by Nuru ya Upendo | 22 January 2026 08:46 pm01
Kama tunavyofahamu katika maandiko Mitume walipofika mji wa Thesalonike kwa ajili ya injili, na kukutana na wenyeji wa mji ule, na kusikia walichokihubiri maandiko yanatuambia walipiga kelele sana na kusema maneno haya;
“Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako”
Matendo ya Mitume 17:6
[6]na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,
Ulishawahi kutafakari kwa ukaribu maneno hayo walichokimaanisha?
Wanasema;
Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,
Maana yake ni kuwa ulimwengu na wao, ni kama vitu viwili tofauti…
Wamefika na huku pia….yaani wameshaushinda ulimwengu wanakuja na huko kwao kumalizia walichokifanya kule..
Hii ikiwa na maana…mitume walishapata ushindi kabla hata ya kufika maeneo yote…
Kuna mahali pajulikanapo ulimwenguni ambapo tayari walishapashinda.
Sasa huo ulimwengu ni upi?
Chukulia mfano wa dunia ya sasa.. kuna usemi wasemao nchi za Afrika ni dunia ya tatu.. ijapokuwa wote tupo kwenye sayari moja, ujulikano dunia, lakini uhalisia dunia zipo tatu…Zile nchi zilizoendelea sana…Kama vile Marekani, urusi, China, ufaransa..ni dunia ya kwanza… na zile zilizo katika uchumi wa kati ni dunia ya pili na hizi maskini ni dunia ya tatu..
Sasa ikitokea mtu akayapiga hayo mataifa makubwa na kuyateka, maana yake huyo mtu ameiteka dunia, ameipindua dunia…..hata kama hajapigana na haya mengine madogo..lakini ikiwa nguvu zake zimewashinda wale basi hawa wengine ni maji tu.
Vivyo hivyo waamini wa wakati ule walionekana, wanamapinduzi wakubwa sana..kwasababu ushindi wao ulianzia kwenye vichwa.
Sasa huu ulimwengu ni upi?
JIBU: Ulimwengu wa Roho.
Zamani zile dini zilijulikana kama msingi mikubwa sana inayosukuma mielekeo ya mataifa.. hivyo Kristo alipokuja aliweza kuvunja misingi ya imani potofu na dhaifu kuanzia pale pale Israeli mpaka miisho ya dunia. Alileta Nuru duniani ambayo giza lolote halikuweza kulishinda..
Yohana 1:4-5
[4]Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.
[5]Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Ndio maana kipindi cha injili utaona Wayahudi wengi waliokoka, wapagani wengi wakaacha miungu yao..wakaichoma moto, utaona hata kule Efeso mungu mke aliyeabudiwa ulimwenguni kote (Matendo 19:27), mitume walipofika habari yake ikaishia pale pale, tofauti na zamani manabii walishindana sana na mabaali lakini hawakuweza kuyashinda..kwasababu hakukuwa na nguvu ya kutosha ya kumshinda mkuu wa ulimwengu huu(shetani)
Yohana 16:11
[11]kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
Hivyo ulimwengu wa roho uligeuzwa juu chini, mapepo yaliwakimbia wengi, watu walifunguliwa kwenye vifungo vya giza..makaburi waliwaachia wafu..kila siku watu waliongozeka kumjua Mungu…na kuachana na dhambi.
Matendo 19:19-20
[19]Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.
[20]Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.
Huu ndio ulimwengu sugu uliopata tiba…ulimwengu wa giza, kama kichwa cha mifumo yote mibovu ya dunia…uliwekwa chini…
Hivyo wale watu walipoona imani za watu zinageuzwa kwa kasi hata za maakida wakubwa,(Matendo 13:7-12) majemedari, watu wenye vyeo, wake kwa waume, nao pia wanaigeukia imani..wakatambua ya kuwa kila kitu kimekwisha sasa, sisi ni masalia..tu.
Walijiona kama mapanzi, ni sawa na wana wa Israeli walipoweza kuliangusha taifa la Misri, hata kabla ya kufika Yeriko, Wale watu wenyewe walishajiona kama mapanzi..Kwasababu kichwa cha ulimwengu kimeshaangushwa.
Vivyo hivyo hata sasa, ni lazima tujue kuwa sisi tuliomwamini Yesu…tayari tumeshaupindua ulimwengu kwa Injili iliyokwisha fika kuzimu kwenye kiti cha enzi wa shetani…
Hakuna chenye nguvu ya kutuzuia sisi tena, sisi ni watawala wa dunia.
Wanasiasi, hawawezi kutuzuia, wanadamu hawawezi kutusimamisha..wao ni kama mapanzi tu kwetu…
Hatuna budi kuuinua ujasiri wetu wote…tufikie mataifa yote kuhubiri injili kwasababu ulimwengu tayari tumeshaupindua…hatuhitaji kwenda tena kuupindua..sisi ni kumalizia tu masalia. Unasubiri nini usiamke kuihubiri injili? Amka sasa…
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
PELEKA INJILI KOTE KOTE KWA SADAKA YAKO.
KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/01/22/watu-hawa-walioupindua-ulimwengu-wamefika-huku-nako/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.