KAMA NISIPOKUTAWADHA, HUNA SHIRIKA NAMI

by Nuru ya Upendo | 6 January 2026 08:46 am01

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima

Tengeneza picha Mungu amekutokea amesimama mbele yako, wakati ukiwa na mawazo ya kumwangukia chini umsujudie, unashangaa yeye moja kwa moja anakuwa wa kwanza kuinama na kukusafisha miguu yako…

Hivi utajisikiaje? Ukweli ni kwamba hutajisikia huru hata kidogo, kwa ufupi hutakubali kitendo hicho kifanywe na yeye kutoka na ukuu wake, na heshima yake iliyozidi vyote, ni sawa na uone baba amemnunulia mtoto wake zawadi halafu yeye ndio anayekuwa wa kwanza kumshukuru mtoto, tena kwa kumwinamia..ni wazi kuwa hilo halijakaa sawa, au mtu aliyeibiwa mali zake nyingi, halafu amekutana na aliyemwibia badala ya mwenye mali kungojea kuombwa msamaha, yeye ndio anajionyesha kama ni mkosaji kwake…unaona ni jambo ambalo halina uhalisia, halikubaliki kifikra hata kidogo…

Kwa namna ya kawaida hali kama hizi akitendewa mtu hawezi kuridhia…lakini Mungu anatutendea sisi na anasema kama hutakubali kutendewa naye hivyo kamwe hutuna ushirika naye.

Ndicho kilichotokea kwa mitume na Petro. Wakati ule walipomwona Bwana Yesu, anashika kitambaa na maji kisha akaanza kuwaosha na kuwapangusa miguu yao…Petro hakuweza kuridhia akasema Bwana hutanitawadha miguu kamwe. Lakini Yesu akamwambia usipokubali huna ushirika nami.

Yohana 13:8

[8]Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. 

Hii ni kufunua nini…

Ni lazima tumjue Kristo, ni kweli anasimama kwetu kama mfalme, kama Bwana, kama Mungu…tunamwabudu…lakini pia anasimama kama mtumishi wetu..Ni jambo ambalo hatuwezi kuingia akilini  lakini ndivyo alivyo, amependa yeye kuwa hivyo kwetu.

Ni mfalme mwenye taji la kifalme lakini wakati huo huo pia mfalme aliyebeba kitambaa cha kuwasafisha watu miguu.

Hiyo ndio sifa ya ufalme wake. Amesimama kama muumba wetu tumwabuduye, lakini pia anatutumikia, katika kutuponya magonjwa yetu, kutulisha, kutuvisha, kutuombea, kutulinda, kutufuta machozi, na kuchukua mizigo yetu mfano wa punda na hata kufanya mambo ambayo sisi hatuwezi stahimili akitufunulia yote kwa jinsi anavyojishusha na kujishughulisha sana na mambo yetu…. Na mfano tukitataa yeye asituhudumie hivyo anasema wazi kuwa hatuna ushirika naye.

Maana yake ni fahari yake kututendea hayo, wala yeye hayahesabu kuwa ni kitu.

Anatufundisha nini?

Tuwe watumishi pia wa wengine kwa namna hiyo, kama yeye alivyo kwetu…kujitoa kwake sio kutimiza wajibu bali ni fahari yake ambayo isipokubaliwa inaharibu moja kwa moja mahusiano.

Kumsaidia mpendwa mwenzako iwe ni furaha..kujinyenyekeza kwake isiwe ni sababu za umri au cheo bali fahari..Kumwombea iwe ni fahari yako, kumsikiliza iwe ni furaha yako…hivyo ndivyo Bwana anavyotaka.. na ndivyo alivyomwambia Petro.

Yohana 13:12-17

[12]Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? 

[13]Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. 

[14]Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. 

[15]Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. 

[16]Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. 

[17]Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. 

Neema ya Bwana itusaidie.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WEWE NI ZAO LA MAHUSIANO NA USHIRIKA.

USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU UKAE NANYI NYOTE.

WENGINE WANAKESHA KWAAJILI YAKO.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/01/06/kama-nisipokutawadha-huna-shirika-nami/