by Nuru ya Upendo | 28 February 2026 08:46 pm02
Jina la Mwokozi Mkuu YESU KRISTO, libarikiwe.
Kabla ya kusogea mbele kujifunza ujumbe huu, ni vizuri tukarejea sehemu ya kwanza ya ujumbe huu inayosema “FAHAMU JINSI YA KUPATA MAMLAKA YA DAMU YA YESU”
Katika ujumbe huo tuliona ni kwa namna gani tunaweza kuwa na uhalali wa kuitumia Damu ya YESU, ikiwa tutakuwa ndugu zake, fuatilia ujumbe huo hapa >>>FAHAMU JINSI YA KUPATA MAMLAKA YA DAMU WA YESU.
Sasa kuna umuhimu mkubwa sana wa “KUYAJUA” na “KUYATENDA MAPENZI YA MUNGU”.. Kwani hiyo ndio tiketi ya ‘KUMWONA MUNGU’ siku ya mwisho.
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni”.
Na tena Neno la Mungu linatusisitiza kutafuta kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa bidii muda tuliobakiwa nao hapa duniani..
1Petro 4:2 “Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali KATIKA MAPENZI YA MUNGU, WAKATI WENU ULIOBAKI WA KUKAA HAPA DUNIANI”.
Sasa Mapenzi ya MUNGU yamegawanyika katika sehemu kuu Mbili.. 1) Mapenzi ya Mungu kwa Mtu binafsi, na 2) Mapenzi ya Mungu kwa watu wote.
Ni lazima tufanya Mapenzi ya Mungu katika migawanyiko yote hii miwili.. ni kama sheria, zipo sheria ulizojiwekea wewe, na zile ulizowekewa na nchi, ni lazima zote iziishi. Hali kadhalika yapo mapenzi ya Mungu kwako wewe au mimi binafsi, na yale Mapenzi ya Mungu kwa watu wote.. hebu tutazame moja baada ya lingine.
1. MAPENZI YA MUNGU KWA MTU BINAFSI.
Hili ni kusudi ambalo Mungu anataka ulifanya ukiwa hapa duniani kupitia karama, au nafasi uliyopewa na MUNGU. Ni lazima ufahamu duniani umeitiwa kufanya nini wewe kama wewe.. Kama umeitwa kuwa Askofu, au mwalimu, au mchungaji, au nabii, au mtume, au mwinjilisti, au mtu mwenye kukirimu, au mshauri, au mwingine yoyote katika nafasi yoyote ile kwa ajili ya ufalme wa MUNGU.
Usipojua mapenzi ya MUNGU ni yapi ni ngumu kuishi kwa kumpendeza MUNGU, kwasababu utafanya jambo lisilompendeza Mungu, utaishi mahali pasipopendeza Mungu, utaenda katika njia ambayo Mungu hajaikusudia juu yako.
Na mapenzi ya Mungu yanatofautiana kwa mtu na mtu.. anavyotembea mwingine si sawa na utakavyotembea wewe,..lakini wewe umekusudiwa njia yako tofauti na mwingine, ni lazima uijue.
Sasa unajuaje kusudi/mapenzi ya Mungu kwako?
Njia ya kwanza ni ya kumpokea YESU na kutubu dhambi.. baada ya hapo, kuomba huku ukidumu katika kumpenda MUNGU, Roho Mtakatifu atakuongoza katika kusudi lake, na ukikaa katika kusudi/mapenzi ya MUNGU, utaona amani ya kiMungu ndani yako, na pia mafanikio katika utumishi huo.
Na utakapojaribu kuacha njia hiyo utaona mambo hayaendi kabisa..hapo utajua kuwa ulikuwa kwenye njia sahihi ya mapenzi ya MUNGU.
2. MAPENZI YA MUNGU KWA WATU WOTE.
Baada ya kujua mapenzi ya MUNGU kwako ni yapo, kwamba unapaswa ufanye nini, wakati mwingine uishi wapi, au utembee na nani safari bado haijaisha ni lazima pia uyajue mapenzi ya MUNGU kwa watu wote, aliyoyakusudia kila mtu ayaishi.
Sasa hayo mapenzi ya MUNGU kwa wote ni yapi?.. Tusome maandiko yafuatayo..
1Wathesalonike 4:3 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;
4 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;
5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu”.
Kumbe mapenzi ya Mungu kwetu sote ni KUTAKASWA (Yaani utakatifu), na TUEPUKANE NA UASHERATI (wa mwilini na rohoni) na TUJUE KUIWEZA MIILI YETU KATIKA UTAKATIFU na HESHIMA.
Hapa ndipo shetani anapofumba macho wengi.. ni kweli tumejua mapenzi ya MUNGU kwetu ni kumtumikia, kumwimbia, kuhubiri, kufanya uinjilisti, lakini tumekosa kujua kuwa mapenzi ya MUNGU kwetu wote (kama watu wa Mungu) ni kuishi maisha matakatifu, yenye staha mwilini na rohoni.
Utakuta mkristo ameokoka anamwimbia Mungu, anahubiri na kweli wito wa MUNGU ndio uliomweka hapo, lakini tazama uvaaji wake, tazama maisha yake ya sirini, ni dhambi tupu imetawala.
Ni lazima kuyafanya mapenzi ya Mungu katika migawanyiko yote.
Bwana atusaidie sana kuliona hili, na yeye ni mwaminifu hajatuitia kwa hukumu bali tupate Baraka na faida, usiukimbie utakatifu ndugu mpendwa katika KRISTO, pasipo huo hatutaweza kumwona MUNGU (Waebrania 12:14).
Na kwa nguvu zetu hatutaweza kuishi maisha hayo ya usafi, lakini kwa msaada wa Roho Mtakatifu yote yanawezekana, tafuta ujazo wa Roho Mtakatifu.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Ipi tofauti ya utakatifu na utukufu?
JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/02/28/yafahamu-na-yatende-mapenzi-ya-mungu/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.