JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

by Admin | 19 July 2018 08:46 pm07

Moja ya maagizo muhimu sana ambayo Bwana YESU KRISTO aliyatoa kwa kanisa ni ubatizo.

Mengine yakiwemo kushiriki,kutawadhana miguu kwa wakristo,wanawake kufunika vichwa vyao wakati wa ibada.Kati ya hayo ubatizo ni muhimu sana kwa mwamini yeyote kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake.Lakini ubatizo huu shetani ameuharibu usifanyike ipasavyo kwa sababu anajua una madhara makubwa katika kumbadilisha mkristo.na hiyo ndiyo imekuwa kazi ya shetani tangu awali kuyapindisha maneno ya Mungu na kuzuia watu wasimfikie Mungu katika utimilifu wote.

Makanisa mengi leo hii yanabatiza watu au watoto wachanga kwa kuwanyunyuzia maji. Wakibatiza kwa jina la BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU kulingana na mathayo 28:19. “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho mtakatifu”..swali ni je! hili jina linatumiwa ipasavyo kubatizia?

Kwa kukosa Roho ya ufunuo na uelewa wa maandiko viongozi wengi wa dini wameacha kweli. Na kugeukia mafundisho ya kipagani na kibaya zaidi wengi wao wanaujua ukweli lakini wanawaficha watu wasiujue ukweli kwa kuogopa kufukuzwa kwenye mashirika yao ya dini. Watu kama hawa ni adui wa msalaba

 Bwana aliowazungumzia akisema 

Mathayo 23:13″ ole wenu waandishi na mafarisayo, wanafki! kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamuingii wala wanaoingia hamwaachi waingie.”

 Tukirejea tena kwenye maandiko

Yohana 5:42-43 “walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.Mimi nimekuja kwa JINA LA BABA YANGU, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.”

hapa tunaona dhahiri kabisa jina alilonalo Yesu ni jina la BABA yake. Kwa namna hiyo basi jina la baba yake ni Yesu.

Tukirudi tena kwenye maandiko yohana 14:26 Yesu Kristo alisema “lakini huyo msaidizi,huyo Roho mtakatifu ambaye baba atampeleka  KWA JINA LANGU, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”na  hapa tunaona Roho Mtakatifu alitolewa kwetu kwa jina la Bwana Yesu. kwahiyo hapa biblia inatufundisha dhahiri kabisa kuwa jina la Roho Mtakatifu ni Yesu.

Na tena kwenye maandiko tunaona kuwa Roho Mtakatifu ndiye Baba mathayo 1:20 “…Yusufu, mwana wa Daudi usihofu kumchukua Mariamu mkeo maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu” kwahiyo Baba ndiye yule yule Roho na ndiye yule yule aliyechukua mwili na kuishi pamoja nasi kwahiyo hapa hatuoni ‘utatu’ wa aina yeyote ambao unahubiriwa leo hii na makanisa mengi.  Mungu ni mmoja tu!.

Kwahiyo jina la Baba ni Yesu na jina la Mwana ni Yesu na jina la Roho Mtakatifu ni Yesu; baba,mwana na roho ni vyeo na sio majina kwa mfano mtu anaweza akawa baba kwa mtoto wake,mume kwa mke wake,babu kwa mjukuu wake lakini jina lake anaweza akawa anaitwa Yohana na sio ‘baba,mume au mjukuu’ vivyo hivyo kwa Mungu.aliposema mkawabatize kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu alikuwa anazungumzia Jina la YESU KRISTO ambalo ndilo jina la baba na mwana na Roho Mtakatifu.

Katika biblia Wakristo na mitume wote walibatizwa na kubatiza kwa JINA LA YESU KRISTO na sio kwa JINA LA BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU. ubatizo huu wa uwongo ulikuja kuingizwa na kanisa katoliki katika baraza la Nikea mwaka 325 AD pale ukristo ulipochanganywa na upagani na ibada ya miungu mingi ya Roma.

Tukisoma matendo ya mitume 2:37-38 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao. wakamwambia Petro na mitume wengine , tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, tubuni mkabatizwa kila mmoja KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”

Tukisoma tena  katika maandiko Filipo alipoenda Samaria na wale watu wa ule mji walipoiamini injili walibatizwa wote kwa jina lake Yesu Kristo matendo 8:12 ” lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habati njema za ufalme wa Mungu na  JINA LAKE YESU KRISTO  wakabatizwa wanaume na wanawake”

Na pia matendo 8:14-17  inasema ” Na mitume walipokuwa Yerusalemu, waliposika ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu.wakawapelekea Petro na Yohana ambao waliposhuka wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila WAMEBATIZWA TU KWA JINA  LAKE BWANA YESU”

Tukirejea tena.

Matendo 10:48  Petro alipokuwa nyumbani mwa Kornelio alisema maneno haya “Ni nani awezaye kuzuia maji,hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vilevile kama sisi? akaamuru WABATIZWE KWA JINA LAKE YESU KRISTO”

Tukisoma tena katika matendo 19:2-6  hapa Paulo akiwa Efeso alikutana na watu kadha wa kadha akawauliza.” je! mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?, wakamjibu, la, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? wakasema, kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani Yesu. Waliposikia haya WAKABATIZWA KWA JINA LA BWANA YESU”

Mitume wote hawa kuanzia Petro,Yohana,Filipo na mtume Paulo wote hawa walibatiza kwa jina la Yesu Kristo je? tuwaulize hawa viongozi wa dini wanaobatiza kwa jina la baba na mwana na roho mtakatifu wameutolea wapi??? na biblia inasema katika

Wakolosai 3:17 ” na kila mfanyalo kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote  katika Jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu baba kwa yeye”..

hii ina maana tukiomba tunaomba kwa jina la Yesu,tukitoa pepo tunatoa kwa Jina la Yesu, tukiponya watu tunaponya kwa jina la Yesu,tukifufua wafu tunafufua kwa jina la Yesu na tukibatizwa tunabatizwa kwa jina la YESU biblia inasema kwenye

Matendo 4:12 “…kwa maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”

na hakuna mahali popote katika biblia mtu alibatizwa kwa jina la Baba na Mwana na Roho mtakatifu

na maana ya neno ubatizo ni “kuzamishwa” na sio kunyunyuziwa, kwahiyo ni lazima kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji sawasawa na maandiko na hakuna mahali popote katika maandiko watoto wachanga wanabatizwa. Ubatizo ni pale mtu anapoona sababu ya yeye kutubu na kuoshwa dhambi zake ndipo anapoenda kubatizwa kwa jina la Yesu kwa ondoleo la dhambi zake.

Ewe ndugu Mkristo epuka mapokeo ambayo Yesu aliyaita “chachu ya mafarisayo” penda kuujua ukweli ndugu mpendwa na ubadilike na umuombe Roho wa Mungu akuongoze katika kweli yote usipende mtu yeyote achezee hatima yako ya maisha ya milele, uuchunge wokovu wako kuliko kitu chochote kile,Mpende Mungu, upende kuujua ukweli,ipende biblia..Mwulize mchungaji wako kwa upendo kabisa kwanini anayafanya hayo huku anaujua ukweli na kama haujui mwambie abadilike aendane na kweli ya Mungu inavyosema kulingana na maandiko.

Kama hujabatizwa au umebatizwa katika ubatizo usio sahihi ni vema ukabatizwa tena kwa jina la YESU KRISTO kwa ondoleo la dhambi zako kwani ubatizo sahihi ni muhimu sana..ukitaka kubatizwa tafuta kanisa lolote wanaoamini katika ubatizo sahihi tulioutaja hapo  juu au unaweza ukawasiliana nasi tutakusaidia namna ya kupata huduma ya ubatizo sahihi, karibu na mahali ulipo 0789001312

 Mungu akubariki 

  jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP             

  (ubatizo sahihi wa kuzamishwa na KWA JINA LA YESU KRISTO)

Muhtasari wa maelezo haya kwa njia ya video unaweza kuyapata hapa chini.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=kuCSAZcnM80[/embedyt]

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada zinazoendana:


Mada Nyinginezo:

MAAGIZO YA BWANA YESU NI BORA KULIKO MAAGIZO YA DAKTARI:

SAUTI AU NGURUMO

JE, KAMA HAUNA UBATIZO SAHIHI HAUWEZI KUWA NA ROHO MTAKATIFU?

JE! NI HATUA ZIPI MUHIMU ZA KUFUATA BAADA YA UBATIZO?

UBATIZO WA MOTO NI UPI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/19/ubatizo-sahihi/