Mungu huwa anasema nasi mara nyingi mioyoni mwetu, lakini huwa hatuzingatii na mwisho wake tunaingia katika matatizo.
Matokeo ya kutozingatia sauti ya Mungu ni makubwa, hebu tujifunze kwa mwana mpotevu, aliyeomba urithi kwa Baba yake.
Luka 15:11 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.
13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati”.
14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
17 ALIPOZINGATIA MOYONI MWAKE, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako”
Nataka tuone huo mstari wa 17, unaosema.. “ALIPOZINGATIA MOYONI MWAKE”.
Maana yake tayari sauti ya MUNGU ilikuwa imeshaanza kumsemesha muda mrefu sana moyoni mwake, kwamba njia anayoiendea sio sahihi, mambo anayoyafanya ni mabaya na hivyo ageuke, lakini hakuwa ANAZINGATIA hiyo sauti.
Na kwa kadiri alivyokuwa anaipuuzia ndivyo mambo yalivyozidi kuwa mabaya, mpaka siku alipoamua kuizingatia.
Inawezekana sauti ya MUNGU inasema nawe moyoni mwako muda mrefu (dhamiri inakushuhudia), usiiendee hiyo njia, usiendelee kufanya hayo unayoyafanya, lakini huzingatii, leo anza kuzingatia sauti ya MUNGU, na geuka acha hiyo njia, mrudie Baba yako, mpe Mungu moyo wako…
Mithali 23:26 “Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu”.
Zingatia sauti inayokuambia UOMBE, zingatia sauti inayokuambia ufunge, Zingatia sauti inayokuambia usome Neno, zingatia sauti inayokuambia Usamehe, zingatia sauti inayokuambia mtumikie MUNGU, wakati mwingine zingatia hata sauti unayokuambia uhame hapo ulipo…
Matokeo ya kuikaidi hiyo sauti ni mabaya, ni kama hayo ya Mwana mpotevu na yale ya Yona.
Bwana atusaidie.