AGIZO LA TOBA LINAENDANA NA UBATIZO!.

AGIZO LA TOBA LINAENDANA NA UBATIZO!.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia!.

Usipoujua ufunuo umhusuyo Yesu hutaona sababu ya kumwamini wala kumfuata, vile vile usipopata ufunuo wa kutosha uhusuo ubatizo hutaona umuhimu wa kubatizwa! (utaona ni habari tu ya kawaida, kwamba ukibatizwa au usipobatizwa vyote ni sawa tu).

Nataka nikuambie ndugu, ubatizo ni tendo la muhimu sana kuliko wengi tunavyodhani. Na leo nataka tuone ni jinsi gani agizo la Ubatizo lilivyoambata na Toba, kwamba baada ya kutubu ni lazima kubatizwa.

Hebu tuyasome maneno yafuatayo ya Bwana Yesu..

Luka 24:46  “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;

47  na kwamba mataifa yote “WATAHUBIRIWA KWA JINA LAKE HABARI YA TOBA NA ONDOLEO LA DHAMBI, kuanza tangu Yerusalemu”.

Nataka tuone na kuutafakari kwa kina huo mstari wa 47 unaosema kuwa mataifa yote watahubiriwa “KWA JINA LAKE HABARI YA TOBA NA ONDOLEO LA DHAMBI”

Hili ni agizo ambalo Bwana Yesu aliwapa wanafunzi wake kwamba watu wote ni lazima wahubiriwe habari ya toba na ondoleo la dhambi kwa jina lake.

Mitume walilisikia hili agizo la Bwana, na walilishika  sasa hebu tuangalie ni kwa namna gani walilitekeleza,..je walikwenda kuwaambia tu watu “watubu waondolewe dhambi zao au kuna la ziada walilifanya ”

Tusome kitabu cha Matendo 2:36-38

Matendo 2:36  “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38  Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Umeona hapa! Petro anawaambia watu “watubu na kubatizwa kwa jina lake Yesu, wapate ondoleo la dhambi zao”.. na sio tu “Tubuni mpate ondoleo la dhambi”….. sasa linganisha na yale maagizo Bwana aliyowapa akina Petro kuwa “wakawahubirie watu wote kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi”.

Kumbe kuhubiriwa habari ya Toba na ondoleo la dhambi ni pamoja na ubatizo!.. Maana yake ili mtu apate ondoleo kamili la dhambi zake ni lazima pia akabatizwe (Katikati ya Toba na ondoleo la dhambi, kuna ubatizo ambao shetani kawafumba watu macho wasiuone)..Ndio maana ni ngumu leo hii wengi kushinda dhambi, kwasababu mzizi wa dhambi katika maisha yao haujaondolewa, kwasababu wameukosa ubatizo sahihi.

Mitume sehemu zote walihubiri hivi, kwamba watu baada ya kutubu ni lazima wakabatizwe ili dhambi zao ziondolewe… na mitume kamwe wasingeweza kufanya kitu chochote kilicho kinyume na maagizo ya Bwana Yesu…ikiwa na maana kuwa walimwelewa sana Bwana pale aliposema kuwa wakawahubirie mataifa yote kwa jina lake, kwamba ubatizo pia kwa jina lake ni sehemu ya mahubiri yao.

Swali ni je!, na wewe umebatizwa kwa maji mengi na  katika ubatizo sahihi wa jina la Bwana Yesu?.. Kumbuka, kama ulibatizwa utotoni basi fahamu kuwa watoto wachanga hawabatizwi kwasababu bado hawajatubu, (kujitambua hawajajitambua watawezaje kutubu?) ni sharti kwanza wahubiriwe wamwamini Mwokozi na kujijua kuwa wao ni wenye dhambi ndipo watubu na kubatizwa.  Bwana akubariki.

Tafuta ubatizo sahihi kama bado hujabatizwa, na kama utahitaji msaada Zaidi wa namna ya kupata ubatizo karibu na mahali ulipo basi utawasiliana nasi kupitia namba zetu hapa chini.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU

HUNA SHIRIKA NAMI.

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments