LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu, ambalo ndio cha kweli cha roho zetu.

Kawaida ya Mungu ni huwa hatoi agizo juu ya agizo. Yaani kwa mfano leo akikupa agizo fulani ulitelekeze, haundi agizo lingine juu yake kulibatilisha hilo la kwanza, Atafanya hivyo endapo tu lile la kwanza litakuwa limeisha muda wake.

Mara nyingi tunakuwa tukiacha yale maagizo ya kwanza ya Mungu, na hiyo inatupelekea aidha kukutana na hukumu yake, au kushindwa kutekeleza mipango yetu  kwa wakati.

Kwamfano utakutana na nabii mmoja katika biblia enzi za wafalme, ambaye alipewa maagizo na Mungu ya kwenda kumtolea unabii Mfalme mwasi Yeroboamu, akaambiwa akishamaliza kazi yake asile wala asinywe chochote katika mji huo, wala asilale au kupumzika na njia atakayoipita asiirudie tena hiyo hiyo. Lakini huyu nabii alipomaliza kweli kazi ya huduma alianza safari ya kuondoka. Lakini akiwa njiani alikutana na nabii mwingine mzee, akamshurutisha, aende kulala nyumbani kwake. Lakini yeye akamwambia Bwana amenionya nisikae mahali popote kwenye mji huu.

Sasa yule nabii mzee alipoona kuwa kijana huyu hataki, akamtungia habari za uongo na kumwambia, Bwana ameniambia ameghahiri, mpango wake, hivyo anataka uje ule upumzike nyumbani kwangu. Na yule kijana pasipo kufikiria ni kwanini Mungu awe kigeugeu, saa hiyo hiyo akamwamini, kwasababu  tu ni nabii mwenzake tena mzee, anauzoefu wa mambo ya kinabii, akaenda kukaa kwake.  Kitu kilichomtokea hatuna haja ya kueleza, sote tunajua alikuja kuliwa na simba, kwa kuyaasi maagizo ya Mungu (Soma 1Wafalme 13)

Tunamwona Mtu mwingine anaitwa, Balaamu, naye pia mwanzoni Mungu alimuonya asiende kuwalaani Israeli, lakini baadaye akawa analazimisha mawazo yake kwa Mungu, kilichofuata ilikuwa ni Mungu kumwambia haya nenda nitakuwa pamoja nawe..kumbe hakujua tayari njia Mungu alikuwa ameshamuandalia malaika wake amuue, na kama sio yule punda kumsaidia habari yake tusingeisoma leo hii kwenye biblia (Soma Hesabu 22).

Hiyo yote ni kutozingatia agizo la kwanza Mungu alilokupa, Siku zote agizo linalokuja juu ya agizo lile la mwanzo huwa halitokani na Mungu.

Tukisoma tena habari nyingine maarufu katika biblia ile ya Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka  Babeli utumwani, baada ya kukaa kule miaka 70. Biblia inatuambia Mungu alimuamsha moyo mfalme Koreshi wa uajemi, ili atoe amri kuwa watu wote waondoke kwenye makoloni yake, waende Yerusalemu kumjengea Mungu nyumba, kufuatana na unabii uliotolewa na Yeremia zamani.

Tunaona baada ya hapo Mfalme aliwapa zawadi nyingi sana, Hivyo waliondoka kwa moyo mkunjufu  wakijua kabisa Mungu kaitimiza ahadi yake ya kwenda kumjengea nyumba Yerusalemu. Lakini walipofika kule na kuanza kutia msingi wa nyumba ya Mungu, maadui zao wakaanza kunyanyuka hilo likawadhoofisha, na kama hiyo haitoshi wakaandika waraka wa uchongezi wakampelekea mfalme mwingine wa uajemi ambaye alikuja kutawala baada ya Koreshi, aliyeitwa Dario,  mfalme alipousoma, akatoa amri nyingine, kuwa usiendelee ujenzi wowote Yerusalemu, wa nyumba ya Bwana. Na mtu yeyote atakayefanya vile ilikuwa ni kifo.

Wayahudi waliposikia, juu waraka huo mpya, wote wakavunjika moyo, wakaacha kuijenga nyumba ya Mungu ambayo ilikuwa tayari katika hatua nzuri, Hivyo ikapelekea nyumba hiyo kubakia hivyo hivyo kwa muda wa miaka mingi sana..Kila mtu akarudi kuendelea na shughuli zake kila siku.

Wakasau kuwa ni Mungu ndiye aliyewapa maagizo kuwa wakamjengee nyumba yeye, hawakujiuliza sasa haya maagizo mengine yanatoka wapi?

Mpaka baadaye sana, tunaona manabii wawili yaani Hagai na Zekaria wanatokea, wanawatabiria na kuwauliza kwanini mnaacha kujenga nyumba ya Mungu, wakidai kuwa huu sio wakati wa kumjengea Mungu? Kwa muda wako soma kitabu chote cha Hagai utaona mambo hayo.

Unaona, walisikiliza sauti ya pili, wakaicha ile ya kwanza, na hiyo ikawapelekea kucheleweshwa kwa huduma yao waliyokuwa wameshaianza,.. Siku zote sauti ya pili ni ya shetani, na sio ya Mungu.

Vilevile katika agano jipya kuna agizo ambalo tayari Mungu alishatupa.

Marko 16:15-16 Inasema..

“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”.

Hili ni agizo ambalo Kristo alishatoa kibali, kufanya.. Lakini dunia ya sasa shetani ameshaiingilia, kiasi kwamba, sehemu nyingine watu hawaruhusiwi kuhubiri kabisa, sheria za nchi zao zimekataza..Sasa wewe kama mkristo ukiogopa sheria ya wanadamu, ukasema pengine huu sio wakati wa kufanya hivyo, ujue kuwa utafanana na wana wa Israeli walipokuwa wanalijenga hekalu la pili, utasubiria wee, na kamwe hiyo siku ambayo unayoina itafaa haitafika, Mungu atakachofanya ni kukumbusha tu, uliacha agizo la kwanza.

Sio hilo tu yapo maagizo mengine madogo madogo, yanakubana kiasi kwamba yanakufanya ushindwe hata kuiendeleza kazi ya Mungu, mpaka uwe na hiki au kile, au ukamilishe hiki au kile..Hayo yote hatupaswi kuyazingatia sana, mengine yana agenda ya shetani nyuma yake kukumwisha tu, bali tuzingatie lile agizo kuu la mwanzo ambalo Kristo ametupa enendeni ulimwenguni kote.

Mwingine atasema familia yangu iko hvi au vile..hupaswi kuangalia hayo yote

Safari ya imani, si mteremko muda wote, kuna wakati itasumbuliwa na mambo mengi, lakini hatupaswi kuyaogopa kwasababu Mungu ameshaahidi atakuwa na sisi katika hayo yote. Kama tu vile alivyokuwa kwa mababa zetu katika mapito yao.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAAGIZO YA BWANA YESU NI BORA KULIKO MAAGIZO YA DAKTARI:

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments