HUNA SHIRIKA NAMI.

HUNA SHIRIKA NAMI.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu lililo mwanga wa njia yetu na taa iongozayo miguu yetu.

Kuna mambo ambayo mbele ya macho yetu ni madogo, na huenda yakaonekana hayana maana sana au umuhimu sana, lakini kwa Mungu ni ya maana sana, kiasi kwamba usipoyafanya baada ya kuyajua yanaweza kukuweka mbali na Mungu maili nyingi sana sana pasipo hata kutegemea.

Na kuna mambo ambayo mbele ya macho yetu tunayaona ni ya muhimu sana lakini mbele za Mungu yakawa ni madogo sana. Sasa ni muhimu sana kujua yale ya muhimu na yale ambayo si ya muhimu. Na kawaida ya shetani ni kuyafanya yale ambayo si ya muhimu sana kuwa ya Muhimu na yale ya Muhimu sana kuwa ya kawaida.

Kwamfano kuna mahali Bwana Yesu aliwaambia Mafarisayo kuwa wameacha mambo ya msingi na muhimu kama Adili, rehema na imani na badala yake wanakesha kuzitukuza zaka wanazozitoa..Wakidhani kuwa Mungu anapendezwa na Zaka zao zaidi ya wao kuwa na rehema, kwasababu yeye mwenyewe alisema kuwa anataka rehema na si sadaka! (Mathayo 9:13). Maana yake cha msingi kwanza ni rehema na ndipo sadaka zifuate..

Mathayo 23:23  “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.

24  Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia”.

Vile vile kuna maagizo mengine manne (4) ambayo ni ya Muhimu lakini shetani kayafanya yaonekane kama sio ya muhimu machoni pa watu.

1.Ubatizo.

Ubatizo ni agizo la muhimu sana kwa kila mtu baada tu ya kuamini, na ubatizo ulio sahihi na wa kimaandiko ni ule wa kuzama katika maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (Soma Yohana 3:23, Matendo 2:38, na Matendo 19:5), shetani ameurahisisha ubatizo machoni pa watu wengi kwasababu anaujua umuhimu wake, na kaelekeza nguvu kubwa sana hapo kuzuia watu wasibatizwe kwasababu anaelewa uthamani wa ubatizo.

Ndio maana leo hii utaona mtu yupo tayari kwenda kuogelea katika fukwe za bahari, au katika mabwawa maalumu (swimming pools) hata masaa 6 na asichoke, lakini kitendo cha kutii tu agizo la kuzamishwa kwenye maji mara moja na kuibuka kwa jina la Yesu hataki, hapo ndio utaona jinsi shetani alivyowekeza nguvu zake nyingi, kuzuia jambo hilo.

2. Wanawake kufunika vichwa (wawapo ibadani).

Biblia imeagiza wanawake wafunike vichwa wawapo ibadani kwasababu ya malaika (1Wakorintho 11:10). Sasa ukitaka kujua malaika wana umuhimu gani kasome safari ya wana wa Israeli, ujue waliwekwa chini ya nani.

Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. 

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake”.

Mwanamke asiyefunika kichwa chake awapo ibadani baada ya kuujua ukweli, anaharibu uwepo wa Mungu na kujipunguzia Baraka za rohoni (haya ni mambo madogo machoni petu lakini mbele za Mungu ni makubwa na ya muhimu).

3. Kushiriki meza ya Bwana.

Bwana Yesu alisema tushiriki meza yake mara kwa mara, kwaajili ya ukumbusho wake.. Bwana Yesu kaitukuza meza yake hiyo zaidi hata ya siku yake ya kuzaliwa.. Hakuna mahali popote kaagiza tufanye ukumbusho wa siku yake ya kuzaliwa, lakini hapa kaagiza tushiriki meza yake kama ukumbusho wa siku yake ya kufa

1Wakorintho 11:24  “naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU.

25  Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, KWA UKUMBUSHO WANGU.

26  Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo”.

Sasa sisi tukilipuuzia agizo hili la kushiriki meza ya Bwana na kuona kama ni dogo tu!, na lisilo na maana.. Basi tufahamu kuwa tumekaidi Agizo kuu la muhimu kwa faida yetu wenyewe.. Kama upo mahali ambapo hupati nafasi ya kushiriki meza ya Bwana basi harakisha sana kutafuta kufanya hivyo.

4. Kutawadhana miguu.

Moja ya Agizo ambalo shetani kalifanya lionekane halina maana kabisa ni hili la kuoshana miguu, lakini ni agizo kuu sana, na la Muhimu sana.. Hebu turejee biblia tuone kama agizo hili lina umuhimu wowote.

Yohana 13:5  “Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.

6  Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi?

7  Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye.

8  Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. YESU AKAMWAMBIA, KAMA NISIPOKUTAWADHA, HUNA SHIRIKA NAMI.

9  Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia.

10  Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote”

Hebu rudia kuusoma huo mstari wa 8, majibu Bwana Yesu aliyompa Petro.. alimwambia “KAMA NISIPOKUTAWADHA, HUNA SHIRIKA NAMI”.  Kumbe kitendo cha kudharau au kukataa kuoshana miguu kinaweza kusababisha sisi kupoteza ushirika na Mungu moja kwa moja!!… ni jambo la kuogopesha sana!, na la kulitafakari sana..

Hebu tuendelee kusoma mistari inayofuata, tuone kama agizo hilo lilikuwa ni lazima kwetu..

1Wakorintho 13:12  “Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?

13  Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.

14  Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.

15  Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

16  Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.

17  Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda”

Hapo Bwana Yesu kasema wazi kabisa wala hatuhitaji ufunuo wowote kuelewa… Ni lazima kuoshana miguu sisi wakristo kwa wakristo..na ndio ulikuwa utaratibu wa kanisa la kwanza (soma 1Timotheo 5:9-10). Kwahiyo na sisi ni lazima tutii agizo hilo vinginevyo tutapoteza ushirika na Bwana.

Shetani atakuhubiria leo kupitia watumishi wake kuwa “agizo hilo si la msingi” ndugu usidanganyike!..hata Petro alidhani hivyo, lakini saa alipoujua ukweli, alitamani hata Bwana Yesu amwoshe mwili mzima!..

Bwana Yesu atusaidie.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Ni maneno gani Bwana Yesu aliyokuwa anayaandika ardhini? (Yohana 8:7).

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments