GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

Kuna gharama kubwa sana katika kuupata ufalme wa mbinguni kama Bwana Yesu alivyotangulia kusema kwenye Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. ” Hii ikiwa na maana kuwa ufalme wa mbinguni ni kitu kinachogombaniwa kwa nguvu na watakaokipata ni wachache. Na kumbuka NGUVU zinazozungumziwa hapo sio nguvu za kimwilini, Tukisoma..

Mathayo 13:44-46 “

44 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akalinunua shamba lile.

45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;

46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akainunua. “

gharama ya ufalme wa mbinguni..Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;  46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akainunua. "

Bwana Yesu alifananisha ufalme wa mbinguni na maisha yetu tunayoishi kila siku, kama tukisoma hiyo mifano hapo juu tunaona kuna mfanya biashara aliyekuwa anatafuta lulu nzuri ya thamani kubwa, na alipoiona akaipenda sana, pengine hakuwa na fedha za kutosha, kuinunua kutokana na gharama ya LULU hiyo ilivyokuwa na thamani kubwa, lakini kwasababu ni mfanya biashara, alitafakari sana, kwamba japo inauzwa kwa thamani nyingi, lakini akiipata ataweza kuiuza mahali pengine kwa gharama kubwa zaidi, Hivyo atarudisha fedha aliyoinunulia pamoja na faida nyingi juu yake.

Kwasababu hiyo basi ilimpasa aende kuuza kila kitu alichokuwa nacho pengine hata nyumba yake, na miradi yake yote, ilimradi tu afikie kiwango kile cha pesa akainunue lulu ile yenye thamani kubwa.

Labda pengine alivyodhamiria kufanya hivyo, alionekana mwendawazimu mbele za watu kuuza mali alizozitaabikia kwa muda mrefu, lakini kwasababu ni mfanya biashara alifahamu ni kitu gani anafanya.

Vivyo hivyo na yule mwingine aliyeona hazina iliyositirika katika shamba na kwenda kuuza vyote alivyonavyo hakuwa mwendawazimu, pengine aliiona ALMASI imejichimbia katika kiwanja cha jirani yake, hivyo ili aweze kuipata ni sharti kile kiwanja kiwe chake, ili awe na ruksa ya kuifukua,

Sasa kwa ujanja, akaenda kumshawishi mwenye kiwanja amuuzie hata kwa bei mara 10 ya bei halisi ya kiwanja kile ili aweze kukipata kwa haraka na bila ya usumbufu , kwa kuwa mtu huyo anajua ni kitu gani anachokifanya, akaamua akauze kila kitu alichokuwa nacho, pengine mifugo yake, au majumba yake, au magari yake, na kama fedha isingetosha angeweza hata kwenda kukopa ili atimize lengo lake la kupata kiwanja kile.

Lakini kwa namna ya kawaida watu wangemuona kama amelogwa, au amerukwa na akili, kugharimikia kitu kisichokuwa na faida, lakini yeye hakuona tu kiwanja, bali aliuona UTAJIRI mkubwa zaidi ya kile kiwanja.

Mifano hiyo hiyo inatufundisha sisi kama wanadamu, HATUTAWEZA KUUPATA UFALME WA MBINGUNI, KAMA BADO HATUJAJUA THAMANI YAKE. Kumbuka yule mfanyabiasha hakuona tu lulu bali aliona thamani kubwa iliyopo ndani ya lulu, ndiyo ikamgharimu kuuza kila kitu, vivyo hivyo na yule aliyenunua shamba, hakuona tu shamba, bali aliona thamani ya kitu kilichokuwa kimejificha ndani ya lile shamba na ndipo gharama za kukipata hicho kitu zinajitokeza.

Na katika ufalme wa mbinguni, usiuone tu ufalme wa mbinguni halafu basi, bali tazama thamani na utajiri ulioko ndani ya huo ufalme, ukishalifahamu hilo au kupata ufunuo huo utakuwa na nguvu za kuchukuliana na gharama zozote utakazokumbana nazo kwa furaha zote.

Tukirudi kwa kijana mmoja aliyeitwa Musa, tunaona alizaliwa katika makasri ya kifalme ya FARAO, aliyekuwa msomi, na mtawala mwenye cheo, pamoja na mali nyingi, lakini ilifika wakati neema za Mungu ilifunguliwa machoni pake,na kuuona uzuri ulio katika ufalme wa mbinguni, hivyo kwa furaha yote aliamua kuuza kila kitu alichokuwa nacho ili aupate ,alidharau elimu yake ya kipagani, alidharau cheo chake kama mfalme mrithi, alidharau anasa na fahari alizokuwa anazipata katika jumba la kifalme, ili tu aupate ufalme usioharibika wa mbinguni..

Mtume Paulo aliandika katika.Wabrania 11:24 Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. “

Tunaona hapo Musa alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni Utajiri mkuu kuliko hazina zote za Misri, ilimpasa AUZE baadhi ya mambo, ili aweze KUUNUNUA ufalme wa mbinguni, aliuona utajiri mkubwa huko mbeleni kuliko hazina zote za Misri, Ilimpasa auze umaarufu wake, ilimpasa auze anasa zake, ilimpasa auze ujana wake, ilimpasa auze kiburi chake, ilimpasa auze fashion zake, ilimpasa auze majigambo yake na ujuzi wake, ilimpasa auze dhuluma yake, ili aweze kufikia viwango vya kuununua ule UFALME WA MBINGUNI.

Vivyo hivyo na mtume Paulo mwenyewe aliingia gharama hizo hizo..ukisoma Wafilipi 3:7-8 inasema..

” Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama “MAVI” ili nipate Kristo; “

Paulo ambaye alikuwa ni msomi mwenye cheo na kiburi alihesabu mambo yote kuwa kama mavi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni, kumbuka kilichomfanya achukue uamuzi huo sio tu kwasababu ni neno “ufalme wa mbinguni” , hapana bali ni UTAJIRI aliouna angeupata katika huo ufalme.Na kwa kufunuliwa na Roho Paulo alifika wakati na kusema

 Warumi 8:18-19

18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama UTUKUFU ULE UTAKAOFUNULIWA KWETU.

19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.

Hivyo ndugu fungua macho yako uone thamani na utajiri mkubwa ulio katika huo ufalme, ndipo utakapoona sababu ya kuacha kila kitu kisichompendeza Mungu kwa furaha zote na kumwandamia Mungu kwa hali zote,. Kumbuka thawabu za UFALME WA MBINGUNI, zitakazokuja huko ni mambo mazuri ambayo biblia inasema katika..1Wakoritho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,)

Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. “, pia usisahau, kutakuwa na wafalme na wenye mamlaka kubwa, pamoja na makuhani wa Mungu hawa watakaa pamoja na Kristo na kuhudumu pamoja naye, na huko watakuwepo pia watu wa kawaida tu, thawabu zitatofautiana sana, na ni milele, ikiwa na maana kuwa kama wewe ni mdogo kule utabaki hivyo hivyo milele, na kama wewe ni mfalme kule utadumu mfalme milele, na Bwana wetu YESU KRISTO akiwa kama MFALME WA WAFALME.  

Jina la BWANA YESU LIBARIKIWE.

Kuna wakati mitume walimuuliza Bwana..

Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. “

Hivyo wale watakaoketi karibu na Bwana ni wale tu, walioona thamani na kuingia gharama za kuununua ufalme wa mbinguni, je! ufalme huu unathamani gani kwako? , wewe mwanamke hauwezi ukaacha fashion na kuvaa hivyo vimini na suruali, kwasababu hauoni faida yoyote ya kuacha kufanya hivyo, mwanamume hauwezi kuacha pombe na sigara kwasababu kwako ni sawasawa ni biashara isiyo na faida, hauwezi kuacha uasherati, wizi kwasababu faida ya ile LULU(UFALME WA MBINGUNI) haijafunuliwa machoni pako. Laiti ungeifahamu thamani ya LULU usingefanya hivyo.

Lakini kumbuka wana wa Mungu, sio wajinga kuwaona wanauza mambo ya ulimwengu huu sasa ivi ili wanunue mambo ya ulimwengu unaokuja, ni kwasababu wanaona mbele, na kujipenda na wanapenda maisha ndio maana wanatafuta maisha ya milele yanayodumu, na wanapenda furaha zaidi hata ya wewe unayejiona unajistarehesha katika anasa za ulimwengu huu.

Kanisa tunaloishi ndilo la mwisho linalojulikana kama LAODIKIA kulingana na Kalenda ya Mungu, na ujumbe wetu tuliopewa umeandikwa katika kitabu cha Ufunuo 3:14 unasomeka hivi..

“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO, UPATE KUWA TAJIRI, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. “

Bwana ametupa shauri tukanunue dhahabu kwake tupate kuwa matajiri, kumbuka ili KUNUNUA lazima TUUZE yote maovu tulionayo ili tuweze kukidhi viwango vya kuupata ufalme wa mbinguni. Maombi yangu ni Bwana akupe neema ya kuona THAMANI YA UFALME WA MBINGUNI kwasababu UFALME WA MBINGUNI unapatikana kwa nguvu, na wenye nguvu ndio wanaouteka.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/bei-ya-ufalme-wa-mbinguni/