KUONGOZA WATU WENYE SHINGO NGUMU.

by Nuru ya Upendo | 7 October 2025 08:46 pm10

Haya ni mafundisho maalumu kwa viongozi aidha wachungaji, au wasimamizi ndani ya kanisa..Maadamu una kundi la watu aidha 2-3 au zaidi la kuwasimamia, basi mafunzo haya yatakusaidia sana.

Kutoka 32:9-10

[9]Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu 

[10]basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. 

Mungu alipomuita Musa kwenda kuwaokoa watu wake, alijua asili Ya hao watu watakuwa ni wa namna gani. Pengine Musa alidhani anawaokoa watu ambao ni wema sana, watulivu, na wapole.

Lakini mambo hayakuwa kama hivyo, licha ya kuona miujiza mikubwa namna ile, bahari kupasuka, mana kushuka Mbinguni, miamba kutoa maji, nguzo ya moto kuwaongoza usiku kila siku…

Bado walitengeneza sanamu za ndama na kusema hii ndio miungu yetu iliyotutoa Misri tuiabudu..walinung’unika, walimsengenya kiongozi wao, waliasi na kujiundia Makundi..Ni watu ambao walikuwa ni wagumu kuongoza, wazito kutii na wapesi kulalamika.

Ni vema kujua kuwa kila kiongozi wa kweli kuna siku atapitia kama Musa alivyopitia.. 

Ikifikia hatua hii wengi wanasema kama utumishi ndio huu ni heri niache, kama naonyesha fadhila zote hizi kinyume chake narudishiwa masengenyo na uasi, ni heri niache…

Ukifikiri hivyo bado hujawa kiongozi, Mungu alijua asili yao kwamba ni watu wenye shingo ngumu..alijua Yuda ni msaliti lakini bado alimpatia mwanae, amchunge.

Kutoka 32:9-10

[9]Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu 

Hao hao bado aliwaokoa na akataka wachungwe..

Shingo ngumu ni mtu wa namna gani?. Ni mtu anayefananishwa na ng’ombe ambaye hataki kufungwa Nira na Bwana wake…shingo inakuwa ngumu kuvishwa nira..

Hii ni aina ya watu ambao Hawana utii, hawachungiki, hata waone miujiza mikubwa namna Gani, hata wasaidiweje, si rahisi kuacha tabia zao za usengenyaji, wizi, uasi. Kiburi N.k.

Lakini bado Mungu anawaacha chini ya mchungaji waangaliwe..

Musa alikutana na waabudu sanamu, wanung’unikaji, Na wasahaulifu wa fadhili za Mungu…

Lakini alifanyaje?

Hata pale ambapo Mungu alitaka kuwaangamiza Musa aliwaombea. Alisimama kufanya upatanisho kwa ajili yao.

Ni ujumbe gani tunapewa?

Kiongozi wa kweli badala ya kughahiri kumchunga kondoo wake humwombea kwa bidii ili Bwana amponye asipotee kabisa kwenye dhambi.

Kiongozi wa kweli, huwa tayari hata kupoteza maisha yake kwa kondoo wake.. Musa alisema..

Kutoka 32: 32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. 

Uongozi sahihi sio Kuongoza Watu wakamilifu, lakini kuongozo Watu dhaifu Kwa Mungu mkamilifu.

Uongozi Sahihi huweka katika uwiano sahihi “neema na kweli”

Ni vema kufahamu pia si kila wakati Musa alikuwa anasimama kuwatetea Waovu, hapana wakati mwingine aliruhusu upanga wa Mungu upite, Ili dhambi iogopwe…utakumbuka wakati ule walipotengeneza Sanamu ya ndama, na hasira Ya ki-Mungu ilimvaa Musa, ndipo Akazivunja zile mbao mbili, kisha awaita watu walio upande wa Bwana wamfuate, Na wale waliosalia waliadhibiwa vikali kwa mauti.

Dhambi iwapo kanisani, haipaswi kuvumiliwa..Kutoa adhabu na wakati mwingine kuwaondoa wale wabaya ndani ya kundi ili lisiendelee kuharibiwa..

Lakini katika yote wewe kama kiongozi, huna budi kujifunza Uvumilivu, kuwaombea kondoo wako, na kuwa mpole, lakini pia kushughulika na dhambi Vikali katika nyumba ya Bwana. 

Lakini kumbuka ijapokuwa Ni kazi, yenye mapito mengi ya masumbufu na maumivu Lakini thawabu yake na faida yake haifananishwi na gharama ulizoingia.. Hivyo penda kuchunga watu wa Mungu…Ndio heshima ya juu ya upendo kwa Mungu wako.

Mithali 14:4

[4]Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe; Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi. 

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

TOFAUTISHA KATI YA MAFUNDISHO YA YESU, NA YA WAANDISHI.

MHESHIMU MCHUNGAJI WAKO.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/10/07/kuongoza-watu-wenye-shingo-ngumu/