MAFUNDISHO YA MASHETANI

by Admin | 1 January 2019 08:46 pm01

1 Timotheo 4 : 1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

Biblia inasema, nyakati za mwisho wengine, watajitenga na IMANI, Imani inayozungumziwa hapo si imani nyingine zaidi ya Imani katika Yesu Kristo.

Mungu alimuumba mwanadamu na sehemu mbili, Sehemu ya Roho na Sehemu ya mwili.

Sehemu ya mwili ndio hii tunayoiona kwa macho, milima, mabonde, miti, nyumba, bahari, wanadamu, wanyama n.k. Na sehemu ya Roho hatuioni kwa macho, imefungwa kwetu wanadamu.

Sehemu hii ya Roho ndio mahali Mungu, anapoonekana, na ndio mahali malaika wanapoonekana na ndio mahali shetani na malaika zake wanapoonekana, ndio mahali vita vinapopiganwa na ndio mahali vyanzo vya mambo yote vinapotokea.

Sasa baada ya Adamu kuanguka, Bwana hajaruhusu tuingie katika ulimwengu wa Roho, hakuruhusu macho yetu ya Roho yafumbuliwe tuone kila kitu kinachoendelea katika ulimwengu wa Roho.Na endapo tungefumbuliwa macho tuone mambo gani yanaendelea katika ulimwengu wa Roho duniani kusingekuwa mahali pa kukalika, kwasababu tungekuwa tunaona mambo mengi mno ya ajabu, na kila siku tungekuwa tunaona mambo mapya. Tungekuwa tunaona mambo mengine ambayo yangekuwa hata hayatusaidii..Ingekuwa ni dunia iliyojaa vurugu mno. Kwasababu ulimwengu wa Roho umejaa mambo mengi.

Tuchukue mfano, wakati ule Nabii Elisha alipomwomba Mungu amfungue macho Yule mtumwa wake, na alipofunguliwa macho aliona kilima chote kimejaa jeshi la malaika wenye upanga..Sasa kumbuka malaika hata siku moja hawapigani na wanadamu, bali wanashindana na majeshi ya mapepo wabaya.. kwahiyo kama kulikuwa na majeshi ya malaika wa mbinguni, ni wazi kuwa yalikuwepo pia majeshi ya mapepo yaliyokuwa tayari kushindana na lile jeshi la malaika, kwahiyo kama Bwana angeruhusu Yule mtu aendelee kuona yale mambo ya rohoni ni wazi kuwa angeona vita viwili vinaendelea, vya kwanza vya malaika na vya pili vya wanadamu.

2 Wafalme 6: 15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.

mafundisho ya mashetani

Kwahiyo unaweza ukaona kuwa ulimwengu wa Roho, wa malaika upo, na una mambo mengi mno, yasiyoelezeka na mengine ni magumu kuyatambua, yamekaa kimafumbo jaribu kufikiri Yohana aliyeandika kitabu cha ufunuo anaona malaika wana Uso wa TAI, mwingine ana kichwa cha NDAMA, mwingine ana kichwa kama cha SIMBA na bado wana mabawa, na wana kwato!! Umewahi kujiuliza hivyo viumbe endapo tukiwa tunaviona kila siku duniani kutakuwaje?? Nabii Ezekieli naye alionyeshwa mambo hayo hayo,Nabii Isaya naye alionyeshwa mambo hayo hayo, lakini hawakuyaelewa kwa undani mambo hayo kwasababu ni mambo ya Rohoni.

Kwahiyo ni wazi kuwa Sio mpango wa Mungu, tuwe na uwezo kila dakika kuyaona mambo ya rohoni, vinginevyo maisha yatakuwa hayana maana.

Lakini maandiko yanasema Yohana 4.23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 MUNGU NI ROHO, NAO WAMWABUDUO YEYE IMEWAPASA KUMWABUDU KATIKA ROHO NA KWELI.”

Sasa hapa ndipo pa kuzingatia sana, maana pasipoeleweka vizuri, ni rahisi shetani kumzamisha mtu katika MAFUNDISHO YA MASHETANI.

Biblia inasema “saa yaja ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli”

Biblia iliposema “katika roho na kweli” haikumaanisha kuwa itafika wakati tutakuwa tunazama katika ulimwengu wa roho na kufikia kumwona Mungu na malaika, na hatimaye kumwabudu tukiwa tunamwona wazi kama tunavyowaona mwanadamu wenzetu.. Hapana haikumaanisha hivyo…

Na Shetani ndipo alipoanzia hapa kupandikiza mafundisho yake ya mashetani.

Nini maana ya kumwabudu Mungu katika ROHO NA KWELI?

Kabla ya kujua maana ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli, hebu turudi nyuma kidogo…Kumbuka kama tulivyosema ulimwengu wa Roho ni ulimwengu wa Malaika, ikiwa na maana kuwa vita vyote na mambo yote yanayoendelea katika ulimwengu wa Roho Mungu huwa anawatumia malaika zake kuyafanikisha, mambo hayo namna ya kuyafanya na jinsi ya kuyafanya hayamuhusu mwanadamu hata kidogo sio sehemu ya mwanadamu..Ni kazi ya malaika Kwamfano Mungu alipomtuma Malaika Gabrieli kwa Mariamu kumpa taarifa za kuzaliwa kwa Mwokozi Bwana Yesu Kristo namna ya kuitengeneza ile mimba tumboni mwa Mariamu pasipo Mwanaume kuhusika haikuwa kazi ya Mariamu, au mwanadamu yoyote yule bali ilikuwa ni kazi ya Malaika wa Mungu katika uwezo wa Roho.

Mungu alipoyaleta yale mapigo yote kwa farao, na kuwaongoza katika lile jangwa kimiujiza haikuwa kazi ya mwanadamu kuyatengeneza yale mapigo..mwanadamu alikuwa na kazi yake tutakuja kuiona mbele kidogo.

Kadhalika kazi ya kuleta tauni katikati ya watu wakati wa Mfalme Daudi haikuwa kazi ya wanadamu bali ilikuwa ni kazi ya Malaika wakifanya kazi katika ulimwengu wa roho..Hao ndio Bwana aliowatia mafuta kuweza kufanya mambo makubwa yasiyowezekana kwa namna ya kawaida.

Sasa mwanadamu ambaye anamcha Mungu hajapewa maarifa hayo, mwanadamu anayemcha Mungu hajapewa uwezo wa kuingia kwenye ulimwengu wa roho na kutengeneza mambo au kuingia na kupambana na roho za malaika walioasi.

Sasa uwezo mwanadamu anayemcha Mungu aliopewa na Mungu ni mwongozo wa namna ya kuwafanya hawa malaika waweze kumhudumia yeye. Mwongozo wa namna ya kutembea na kundi hili la malaika watakatifu.

Ni sawasawa na mwanadamu na Farasi, mwanadamu hajapewa uwezo wa kukimbia kwa kasi kama farasi, hajapewa mapafu kama ya farasi, lakini amepewa uwezo wa kumwongoza Yule farasi amtii yeye ampeleke katika mwendo anaotaka..

Na huo mwongozo mwanadamu aliopewa utakaomsaidia yeye kutembea na malaika walio na nguvu na uwezo katika ulimwengu wa Roho ni BIBLIA TAKATIFU (yaani NENO LA MUNGU). Ni kama tu Mtu asiyekuwa na MANUAL ya kuendesha gari, hataweza kuliendesha gari hilo hata iweje, kadhalika mtu ambaye hajafundishwa namna ya kumpanda farasi na kumwendesha hataweza kumwendesha, badala yake anaweza akajikuta hata akajeruhiwa na Yule farasi farasi.

Naamini kidogo kidogo utakuwa umeshaanza kuelewa nini maana ya kuingia katika ROHO…Kwahiyo maana ya kuingia katika roho sio kugeuka na kuanza kujifananisha na malaika, au mapepo hapana bali ni kuelewa uwezo uliopewa wa kutembea na malaika ambao hao ndio wanaojua namna ya kutengeneza mambo katika ulimwengu wa roho.

Kwasababu hiyo basi Mwanadamu anayemcha Mungu hawezi akajua njama za adui zote na elimu yake kwa mapana na marefu, hawezi akajua idadi ya mapepo yaliyopo, hawezi akajua yanafanyaje fanyaje kazi..malaika watakatifu ndio wanaojua (wamepewa uwezo huo na Mungu mwenyewe) ..Sisi tunachojua tu tukitaka tulindwe na Yule adui Kwanza tumwamini Bwana Yesu Kristo, kisha tukabatizwe kisha tuishi maisha matakatifu na ya uangalifu, tukidumu katika kusali na ushirika. Hiyo inatosha kabisa kuwafanya wale malaika watakatifu watupiganie dhidi ya mapepo wabaya.

Tukitaka tusife tuishi maisha marefu, wale malaika Bwana aliowapaka mafuta katika ulimwengu wa Roho wanajua namna ya kumzuia shetani na mapepo wake wasituguse mpaka tutakapotimiza umri wa kuondoka duniani, hivyo kama maandiko yanavyosema “waheshimu baba yako na mama yako upate siku nyingi na za heri” hivyo wale malaika watakatifu wanatembea na mtu anayelishika neno hilo, na mtu Yule anajikuta anakingiwa na ajali na dhiki za Yule mwovu na kutimiza umri wa maisha yake..Sasa huyu mtu tayari kashaingia katika roho. Anakuwa anamwabudu Mungu katika roho na kweli. Kwasababu maneno ya Yesu Kristo ndio Roho. (Yohana 6:63)

Au mtu wa Mungu anapoumwa wale malaika wanaohusika na uponyaji, waliohusika na kuitengeza mimba ya Mariamu pasipo mwanamume kwa uwezo wa roho ndio hao hao pia wana uwezo wa kuondoa ugonjwa pasipo daktari lakini wanafanya kazi na mtu anayeliaimi neno hili “kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

Kwahiyo hizo ndizo silaha zetu sisi katika ulimwengu wa Roho, kulishika NENO la Mungu pamoja Na kuwa na IMANI katika Neno lake.

Na ndio maana Mtume Paulo alisema katika..

Waefeso 4: 11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni NENO LA MUNGU;”

Unaona hapo? Ukilijua Neno la Mungu kwa undani,wewe tayari ni Mtu wa rohoni, ambaye unashindana vita visivyoonekana kwa macho na unashinda, hauna haja ya kuona mapepo, hauna haja ya kuona wachawi, hauna haja ya kuona majini, vibwengo, hauna haja ya kumwona hata shetani mwenyewe,..na zaidi ya yote hauna haja ya kuwaona hata malaika..Wao wanafanya kazi zao katika ulimwengu wa roho ambao wewe ndio unaoupalilia kwa kulishika na kuliamini Neno la Mungu..

Sasa mafundisho ya mashetani leo ni yapi?

Mafundisho ya mashetani ni yale yanayokufundisha kwamba unaweza ukaingia katika ulimwengu wa roho na wewe ukashindana na mapepo kama wanavyofanya malaika…Ndio hapo shetani anatumia nguvu kubwa kuwavuta watu wasilijue Neno la Mungu, na kuwafanya wakeshe kutafuta kujua elimu za mapepo, utakuta anawafundisha watu aina za mepepo na majini, na utendaji wao kazi. Wengine wanawafundisha watu wasile vyakula Fulani au wasipande miti Fulani majumbani mwao, kwasababu vina uhusiano wa moja kwa moja na mapepo n.k.

Wengine wanafundisha watu kwamba usiende kuogelewa baharini au mtoni saa 7 au kabla ya kuogelea baharini, kemea kwanza pepo la maji, kwamba kabla ya kupita karibu na makaburi kemea kwanza pepo la mauti lisije likakuingia, unapokaribishwa kwa mtu usiyemjua usile kwanza chakula Fulani, kwamba ukiona mtu kakuamkia na kukuonyesha ishara Fulani, kemea hilo ni pepo la mauti, unapougua kichomi basi umetumiwa jini Fulani n.k..

Unapofika mahali Fulani usipende kutenda wema, nyota yako itachukuliwa n.k nataka nikwambie ndugu hizo zote ni ELIMU ZA MASHETANI.!!

Sisi tuliompa Bwana Yesu Kristo maisha yetu tunafahamu Neno moja tu!! Nalo ni hili “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Hesabu 23:23”. Hiyo ndio silaha tuliyo nayo sisi..Ni namna gani inatenda kazi?? Hatujui Malaika ndio wanaojua…wao ndio wanaojua kuna aina ngapi za vibwengo, na wachawi, na mapepo na namna ya kuwashughulikia sisi sio kazi yetu kujua aina za mapepo na utandaji kazi wao…

Tunapotenda wema na kuambiwa nyota zetu zitachukuliwa…hilo hatulijui sisi tunachojua ni kwamba.. “hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyetu utakaopotea, na nywele zetu zote zimehesabiwa Luka 21:18” Ni kwa namna gani hilo linatenda kazi? Hiyo sio kazi yetu kujua, Malaika watakatifu ndio waliobobea katika mambo ya rohoni hao ndio wanazo hizo teknolojia ya kuzihifadhi nyota zetu kama zipo, sisi hatuna huo uwezo. Sisi kazi zetu ni kulishika Neno lake tu!

Biblia inatuonya hizi elimu/mafundisho siku za mwisho yatakuwa mengi, yakiwatoa watu katika Imani lengo ni kuwafanya watu wajitenge na Imani, . Na badala ya kumfungua mtu, utakuta ndio zinamfunga na kumfanya awe mwoga wa wokovu wake, Hata siku moja Mungu hamletei mtu hofu, bali ujasiri, utakuta watu wamehama nyumba zao kwa kuogopa zimezindikwa na wanahubiriwa hivyo na wanaojiiita watumishi. Wengine kila kukicha ni kufundishwa utendaji kazi wa mapepo tu!! Kila kitu kitakachokuja mbele yako ni kukemea, ukiingia hospitali kemea, kabla ya kulala mwaga damu ya Yesu chooni, mapepo yasikuvae, saa kumi jioni majini aina Fulani yanafunguliwa hivyo usipende kula kitu Fulani huo wakati. Na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo, kila kitu ni mapepo mapepo tu!!

Dada/Kaka unayesoma haya, tafuta kulijua Neno la Mungu na kuliamini, hayo mengine sio kazi yetu kujua, Mtafute Bwana alisema katika Neno lake Maneno yake ndiyo Roho na Uzima(Yohana 6:64)…na maneno yake sio mengine zaidi ya Biblia takatifu, kwahiyo kwa lugha nyingine unaweza kusema biblia takatifu ndio Roho na uzima..Hivyo kuwa mtu wa rohoni ni kuyaishi na kuyaamini maneno ya Yesu Kristo 100% na si kingine.

Kama unataka leo hii uwe mtu wa rohoni, mtii leo maneno yake anayokuambia, kwa kukusudia kutubu dhambi zako kabisa kwa kumaanisha kuacha uasherati wako, kwa kukusudia kuacha pombe zako, uvaaji wako mbaya {vimini, surali,wigi,wanja,lipstick, herein n.k}, kwa kumaanisha kuacha wizi wako, utukanaji wake, rushwa zako, usengenyaji wako n.k Ili uwe na uhakika wa kuurithi ufalme wa mbinguni na kuruhusu Malaika wa Bwana watembee na wewe siku zote za maisha yako, na kuepukana na mafundisho ya mashetani

Mungu akubariki

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kama umempa Bwana maisha yako, tafadhali tangaza habari zake kwa kadri uwezavyo kwa watu wengine wasiomjua yeye.


Mada zinazoendana


SHETANI NI NANI?

 DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI NI IPI?

HUDUMA KUMI (10) ZA SHETANI DUNIANI NI ZIPI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/01/mafundisho-ya-mashetani/