ZITAMBUE NAKALA(COPY) ZA IBILISI

by Nuru ya Upendo | 30 April 2026 08:46 am04

Jina la Bwana YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze maandiko..

shetani hana jipya zaidi ya kunakili (kucopy) vile vilivyopo na kuvutumia kinyume.

Kwamfano kafara za wanyama kama mbuzi na kondoo kwaajili ya utakaso hazikuanzia kwa shetani, bali zilianza kwa MUNGU, ambapo katika Agano la kwanza (yaani Agano la kale) damu za wanyama hao zilitumika kwaajili ya utakaso, lakini sasa Agano jipya hazitumiki tena kwani Damu ya YESU ni bora zaidi ya damu za wanyama.

Kwahiyo shetani anachokifanya ni kunakili kilichokuwa kinatumika zamani (kisicho na matumizi tena) na kukileta siku za mwisho kwaajili ya matumizi yake, ndio maana utaona waganga wa kienyeji na wachawi ndio sadaka zao hizo.

Sasa sio tu hilo, lakini pia katika utumishi, shetani anayo desturi ya kutengeneza nakala..

Kwa namna gani?

Hebu turejee ile habari ya yule mchawi aliyeitwa.. “Bar-YESU” katika Matendo 13?..tuzisome habari zake kidogo kisha tuendelee mbele..

Matendo 13:6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake BAR-YESU;

7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali SERGIO PAULO, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu”

Huyu “Bar-Yesu” ni nabii wa uongo na ni mchawi, lakini ajabu ni kwamba jina lake limebeba jina la YESU ndani yake.. Je unaelewa maana ya Bar-Yesu?.. maana yake ni “Mwana wa YESU” hiyo ndio tafsiri yake..

Kwahiyo huyu mchawi na nabii wa uongo, alikuwa ni mtu anayemjua YESU na anayedai kufundisha habari za YESU, lakini nyuma yake alikuwa ni mwongo.

Na jambo jingine la ajabu ni kwamba huyu Bar-Yesu alikuwa ni mwalimu wa kiroho wa mtu mmoja aliyeitwa “Sergio-Paulo”… Je unaelewa maana ya Sergio-Paulo?…maana yake ni “Mhudumu-Paulo”..

Kwahiyo wakati YESU wa Mnazareti, anammiliki Paulo mtumishi wa Mungu, yupo mtu anaitwa Bar-YESU anayemmiliki Sergio Paulo.

 Kwahiyo hapa kuna “Sergio-Paulo” na “Bar-Yesu” na kuna “Paulo” na “YESU”. Kuonyesha kuwa shetani hana jipya zaidi ya kunakili vile vilivyopo vilivyo halali na kuvigeuza kwa matumizi yake.

Maandiko yanasema hivyo…

2Wakorintho 11:14 “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

15 Basi si neno kubwa watumishi wake NAO WAKIJIGEUZA WAWE MFANO WA WATUMISHI WA HAKI, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao”.

Kwahiyo si kila anaitwa mtumishi wa YESU ni mtumishi kweli wa YESU, vile vile si kila anayejiita ni Mkristo, ni Mkristo kweli kweli, ni muhimu kuwa macho sana, na kujua vipimo halisi vya kuwatambua manabii wa uongo, waalimu wa uongo, wachungaji wa uongo, waimbaji wa uongo pamoja na wakristo wa uongo.

Na kipimo hiko si kingine zaidi ya NENO LA MUNGU, baada ya kujaa Roho Mtakatifu, Neno la MUNGU pekee ndio kipimo cha kumjua huyu ni wa MUNGU au wa ibilsi, hii ni sauti ya Mungu au ya ibilisi.

Je umeokoka?.. unao uhakika wa kwenda mbinguni ikitokea parapanda imelia leo?

Kama bado haujampa YESU maisha yako, bado parapanda haijalia leo, lakini muda wowote mambo yanabadilika, hivyo fanya mabadiliko kabla ya mabadiliko makuu kutokea.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JIHADHARI NA ROHO YA YEZEBELI.

Roho ya Malipizi/ roho za malipizi ni nini?

MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.

MKUU WA UZIMA AKUWEKE HURU.

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/04/30/zitambue-nakalacopy-za-ibilisi/