MTU MWENYE KUSITA-SITA KATIKA MAWAZO MAWILI.

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

Yakobo 1:5-8″  Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. 

6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. 

7 MAANA MTU KAMA YULE ASIDHANI,YA KUWA ATAPOKEA KITU KWA BWANA. 

8 MTU WA NIA MBILI HUSITA-SITA KATIKA NJIA ZAKE ZOTE.”

MTU MWENYE KUSITA-SITA KATIKA MAWAZO MAWILI.

Mtu akishakuwa mkristo vita kubwa anayoanza kupitia ni katika AKILI, shetani anahamisha vita vyake kutoka katika mambo ya nje, kwenda katika mambo ya ndani kwa kusudi moja tu, la kumfanya mtu huyo alitilie SHAKA Neno la Mungu!, kwa kumletea mashaka asiuamini wokovu wake jambo linalompelekea mtu kama huyo kuwa katika hali ya KUSITA KWENYE MAWAZO MAWILI.

Shetani anafahamu kuwa mtu atakapoliamini Neno la Mungu kwa asilimia zote pasipo mashaka atapata anachokitafuta, sasa hapo shetani ndipo anapoanza kuwinda imani ya huyo mtu kwa kumletea mashaka moyoni mwake. Tunaona mfano mtu kama Petro alianza kutembea vizuri juu ya maji lakini alipoanza kutia shaka tu akaanza kuzama.

Kwahiyo silaha kubwa shetani anayoitumia kwa mkristo ni kumletea mashaka asiliamini Neno la Mungu aendelee kubaki katika hali ya kusita-sita asipokee kitu chochote kutoka kwa Bwana. Mbinu hii shetani alitoka nayo tangu Edeni pale Hawa aliporuhusu wazo la shetani la kutilia mashaka NENO la Mungu, na kula tunda ikapelekea mauti jambo ambalo linaendelea mpaka sasa. KULITILIA MASHAKA NENO LA MAUNGU!.

  Kwamfano Neno la Mungu limeahidi “wakutanikapo wawili au watatu kwa jina lake yeye atakuwepo katikati yao”. Lakini shetani atamletea mtu huyo wazo kwenye akili yake likisema : {…Aah! hilo haliwezekani, Mungu yupo mbinguni hawezi kuwepo hapa katikati yetu,hawezi kuwepo sehemu kama hii, sisi ni wachafu kama sivyo mbona hatumuhisi….}.  Sasa mtu huyo akidhani kuwa hilo wazo ni la kwake, kumbe hajui linatoka kwa yule mwovu..kwasababu shetani amemletea hilo wazo likianza na “mimi.. mimi.. mimi”.

Halianzi kama shetani anamwambia mtu huyo bali linakuja kama vile yeye huyo mtu ndio analiwaza hilo wazo. Hivyo inakuwa ni ngumu kwa mtu kama huyo kutambua mawazo ya shetani ni yapi na yake ni yapi. Kwasababu hiyo basi shetani anafanikiwa kumwacha katika hali ya kusita-sita na mwisho wa siku hapokei chochote kutoka kwa Mungu kwasababu Mungu hakai katika mashaka, yeye ni wa kuaminiwa tu!.

  Tuchukue mfano mwingine, Neno la Mungu linasema.“Kwa kupigwa kwake sisi tumepona”. Hivyo Mtu akiwa mgonjwa atakapojaribu tu kulitafakari hili NENO limfae kwa ajili ya uponyaji wake, wazo lingine litamjia kwa haraka kichwani mwake,..{….Aaah! Hivi ni kweli inawezakana, hii inahitaji mtu mwenye upako sana, au mtakatifu sana, mimi nimemkosea sana Mungu hawezi kunisamehe wala kunisikia….} .

Kwahiyo mtu huyu anadhani kuwa mawazo hayo ni yeye kayatengeneza kumbe hajui ni shetani ndiye aliyemtengenezea na kuyapandikiza kwenye Akili yake pasipo mtu huyo kujua, Na kama ilivyo ada  shetani anamletea hilo wazo lianze na neno “mimi,.. mimi”. Hivyo basi mashaka hayo yakishaingia ndani ya moyo wake yanamsababishia mtu huyo asipokee uponyaji wake. Shetani anakuwa amemshinda.

  Mfano mwingine, Bwana Yesu alisema Marko 11:24″  Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. “. Hapa utamkuta mtu yupo katika kusali na kupeleka mahitaji yake binafsi mbele za Mungu akiwa katikati ya kusali wazo linamjia,{…“Aah! Hivi kweli Mungu atajibu maombi yangu, Mungu lazima atakuwa hapendezwi na mimi!. Ili anisikie ingenipasa nifunge kwanza wiki tatu, Aaah! acha tu niombe anaweza akanijibu”….}..

Unaona hapo hilo neno “anaweza”.tayari ni mashaka hayo hana uhakika na anachokiomba akidhani kuwa hayo ni mawazo aliyoyatengeneza yeye, kumbe ni mawazo ya shetani kayatupa kwenye akili yake, na kumfanya mtu huyo kuwa katika hali ya kusita-sita hivyo hawezi kupokea chochote kutoka kwa Mungu, Kwasababu shetani anajua tu! atakapoliamini hilo NENO kwa asilimia zote, pasipo kutilia shaka kwa namna yoyote, Atapokea chochote anachokiomba.

Tazama hichi kisa hapa chini, jinsi mtu huyu alivyompa Kristo maisha yake, siku ya jumatatu, lakini angalia shetani alivyoanza kuiwinda imani yake, na kumpelekea kuwa MTU WA KUSITA-SITA KATIKA MAWAZO MAWILI.

Siku ya jumanne anaanza kujifunza Neno la Mungu…

..Siku ya jumatano anautilia mashaka wokovu wake…

…Alhamisi anajihisi hajaokoka na kurudia kumpa Kristo tena maisha yake…

NAMNA YA KUSHINDA HALI HIYO:

Wazo lolote linalokuja katika kichwa chako linalokufanya ulitilie shaka NENO la Mungu, lipinge na kulikataa kwa JINA LA YESU kwasababu hayo sio mawazo yako bali ni ya shetani ameyaelekeza kwako ili usipokee kitu kutoka kwa Mungu kwasababu Mungu anasema katika 

Yakobo 1:7-8 “Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. 

8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.“.

Hivyo basi  Rudisha mawazo yako na sema ndani ya moyo wako “maneno ya Mungu, ni kweli na hakika”. yashikile hayo hayo pasipo kujihukumu mwenyewe. Na kwa kufanya hivyo shetani atakukimbia na kukufanya kuwa mshindi siku zote na kupokea Ahadi za Mungu.

Usiruhusu mawazo yoyote ya kulichunguza NENO la Mungu kuwa linafanyaje fanyaje kazi, siku zote njia za Mungu hazichunguziki wewe AMINI tu!. Hayo mengine mwachie yeye, amesema kwa kupigwa kwake tumepona! amini hilo NENO kila siku litamke,sema moyoni mwako Mungu siku zote hawezi kusema uongo! usitafute kujua litafanyaje fanyaje kazi, itaonekana kuwa hakuna matumaini! lakini wewe liamini tu na utashangaa unapokea uponyaji wako. NENO la Mungu linasema “yote yawezekana kwake yeye aaminiye”.

Kwahiyo ukiwa katika sala unaomba jambo lolote amini umelipokea. usianze kusita-sita, au kujiuliza uliza au kutafuta njia mbadala,wewe mwamini Mungu lishikilie hilo neno, nalo litatokea kama lilivyo usitazame muda hata kama litachelewa lakini litakuja tu! wewe liamini tu usiruhusu mawazo mengine yoyote ya shetani ya mashaka kuingia ndani yako.

Pambana shetani hapo ndipo anapofanyia vita na hakuna vita vigumu kama hivyo, Tutamshinda shetani tu pale tutakapokuwa na NENO ndani yetu na kuliamini asilimia mia, lakini tukiwa watu wa mashaka kama maandiko yanavyosema TUSITAZAMIE KUPOKEA KITU CHOCHOTE KUTOKA KWA BWANA.

……Hapa yule mtu anatambua uongo wa shetani na anachukua hatua..

…..mwishoni wokovu wake unakuwa thabiti usiokuwa na mashaka…….

Mungu akubariki!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa msaada wa maombi/Ushauri/ubatizo/mafundisho/Whatsapp: Namba zetu ni hizi: 

+255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

UMEPATA UHAKIKA WA KUTOKUINGIA HUKUMUNI KATIKA SIKU ILE?

MTETEZI WAKO NI NANI?

JE! NI SAHIHI KWA MKRISTO KUOA/KUOLEWA NA MTU WA IMANI NYINGINE?

NINI MAANA YA ELOHIMU?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/mtu-mwenye-kusita-sita-katika-mawazo-mawili/