MJUE SANA YESU KRISTO.

by Admin | 21 November 2018 08:46 am11

Moja ya jukumu la muhimu sana la kufanya baada ya kuzaliwa mara ya pili, ni kuzidi kumjua Yesu Kristo kwa undani, kwasababu Agano jipya lote linamuhusu Yesu Kristo, kiini chote cha biblia kinamuhusu Yesu Kristo, Agano la kale lilimuelezea Yesu Kristo kimafumbo lakini agano jipya limemwelezea kwa uwazi wote, Ukristo utakuwa haujakamalika kwa namna yoyote kama tutashindwa kumwelewa vizuri Yesu Kristo.

Tukishindwa kumwelewa Bwana Yesu , ni nani, kwanini alikuja duniani, anatendaje kazi, anataka nini kwetu, na sisi tunahitaji nini kutoka kwake, yuko wapi sasa hivi, anafanya nini n.k basi hatutaweza kumwelewa pia yule anayempinga yeye (Mpinga-Kristo) ni nani na anatoka wapi? Kadhalika Hatutaweza kujua mpinga-Kristo anatendaje kazi.

Kwasababu ni wazi kuwa huwezi kumjua adui ya mtu kabla hujamjua huyo mtu mwenyewe, hakuna mtu anayeweza kufahamu maadui wa mtu asiyemjua, sharti kwanza amjue huyo mtu anapotokea na maisha yake ndani nje yalivyo ndipo aweze kuwatambua na maadui zake. Vivyo hivyo hatutaweza kumjua Mpinga-Kristo kama hatutamjua Yesu Kristo vizuri kwa undani.

Miaka mingi, sana kabla ya mwanadamu wala wanyama kuumbwa, Bwana Mungu alikuwa peke yake, alikuwa hana cheo chochote kwasababu katika hali ya kawaida, ili mtu awe na cheo sharti awepo mtu aliye chini yake.

Sasa Mungu kabla ya kuumba wanadamu wala malaika, kulikuwa hakuna mtu chochote chini yake wala juu yake, hivyo alikuwa hana cheo chochote, alikuwa ni yeye kama yeye tu! na alikuwa pia hana jina, kwasababu jina kazi yake ni utambulisho kwa wasio kujua, hivyo yeye wakati huo alikuwa hana bado wasio mjua wala wanaomjua, hivyo alikuwa ni yeye kama yeye,Na ndio maana alimwambia Musa jina lake ni “MIMI NIKO AMBAYE NIKO”..sasa hilo sio jina kama ukilitafakari kwa makini, bali ni sentensi inayojaribu kuelezea uwepo wa Mungu. Hapo ni Bwana alikuwa akijaribu kumweleza Musa nafasi yake aliyokuwepo nayo kabla ya uumbaji wa kitu chochote kile.

Sasa ulipofika wakati wa uumbaji alipoanza kuumba malaika, ndipo hapo akaanza kuitwa Mungu, kwasababu maana ya Neno Mungu ni “mtengenezaji/au muumbaji” ndipo vikawepo viumbe chini yake vilivyoumbwa na yeye, viumbe hivyo vikaanza kumwita yeye Mungu, lakini kabla ya hapo alikuwa haitwi Mungu. Kwasababu hata katika maisha ya kawaida, Mtu hawezi akaitwa Baba kabla hajapata watoto, siku atakapopata watoto ndipo hapo atakapoitwa Baba au Mama, na ndivyo ilivyokuwa kwa Mungu hakuitwa Mungu, mpaka siku alipoumba.

Na ulipofika wakati wa mwanadamu kuumbwa, ambao aliwaita watoto wake, Cheo chake kilizidi kubadilika na Kuwa Baba, hivyo akawa na vyeo viwili yaani Baba pamoja na Mungu mwenyezi, kwasababu sisi wanadamu tuliomwamini yeye, Mbele za Mungu wetu ni kama watoto wake, Malaika sio watoto wa Mungu, bali sisi wanadamu ndio tunaoitwa watoto wa Mungu..

Waebrania 1:5 “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?” .

Hivyo ulipofika wakati wa Yeye kujidhihirisha kama Baba ni pale alipowatoa wana wa Israeli kutoka Misri akafunua jina lake kama YEHOVA,(Kutoka 6:1-6) Kwahiyo jina la Baba likawa ni YEHOVA, lakini ndio yule yule Mungu mwenyezi na ndio yule yule Baba Yetu. Aliwaokoa wana wa Israeli kama watoto wake kutoka katika mikono ya Farao kwa jina lake Yehova.

Kutoka 4:22 “Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, MPE MWANANGU RUHUSA AENDE, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako”.

Hosea 11: 1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, NIKAMWITA MWANANGU ATOKE MISRI”.

Unaona Sasa kwasababu Israeli ni Mzaliwa wa Kwanza, ni lazima awepo mzaliwa wa pili, na huyo sio mwingine zaidi ya watu wa mataifa, Hivyo watu wa Mataifa nao pia waliingizwa katika neema hii ya kuitwa wana wa Mungu..

Warumi 9:23 “tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;

24 ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ILA NA WATU WA MATAIFA PIA?

25 Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu.

26 Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, NINYI SI WATU WANGU, HAPO WATAITWA WANA WA MUNGU ALIYE HAI”.

Lakini kama tunavyojua agano la kwanza halikuweza kumkamilisha mwana wa kwanza (wana wa Israeli) kuwa mkamilifu, kadhalika lisingeweza pia kumkamilisha mwana wa pili (yaani watu wa mataifa) kuwa wakamilifu, hivyo Bwana Mungu mwenyezi akatengeneza njia nyingine ya kuwakamilisha wana wake wote wawili (yaani wayahudi na watu wa mataifa), ambayo katika hiyo watakuwa wakamilifu kweli kweli…. Na ndio hapo akauvaa mwili yeye mwenyewe YEHOVA na kuwa mwanadamu, ili kuwa kipatanishi kati ya wanadamu na nafsi yake mwenyewe.


Akauvaa mwili akazaliwa kama mwanadamu, akatembea kama mwanadamu akaishi kama mwanadamu, akajinyenyekeza kama mwanadamu, hakufanya vile kwa wazi bali alifanya kama siri mpaka utakapofika wakati wa kufunuliwa kwa siri hiyo, kwamba Yesu Kristo alikuwa ni Yehova mwenyewe katika mwili wa kibinadamu, na ndio maana Malaika Gabrieli alimwambia Bikira Mariamu amwite jina lake YESU, sasa tafsiri ya jina Yesu kwa kiebrania ni YEHOVA-MWOKOZI, kwahiyo ni yule yule YEHOVA KATIKA MWILI WA KIBINADAMU, Isipokuwa Jina lake limeongezeka na kuwa YEHOVA-MWOKOZI hivyo amekuja kwa kuokoa. Siri hiyo hawakufunuliwa watu wote isipokuwa wale ambao Bwana alipenda kuwafunulia. Na ndio maana Mtume Paulo aliileza siri hiyo kwa ujasiri katika..

1 Timotheo 3: 16 “Na bila shaka SIRI YA UTAUWA NI KUU. Mungu alidhihirishwa KATIKA MWILI, Akajulika kuwa na HAKI KATIKA ROHO, Akaonekana na malaika, AKAHUBIRIWA KATIKA MATAIFA, AKAAMINIWA KATIKA ULIMWENGU, AKACHUKULIWA JUU katika utukufu”.

Unaona hapo Mtume Paulo anamzungumzia Yesu Kristo, Mungu katika mwili, lakini anasema ni SIRI?

Sasa unaweza ukajiuliza kama Yesu alikuwa ni Mungu katika mwili kwanini aliruhusu watu wamwite yeye mwana wa Mungu? au aruhusu kujulikana kama mwana wa Adamu? Au mwana wa Daudi?.

Bwana Mungu, alipouvaa mwili wa kibinadamu, alijishusha kuwa mdogo sana, sasa mtu hawezi kujishusha na kuwa mdogo na bado atafute kuitwa mkubwa, bila shaka atakuwa ni mnafki. Ndio maana aliwaambia wanafunzi wake, mimi mnaniita Bwana na ndivyo nilivyo lakini sikuja kutumikiwa bali kutumika, na akawaambia mtu akitaka kuwa mkubwa kuliko wote basi awe mtumishi wa wote, hivyo yeye alikuwa kielelezo namba moja cha maneno hayo,

Ili kuelewa vizuri hebu jaribu kutafakari mfano huu, kulikuwa na tajiri mmoja mwenye mali nyingi sana, na mwenye makampuni mengi na wafanya kazi wengi sana, na wengi wa wafanyakazi wake walikuwa hata hawamjui kwa sura kutokana na ukuu wake, wengi walikuwa wanamsikia tu, lakini yule tajiri akaona kuna kasoro Fulani katika moja ya makampuni yake yaliyopo katika moja ya majimbo yake, akasikia kwamba kwenye moja ya hilo kampuni lake, wafanya kazi wananyanyaswa hawalipwi mishahara yao kwa wakati, na kuna ubadhilifu wa fedha mahali Fulani, sasa yule tajiri akaona njia pekee ya kwenda kutafuta suluhisho la hilo tatizo na kujua ukweli wa Mambo sio tu kutuma mawakili wake, bali akaona njia pekee ni kujibadilisha na kutoka kwenye ukurugenzi wake, na kusafiri mpaka kwenye hiyo nchi ambapo kampuni lake lipo na kwenda kujifanya kama nayeye anatafuta ajira ndani ya hilo kampuni, na akishapata naye awe kama mmoja wa watumwa wadogo wa lile kampuni walioajiriwa,..

Sasa kwasababu yeye yupo pale sio kwa kutafuta ukubwa bali kwa kutafuta chanzo cha tatizo, hivyo hawezi kuanza kujitangaza kwamba yeye ndiye Mmiliki wa lile kampuni, hapana bali atafanya mambo yake kwa siri siri, atajifanya mtumwa, na zaidi ya yote, atazitii zile sheria ambazo yeye ndiye aliyezipitisha katika enzi zake, kama vile sio yeye aliyezipitisha, atakipa heshima kile cheo cha mkuu wa makampuni kama vile sio chake, mpaka utakapofika wakati wa yeye kuondoka labda ndio atawaambia moja wa wafanyakazi wake kwamba YEYE NDIYE MKUU WA MAKAMPUNI YALE. Hapo ni baada ya kile alichokuwa anakitafuta kukipata.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu Kristo, yeye alikuwa ni Mungu katika mwili, isipokuwa katika SIRI asingeweza kujiita Mungu kwa namna yeyote ile, alikubali kuitwa mnazareti, alikubali kuitwa mwana wa Mungu, alikubali kuitwa mwana wa Yusufu, alikubali kuitwa mwana wa Daudi , n.k ingawa yeye hakuwa mwana wa Yusufu wala mwana wa Daudi.. kwasababu yeye mwenyewe mahali Fulani aliwauliza mafarisayo…

Mathayo 22:41 “Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo?

42 Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi.

43 Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema,

44 Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako?

45 Basi, DAUDI AKIMWITA BWANA, AMEKUWAJE NI MWANAWE?

46 Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.”

Unaona hapo Bwana anawauliza mafarisayo kama yeye ni mwana wa Daudi, inakuwaje tena Daudi anamwita Kristo Bwana? Kwahiyo unaweza ukaona Bwana Yesu Kristo, kujidhihirisha kama mwanadamu, au kama mwana wa Mungu, au kama mwana wa Yusufu haimaanishi kwamba yeye ni mwanadamu au yeye ni mtoto kweli wa Daudi au yeye ni mtoto kweli wa Yusufu, au yeye ni wa ulimwengu huu.

Hivyo Baada ya Mungu kumaliza kazi ya upatanisho kwa njia ya msalaba pale Kalvari, alirudi katika enzi yake kama Mungu Mkuu, lakini akaituma Roho yake kama Roho Mtakatifu, ambaye ndio yeye mwenyewe lakini katika mfumo wa Roho, kwa namna ya kawaida huwezi kumtenganisha Mtu na Roho yake, mahali mtu alipo ndipo na Roho yake ilipo, huwezi ukasema mtu na Roho ni vitu viwili tofauti hapana ni kitu kimoja, na ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, ni yeye yule aliyekuwa kama Baba mbinguni, kisha akajidhihirisha kama mwana duniani, na sasa yupo pamoja nasi kama Roho Mtakatifu.

Na jina lake ni lake ni YESU KRISTO (YAANI YEHOVA-MWOKOZI). Ana nafsi moja tu, Na hatujapewa jina lingine litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina lake YESU KRISTO, kwa jina hilo tunapata msamaha wa dhambi, na kufunguliwa vifungo vyetu, kwa jina hilo tunabatiziwa, kwa jina hilo tunatolea pepo, kwa jina hilo la Yesu tunatenda mambo yote ya mwilini na rohoni. Na wala hapana wokovu kwa mwingine yoyote isipokuwa kwa Mungu wetu (YESU KRISTO, MUNGU MKUU BWANA WA UTUKUFU).

Kwahiyo Mtu akimkataa Yesu Kristo, amemkataa Mungu mwenyewe, mtu akimpinga Yesu Kristo amempinga Mungu mwenyewe.

Kaka/Dada leo hii umefahamu kuwa Yesu ndiye Mungu, mtazamo wako juu yake upoje? Yeye ndiye atakayeketi katika kiti chake cha enzi na kuhukumu mataifa yote. Jifunze sana kumjua huyu kwasababu yeye ndio Njia pekee ya kuufikia uzima wa milele sio kuwa na dini wala dhehebu au kujiunga na mojawapo ya hayo, njia pekee ya kuupata uzima wa milele ni kumwamini yeye na kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi na maisha ya kale, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina lake hilo “Yesu Kristo” kulingana na ( Matendo 2:38. Mdo 8:16, mdo 19:5 na Mdo 10:45) Na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu. Ni maombi yangu kwamba Bwana atakukirimia neema yake kuyapata hayo na kuzidi kumfahamu sana yeye..

Waefeso 4: 13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo”.

Ubarikiwe!

Tafadhali “share ” ujumbe huu kwa wengine.

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

TUZIJARIBU HIZI ROHO.

MAISHA YETU NI MILKI YA YESU KRISTO.

ITAMBUE KARAMA YA MUNGU.

UMEPATA UHAKIKA WA KUTOKUINGIA HUKUMUNI KATIKA SIKU ILE?

JE! ADAMU ALIWASALIANA NA MUNGU KWA LUGHA IPI PALE BUSTANINI?

JE! KUCHORA TATTOO NI DHAMBI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/11/21/mjue-sana-yesu-kristo/