ikiwemo dhuluma na rushwa, na utapeli na wakamsahau Mungu, hivyo gharika ikawachukua wote.
Ndicho kinachoendelea sasa kwa watu wengi walio nje ya wokovu, rushwa ni kitu cha kawaida kwao, kuoana kiholela ni kitu cha kawaida, (yaani mtu kuoa/kuolewa leo na kesho kuachana na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine ni jambo la kawaida), hali kadhalika kuhudhuria kwenye karamu za ulafi na kula bila kiasi pamoja na kulewa ni mambo ya kawaida kila mahali, ndio maana utaona Bar ni nyingi kila kona.
Lakini hiyo ni ishara kwa watu wasiomjua Mungu, ambayo kiuhalisia pia inatangaza kwamba tunaishi katika siku za mwisho, lakini hebu tuangalie kwa upande mwingine kwa watu wa Mungu (kanisa.)
2. WATU WANAOMJUA MUNGU (Kanisa)
Utauliza je! Watu wanaomjua Mungu pia wanaangukia katika hili kundi la kula na kunywa, kuoa na kuolewa, kununua na kuuza?.. Jibu ni ndio!.. sasa labda utauliza ni kwa namna gani?.. hebu tusome maandiko yafuatayo..
Luka 14:16 “Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,
17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.
18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, NIMENUNUA SHAMBA, SHARTI NIENDE NIKALITAZAME; tafadhali unisamehe.
19 Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.
20 Mwingine akasema, NIMEOA MKE, na kwa sababu hiyo siwezi kuja”
Nataka tuone huo udhuru hao watu walioutoa!.. Kumbuka hao ni waalikwa, maana yake watu wenye mahusiano na mwenye harusi, na huo ni mfano ambao Bwana aliutoa kuhusu karamu ya mwanakondoo itakayofanyika mbinguni baada ya unyakuo,
Kwamba sasa anawaaalika watu, lakini waalikwa (yaani watu wanaomjua Mungu) wanatoa udhuru!, kwamba Nimeoa Mke, wengine nimenunua shamba sharti nikalitazame!.. Je huoni haya ndio yale yale Bwana aliyoyasema kwamba siku za mwisho watu watakuwa wakioa na kuolewa, na kununua na kuuza?
Kumbe ishara hii pia inatimia kwa watu wa Mungu!.. watu wasiomjua Mungu wao wataoana ndoa haramu, watanunua vitu haramu na kuuza kwa njia haramu.. lakini watu wa Mungu wataoa kihalali, na kununua na kuuza kihalali lakini watavifanya hivyo kuwa udhuru utakaowazuia kumsogelea MUNGU zaidi.
Hii ni hali halisi kabisa ya kanisa la leo!.. Asilimia kubwa ya tunaojiita wakristo, shughuli zimetusonga kiasi cha kuupunja muda wa Mungu, hatuombi tena kwasababu ya wingi wa kazi, hatuifanyi tena kazi ya Mungu kwasababu ya majukumu ya kifamilia na ndoa!, hatukusanyiki tena pamoja na wengine kwasababu ya mialiko mingi tuliyonayo ya kula na kunywa!..
Je unajua matokeo yake ni nini?.. Hebu tuendelee na mistari ile..
“20 Mwingine akasema, NIMEOA MKE, na kwa sababu hiyo siwezi kuja,
21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.
22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.
23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.
24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.
Matokeo yake ni kwamba Neema tuliyoipewa watapewa watu wengine , wote wenye kuwa na udhuru mwingi kwa Bwana wapo katika hatari ya kukosa kuingia mbinguni, wapo katika hatari ya kukumbana na gharika ya mwisho ya moto kulingana na Biblia.
Je wewe upo kundi gani?.. Unakula na kunywa kwa anasa au kihalali?, na kama kihalali je hiyo kwako ni udhuru wa kumtafuta Mungu?.. je wewe unanunua na kuuza kiharamu au kihalali?.. na kama ni kihalali je hiyo kwako ndio udhuru wa kutojitoa kwa Mungu?.. majibu yapo kwako na kwangu.
Bwana atusaidie tusiwe watu wa udhuru, bali tumtumikie Bwana kwa moyo wote, kwani hiyo ni amri tuliyopewa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je mtu anaweza kubatizwa mara mbili?
Je tumepewa kujua nyakati na majira ya kurudi kwa Bwana au la?.
KUWA MAKINI, HATUA ZA UNYAKUO ZINAENDELEA.
MGAWANYIKO WA ISHARA ZA UJIO WA BWANA YESU KRISTO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/01/walikuwa-wakinunua-na-kuuza-wakioa-na-kuolewa-kama-ishara-ya-kanisa/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.