AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.

by Admin | 11 September 2018 08:46 am09

Shetani tangu zamani amekua akibuni njia mbali mbali za kumfanya mwanadamu aangumie kwa anguko litakalomfanya asiweze tena kurudi nyuma, Na amekua akifanya hivyo kwa kuchunguza ni njia ipi inayomchukiza Mungu zaidi kuliko nyingine, na akishaipata anakwenda kuwashawishi wanadamu waitende hiyo ili Mungu asiwe na huruma kwao, waangamizwe moja kwa moja.

Kwa mfano tukisoma katika agano la kale, Bwana aliwapa wana wa Israeli amri 10, na zile nne za kwanza, zilimuhusu Mungu mwenyewe, waliambiwa wasiwe na miungu mingine ila Mungu wa Israeli, waliambiwa pia wasijifanyie sanamu ya kuchonga, kwani yeye ni Mungu mwenye wivu, waliambiwa pia wasilitaje bure jina la Bwana Mungu wao,..Sasa ukichunguza utaona shetani alipoona kuwa hizi ndizo Mungu kazitilia msisitizo, na kaziwekwa za kwanza kabisa, tena alipogundua kuwa Mungu ni Mungu mwenye wivu, ndipo akaanza kuwekeza nguvu zake zote hapo, kuwashawishi watu waiendee miungu mingine, na kuabudu sanamu, ili tu, Mungu atiwe wivu, awateketeze watu wake kwa maangamizi yasiyoweza kuponyeka, Na ndio maana ukisoma agano la kale, makosa mengi yaliyokuwa yanawakosesha wana wa Israeli wakati wote mpaka kuwasababishia kupelekwa utumwani, ni IBADA ZA SANAMU.

Hiyo ndio imekuwa desturi ya shetani katika vizazi vyote, lakini pia katika kipindi hichi tunachoishi Mungu alitoa amri ya kile anachokichukia zaidi na ndipo hapo hapo shetani naye kaenda kuwekeza zaidi nguvu zake ili awaangamize watu wengi kirahisi.

Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kufahamu kuwa tunaishi katika Kanisa la mwisho linaloitwa LAODIKIA, kulingana na unabii wa kibiblia, kumbuka yalikuwepo makanisa mengine sita, nayo yalishapita na jumbe zao, na sasa tupo katika kanisa la mwisho, na kanisa hili lilianza kuanzia mwaka 1906 na litaisha na unyakuo… Kwa urefu wa maelezo juu ya makanisa haya 7 unaweza ukasoma kwa kupitia link hii. >>>Nyakati saba za kanisa.

Sasa katika hili kanisa la 7 ambalo ndio tunaishi mimi na wewe, Mungu alizungumza na sisi na kutugawia amri ambayo inapaswa isivunjwe, kama tu ile amri ya kwanza ilivyokuwa katika agano la kale, kwamba mtu yeyote asiwe na miungu mingine ila yeye, kadhalika na katika kanisa hili la mwisho Bwana alitoa amri akasema “UWE MOTO!!”..akaongezea pia na kusema “KAMA HUWEZI KUWA MOTO, NI AFADHALI UWE BARIDI”..hakuishia hapo akaelezea jambo analolichukia kuliko yote, nalo ni “KUWA VUGUVUGU”..

Sasa shetani kwa kulijua hilo, ili amwangamize mwanadamu vizuri, na kumvunja vunja kabisa alikwenda kuwekeza nguvu zake zote mahali ambapo panamkasirisha Mungu zaidi, ili tu mwanadamu atakaponaswa hapo iwe ni ngumu kupona, aangamie milele..na sehemu hiyo sio nyingine zaidi ya kumfanya mtu awe vuguvugu.

Kumbuka shetani sasa hivi hatumii nguvu nyingi sana kuwafanya watu wawe BARIDI, yaani kuwafanya watu wasimjue Mungu kabisa, au kuwafanya wawe wa kidunia kabisa wasitake kujua Mungu au kanisa ni nini! Hapana, hatumii nguvu kubwa kuwafanya watu wasimsikie Yesu Kristo kabisa, yaani waendelee kuabudu miti, n.k. hapana hatumii nguvu kubwa huko kwasababu anajua hapo pana HERI pengine huko mbeleni neema ya Mungu ikipita juu ya huyo mtu kidogo tu anaweza kubadilika na kuwa MOTO..

Shetani anachofanya yeye sasa na majeshi yake, ni kuhakikisha kwa nguvu zote watu wanakuwa VUGUVUGU, yaani anahakikisha kuwa mtu anamfahamu Mungu, lakini amchanganye kidogo na mambo ya giza, anafanya juu chini mtu aende kanisani, baadaye akitoka aende disco, hataki awe ni mtu wa disco tu siku zote na asiende kanisani kabisa hata siku moja, hataki mtu awe ni wakidunia tu siku zote na hata siku moja hana habari na Mungu, anataka vyote vifanyike kwa pamoja kwasababu anajua Mungu kasema ni HERI mtu awe BARIDI kabisa kuliko VUGUVUGU. Kwasababu kama tulivyosema Shetani anajua mtu aliye baridi kabisa pengine huko mbeleni akisikia ukweli kidogo anaweza kubilika hivyo hawezi kuweka tegemeo lake kubwa kwa mtu wa namna hiyo kuliko Yule aliye vuguvugu.

Bwana Yesu alisema maneno haya kwa kanisa hili:

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, YA KUWA HU BARIDI, WALA HU MOTO; ingekuwa HERI kama ungekuwa baridi au moto16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, NITAKUTAPIKA UTOKE KATIKA KINYWA CHANGU ”.

Kama tunavyosoma, adhabu iliyonenwa hapo ya mtu atakayekuwa vuguvugu ni KUTAPIKWA,..Na mtu akishafikia hiyo hatua, basi hawezi kurudi nyuma kuokolewa tena, mtu huyo anakuwa tayari kashatengwa na uso wa Mungu milele, Ulishawahi kuona mtu yeyote akirudia kula matapishi yake tena?, Ni jambo lisilowezekana kabisa, yale matapishi sio chakula tena, ni sawa ni kinyesi tu, hata kuyatazama utaona kinyaa, na ndivyo ilivyo kwa mtu Yule aliye vuguvugu. Na ndio maana Bwana alisema ni heri uwe moto au baridi kuliko kuwa hapo katikati kwasababu mtu wa namna hiyo akishatapikwa kurudiwa tena ni ngumu.

Kumbuka kama tulivyoona shetani hapo ndipo anatilia mkazo, na kashafanikiwa kuwaweka watu wengi katika hali hiyo, mtu awe anajiita mkristo lakini bado ni mlevi, aende kanisani lakini bado anaenda kwa waganga wa kienyeji, kabatizwa katika ubatizo sahihi lakini bado anavuta sigara, anaimba kwaya lakini bado ni mwasherati, analipa zaka lakini bado anatoa hongo, anatabiri na kunena kwa lugha lakini bado anavaa mavazi ya kiasherati, anavaa vimini, suruali, kaptura, anapaka wanja, anahudhuria maombi lakini bado ni msengenyaji na bado anajiita mkristo, unafunga na kusali na babo unaishi na mwanamume au mwanamke ambaye hamjafunga ndoa, ni mshirika wa kwaya na bado umeachana na mke wako au mume wako..Hapo ndipo shetani anapotilia nguvu nyingi.

Sasa shetani ili kulifanikisha jambo hilo,aliwatia mafuta watumishi wake kuwafanya watu wawe BARIDI, pamoja na kuwa VUGUVUGU, wale wanaowafanya watu wawe baridi ndio hao waganga wa kienyeji, na vikundi vya kishetani, pamoja na watu waovu wa ulimwengu huu, lakini hao kama tulivyosema sio wabaya sana, Wapo watumishi wengine wa uongo waliochaguliwa na shetani mahususi kwa kuwafanya watu wawe vuguvugu…Hawa ndio wale mbwa mwitu Bwana aliowasemea katikakati ya kondoo,.

Mathayo 7: 15 “Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? “

Unaona hapo? Hawa wanabeba biblia kama wewe, wanajiita watumishi wa Mungu, na njia pekee ya kuwagundua si kwa kuwatazama bali ni kwa matunda yao,..kwa kutazama jamii ya watu wanaowazalisha(ndio matunda yao), utaweza kufahamu hao watumishi ni wa aina gani…kama ni vuguvugu,moto, au baridi…

Ukiona umedumu kwa muda mrefu katika mafundisho yao, na hujaona mahali popote unagusiwa juu ya hatma ya maisha yako ya kiroho kuhusu mbinguni na kuzimu, ufahamu kuwa upo katika sehemu ya hatari zaidi kuliko ungeenda kujiunga na vikundi vya kichawi au vya waganga wa kienyeji,..ukiona haugusiwi habari za mbinguni kila siku ni biashara tu na mafanikio, upo katika eneo la hatari kuandaliwa kutapikwa na Bwana.,ukiona mahali hapo haugusiwi habari za kutubu dhambi na kuishi maisha matakatifu,badala yake unahubiriwa injili za faraja tu, huku maisha yako ya kiroho yanaporomoka kila siku fahamu kuwa upo mahali pa hatari sana, inusuru roho yako.

Ukiona mahali ambapo huubiriwi misingi ya imani ya kikristo, yaani ubatizo wa maji tele, na ubatizo wa Roho Mtakatifu badala yake ni kupewa tu maji, na chumvi, na sabuni, kama njia ya kufunguliwa, kwasababu biblia inasema mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuingia ufalme wa mbinguni (Yohana 3) jua tu upo katika eneo la hatari, ukiona mahali Neno la Kristo halipewi kipaumbele au muda mrefu kuhubiriwa fahamu kuwa unatengenezewa mazingira ya kuwa vuguvugu, ukiona upo mahali hauhubiriwi usafi wa mwili wako na roho yako, haufundishwi umuhimu wa kujisitiri kwa mwanamke,(1Timotheo 2:9) unakwenda kanisani na vimini, na hauambiwi chochote, ujue kuwa upo katika mikono ya watumishi wa shetani.. Dhumuni la shetani ni kukuweka chini ya mikono yao ili uendelee kuwa vuguvugu, ufikie kipindi Fulani utapikwe na Bwana.

Hata kama watafanya miujiza kiasi gani jiepushe nao Bwana Yesu alisema..

Mathayo 7: 22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Na ndio maana Bwana anasema ni HERI KUWA MOTO, AU BARIDI kuliko kuwa VUGUVUGU, kwa maana nyingine adhabu ya mtu atakayekuwa vuguvugu huko aendako itakuwa ni kubwa kuliko ya Yule aliye baridi kabisa.

Ndugu hii injili unayoisikia kila siku, na hutaki kubadilika, unasema wewe ni mkristo lakini ukiangalia maisha yako na maandiko ni mbalimbali, umejiweka katika eneo la hatari zaidi, shetani anakufurahia kukuona katika hali hiyo, akisubiria hiyo siku Bwana atakayosema basi yatosha! Ili utapikwe, shetani anataka awe na uhakika wewe unakuwa wake milele. Hataki kukupoteza kwa namna yoyote ile na ndio maana anataka uendelee katika hali yako ya UVUGUVUGU. Ujione upo sawa na Mungu kumbe haupo sawa, ujione unempendeza Mungu kumbe unamchukiza n.k, Ni mara ngapi umesikia sauti ya Mungu ikisema na wewe ndani ya moyo wako na hutaki kubadilika?.

Ndugu maneno ya Bwana YESU ni kweli na amina, hasemi UONGO wala HATANII akisema atakutapika ni kweli atakutapika, hivyo mgeukie leo Bwana kikamilifu kama hujafanya hivyo toka katika kamba za kidini na madhehebu zinazokulewesha kukufanya ujione ni mkristo kumbe sio, tafuta kweli ya Neno la Mungu kwa gharama zote. Hili ndilo SHAURI la BWANA YESU KWAKO NDUGU wa Kanisa hili la Laodikia..

Ufunuo 3: 16 “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 NAKUPA SHAURI, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”

Ubarikiwe!

Tafadhali “washirikishe na wengine ujumbe huu”

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

ZIFAHAMU NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE SABA.

MAJI YA UZIMA.

MITUME WOTE WALIOPITA WALIKUWA NI WATU WEUPE, JE! NI KWELI NGOZI NYEUSI ILILAANIWA ?

SABATO HALISI NI LINI, JE! NI JUMAPILI AU JUMAMOSI?, NI SIKU GANI ITUPASAYO KUABUDU?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/09/11/agenda-kubwa-ya-shetani-kwa-kanisa-hili-la-laodikia/