Ni maneno gani Bwana Yesu aliyokuwa anayaandika ardhini? (Yohana 8:7).

Ni maneno gani Bwana Yesu aliyokuwa anayaandika ardhini? (Yohana 8:7).

Jibu: Tuisome Habari nyenyewe…

Yohana 8:3 “Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

4 Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

5 Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

6 Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, AKAANDIKA KWA KIDOLE CHAKE KATIKA NCHI.

7 Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8 Akainama tena, AKAANDIKA KWA KIDOLE CHAKE KATIKA NCHI.

9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.

10 Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

11 Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]”.

Katika tukio hilo maandiko, hayajasema wala kutaja ni kitu gani Bwana Yesu alichokuwa anakiandika ardhini, ikifunua kuwa SIO KITU CHA MUHIMU SANA SISI KUKIJUA, maana ingekuwa ni cha muhimu sana kukijua basi Mtume Yohana asingeacha kukiandika kwa faida yake na yetu pia, au Marko au Mathayo, wangeviandika… Lakini hakikuwa kitu cha muhimu sana kwetu kukijua…Ni sawa tutafute ni aina gani ya udongo, Bwana aliyoitengenezea tope, kwaajili ya kumponya yule kipofu.

Yohana 9:6 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho”.

Unaona?..kujua ni aina gani ya udongo iliyotumika hapo kutengenezea tope, haitusaidii sana, vile vile kujua ni aina gani ya Mti ulitumika kumsulubisha Bwana pale msalabani, pia haitusaidii chochote, kwamba tujue ule mti ulikuwa ni Mkoko, au Mtini, au Mpingo, au Mwerezi au Mwaloni haitusaidii chochote kiroho.. Ndio maana maandiko hayaeleza aina ya mti huo.

Vile vile ni maneno gani Bwana Yesu aliyokuwa anayaandika ardhini sio jambo la muhimu kulijua.. Wengi wanasema Bwana Yesu alikuwa anaandika dhambi za wale Mafarisayo na Masadukayo ardhini, kufuatia andiko la Yeremia 17:13..

Yeremia 17:13 “Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. WAO WATAKAOJITENGA NAMI WATAANDIKWA KATIKA MCHANGA, kwa sababu wamemwacha Bwana, kisima cha maji yaliyo hai”.

Lakini bado hoja hii haina nguvu, kwasababu Bwana Yesu angekuwa kutwa kuchwa anashinda kuandika tu dhambi za watu mchangani, kwasababu waliokuwa wanamkataa ni wengi.

Hivyo alichokuwa anakiandika sio cha Muhimu kukifaham, lakini kilicho cha muhimu kujua ni KWANINI ALIKUWA ANAANDIKA ARDHINI, WAKATI WATU WANAMWONGELESHWA!. Hicho ndio cha muhimu kujua..

Sababu kuu ya  Bwana Yesu kushuka na kuanza kuandika chini, ilikuwa ni kwa “LENGO LA KUWAPA NAFASI YA KUJITAFAKARI na YA KUCHUKUA MAAMUZI THABITI”.

Ili tuelewe vizuri, tuutafakari huu mfano mrahisi.

“Mtu Fulani unayemjua amekuja kwako kukuuliza swali la mtego, au swali ambalo anayo majibu yake..na wewe ukajua anayo majibu yake…Hivyo ukaamua kukaa kimya, usimjibu swali lile, huku ukianza kuchezea chezea shilingi iliyopo mezani, pako mbele yako, au ukaendelea kuchezea simu…Na baadaye akazidi kukuhimiza umjibu… wewe ukamjibu, jibu fupi, la kumtafakarisha..na baada ya kumjibu ukaendelea kuchezea chezea ile shilingi iliyopo mezani au ukaendelea kuchezea simu yako”.

Je kwa tukio hilo kuna lolote la kujifunza katika hiyo shilingi au hiyo simu?.. kwamba tuanze kutafuta kujua ni shilingi ngapi uliyokuwa unaichezea, au ni mizunguko mingapi uliyokuwa unaizungusha au tuanze kutafuta kujua ni nini ulikuwa unakitazama kwenye simu wakati unaongeleshwa?.

Jibu ni la!.. wewe ulikuwa unarusha rusha ile shilingi, au unachezea simu ile kwa lengo la kumpa yule mtu nafasi ya kujitafakari swali alilouliza, hali kadhalika baada ya kumjibu kwa ufupi na kuendelea kuchezea simu yako ni ili kumpa nafasi ya nafasi ya kuondoka, na kutafakari ulichomwambia.. asiendelee kukuuliza maswali ambayo anayo majibu yake. (Na kwa njama hiyo fupi, basi utafanikiwa kumwondoa huyo mtu mbele yako, bila kutumia nguvu nyingi).

Ndicho Bwana Yesu alichowafanyia Mafarisayo, lengo lake ni kuwapa muda wa kujitafakari na kuacha kuuliza maswali ambayo wanayo majibu yake, na vile vile kuondoka pale. Lakini si kuandika dhambi zao ardhini.

Hivyo hiyo ni Hekima Bwana aliyoitumia kufupisha majadiliano marefu, na hoja zisizokuwa na Msingi.

Na sisi tunachoweza kujifunza hapo ni kuwa, sio kila hoja ni za kushiriki, nyingine ni kuzikatisha kwa Hekima.. Si kila swali ni la kujibu kwa urefu, na si kila mazungumzo ni ya kuyakumbatia kwa muda mrefu. Mazungumzo ambayo ni ya mashindano ya dini, hayo Mtume Paulo kwa ufunuo wa Roho alimwonya Timotheo na makanisa yote Kristo, kwamba wajiepushe nayo..

1Timotheo 6:20 “Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo”

2Timotheo 2:14 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao”

Bwana Yesu alipopelekwa mbele ya Makuhani na mbele ya Pilato, hakuwa mtu wa maneno mengi, mara zote alipoulizwa maswali ambayo hayana maana yoyote alikaa kimya!!..

Marko 15:4 “Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi.

4 Pilato akamwuliza tena akisema, HUJIBU NENO? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!

5 Wala Yesu HAKUJIBU NENO TENA, hata Pilato akastaajabu”.

Nasi pia pia hatuna budi kuwa watu wa maneno machache na watu wa kujiepusha na mashindano, ya dini.. Umeona, kwa matendo hayo mawili tu ya Bwana kuacha kuwazungumza na wale mafarisayo na kuendelea kuandika chini, ilitosha kuwaondoa Mafarisayo wale, Zaidi hata angetumia maneno mengi, lakini kwa maneno yale machache na tendo lile moja, alivifunga vyinywa vyao.

Tito 3:9 “Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Je Musa yupo anawashitaki watu..kulingana na Yohana 5:45?

Je kauli ya Bwana Yesu inajichanganya? Katika Yohana 8:14 na Yohana 5:31?

NEEMA YA MUNGU KWA MARIAMU.

Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana?

Kwanini Yakobo na Yohana waliitwa “Wana wa Ngurumo”?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amen