by Nuru ya Upendo | 11 April 2026 08:46 am04
Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze pamoja Biblia.
Bwana alipokutana na Petro aliambiwa “TANGU SASA UTAKUWA UKIVUA WATU”. Hii ni kauli pana, ambayo ni muhimu tuijadili kwa kina kidogo..
Luka 5:10 “na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu
akamwambia SIMONI, USIOGOPE, TANGU SASA UTAKUWA UKIVUA WATU”.
Hapa Bwana YESU alifananisha “Uvuvi wa Samaki” na “Uvunaji wa watu” . Kwa ufupi Bwana YESU alifananisha watu na “Samaki”… Kama vile samaki wanavyovuliwa kutoka majini hali kadhalika watu wanavuliwa kutoka upotevuni.
Sasa kama maji yanavyohusika katika “Uvuvi wa samaki” vile vile maji pia yatahusika “uvuvi wa watu” kama ishara.. na hapa ndio tunakuja kuona umuhimu wa UBATIZO.
Wengi hatuoni umuhimu wa Ubatizo katika kukamilisha wokovu, lakini Ubatizo wa maji mengi unasimama kama muhuri wa kukamilisha wokovu wa mtu (Soma Marko 16:16).
Unapobatizwa kwa maji mengi na kwa jina la BWANA YESU ni ishara ya kwamba umevuliwa kutoka katika ulimwengu..
Sasa jiulize, Umeona wapi samaki anavuliwa kutoka katika nchi kavu?.. Vile vile wewe na mimi kama samaki tuliovuliwa ni lazima tuwe na ishara ya kutoka majini, ndio hapa linakuja agizo la ubatizo.
Na samaki akishatoka majini anapoteza uhai wa maisha yake ya kwanza, na vile vile baada ya ubatizo mtu anapoteza uhai wa maisha yake ya kwanza ya dhambi (maana yake yale maisha ya dhambi anayafia, anakuwa kiumbe kipya).
Je umeshabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO (sawasawa na Matendo 2:38, Matendo 10:48 na Matendo 19:5).. Kama bado unasubiri nini?.. je bado unaendelea kushikilia mapokeo ya dini na dhehebu hata baada ya kuujua ukweli wa Biblia?
Siku ile hatutahukumiwa kulingana na Mapokeo tuliyopokea bali kulingana na maneno yaliyoandikwa katika vitabu vyote sitini na sita vya kwenye Biblia..
Ufunuo 20:12 “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao”.
Maneno ya Mungu ndani ya Biblia ndio yatakayotuhukumu siku ya mwisho, maana yake siku ile tutaulizwa kwa yale yaliyoandikwa kwenye biblia sio kwa yale tuliyoyapokea kwenye dini zetu..
Kwa namna gani?.. Hebu tuingie ndani kidogo kulifafanua hili..
Mtu mmoja alimfuata Bwana YESU na kumwuliza tiketi ya kuurithi uzima wa milele, hebu tusome jibu la Bwana YESU Mkuu.
Luka 10:25 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?
26 Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?”
Tazama jibu la Bwana hapa?.. hakumwambia “umerithishwa nini na wazazi, au umefundishwa nini kwenye dini yako”.. Lakini alimwambia “Imeandikwa nini” lakini sio tu imeandikwa nini, bali pia “Unasomaje”
Ikimaanisha kuwa wakati wa Mwisho, watu watahukumiwa kwa yaliyoandikwa katika Biblia..Na moja wapo ya jambo lililoandikwa katika maandiko ni ubatizo. Sasa kupuuzia agizo la msingi namna hii ni hatari sana, hatutakuwa na la kujibu siku ile, ikiwa tulijua kweli na hatukuifanyia kazi.
shetani amepofusha fikra za watu wengi katika siku hizi za mwisho, na kuwafanya wasijue wala kuona umuhimu wa ubatizo pamoja na baadhi ya mambo mengine ya msingi katika Biblia.
2Wakorintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.
Bwana atusaidie sisi tusiwe miongoni mwao wanapofushwa fikra na ibilisi.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
AGIZO LA TOBA LINAENDANA NA UBATIZO!.
TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU
Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/04/11/je-umevuliwa-kutoka-majini/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.