NJAA IPO?, USIACHE KULA ASALI.

by Admin | 1 January 2019 08:46 pm01

NJAA inaficha uchungu wa kitu, mtu mwenye njaa hata akipewa mboga iliyochungu kiasi gani, bado ataiona ni tamu tu, kwasababu NJAA ipo ndani yake, lakini kwake yeye aliyeshiba, hata chakula kiungwe kwa viungo vingi kiasi gani bado ataona tu kuna kasoro nyingi ndani yake..Ni kwasababu njaa haipo ndani yake.

Unaweza ukajiuliza ni kwanini Neno la Mungu linafananishwa na ASALI? Sababu ni hizi kwanza Asali ni kitu kitamu kuliko vyakula vyote na matunda yote, pili asali ni chakula kisichoharibika kinadumu milele, ni kitu kisichoisha ubora wake kwa mamilioni na mamilioni ya miaka ipo vile vile tofauti na kitu chochote kile kinachoweza kulika, Bwana anasema:

“Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo. 14 Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika.” (Mithali 24: 13)”.

Lakini japo asali ni tamu kuliko vitu vyote kamwe hatuwezi kuuona utamu wake pale nafsi zetu zikiwa zimejikinai, tukijiona kuwa tunajua, tumefika, hakuna mtu anayeweza kutuongezea kitu cha ziada katika ukristo wetu ni dini zetu tu, tukijiona kuwa sisi ni bora kuliko wengine,

tunawadharau wengine wote, hatutaki kuwasikiliza wala kuwahudumia?, tunasema wale sio wa dhehebu letu, hivyo hatuwasikilizi hawana chochote cha kutuongezea, n.k. ..

Hapo hata kama tutalifahamu Neno la Mungu kwa wingi kiasi gani, hata kama tutakuwa na mafunuo mengi kiasi gani, hata kama tutahubiri mikutano mingi kiasi gani, hata kama tutawaombea wagonjwa wakapona kiasi gani..ULE UTAMU WA NENO LA MUNGU HATUTAUHISI KAMWE NDANI YETU.

Na ndio hapo mtu wa namna hiyo anaishia kuwa wa kidini tu, kama wale mafarisayo na masadukayo, walivyokuwa kipindi kile cha Yesu. Walimwona Bwana kama mtu asiyekuwa na dini, wala elimu, walimwona Bwana kama mtu mwenye pepo, walimwona Bwana kama mwana wa Seremala maskini tu asiyejua kitu, , hivyo pale alipokuja na Neno la Uzima kutoka kwa Mungu, walimdharau japo waliufahamu kuwa anachosema ni ukweli lakini kwa kuwa waliridhika tu na dini zao na mapokeo yao, walikuwa wameshiba nafsini mwao, wakaupinga wokovu…..kwani hekima inasema:

“Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.” (Mithali27:7).

Embu leo hii, turuhusu nafsi zetu ziwe na NJAA kwa ajili HAKI na KWELI ya Neno la Mungu Ili endapo maagizo yanayoonekana kuwa ni magumu yatokayo katika Neno la Mungu yatakapokuja mbele yetu tuyaone kuwa ni matamu hata kama yataonekana kuwa ni machungu kwa watu wengine, walioshiba. Pale biblia inapotuagiza mara baada ya kuamini kwetu tukabatizwe kwa kuzamishwa katika maji tele,na katika jina la YESU basi sisi tuwe wepesi wa kutii,maadamu nafsi zetu zina njaa ya haki, hata kama tutaona kisima, au mto au bahari vipo mbali nasi basi tufanye hivyo tu kwasababu Roho zetu zina njaa..Tufanye kama yule Mkushi aliyehitaji kubatizwa akiwa njiani, katika safari yake.

Matendo 8: 35 “Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza”.

Tusifanane na hao walioshiba, wameshakinai sega la asali ambao pamoja na elimu zao kubwa za dini wakilijua hilo wamelipuuzia kama jambo lisilo na umuhimu sana.

(Luka 6:21 Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba.)

Pale biblia inapotuonya tuvae mavazi ya kujisitiri, na tusivae mavazi yaipasayo jinsia tofauti (kumb 22:5). Basi tuone kuwa hicho ni chakula kitamu kwa kutii haraka sana, kwa kwenda kutupa vimini, na suruali, na kaptura ambazo ni za jinsia tofauti na za kwetu [wanawake]. Sisi tusifanane na hao walioshiba wanaosema Mungu haangalii mavazi bali roho, tukiwaacha wale waliojikinai wanaosema tunaishi chini ya neema na wala sio sheria..Sisi tuziache tu nafsi zetu ziwe na njaa..ndipo tutakapoliona Neno la Mungu ni tamu kwetu.

Tuwe kama Daudi, anasema “MAUSIA YAKO NI MATAMU SANA KWANGU, KUPITA ASALI KINYWANI MWANGU Zaburi 119:103.”

Pale biblia inapotuonya tusiabudu sanamu wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala chini duniani, basi moja kwa moja tusijione kuwa dini zetu ni bora kuliko Neno la Mungu, tusione kuwa viongozi wetu wa dini ni bora kuliko Neno la Mungu, tusione kuwa dhehebu letu ni zaidi ya Neno la Mungu na kupuuzia, na kuzidi kuabudu sanamu za wafu na kuzifanyia ibada na kusali rozari za kipagani vitu ambavyo Neno limekataza. Sisi tutii tu hata kama dini zetu zinatukemea. Kwasababu tunataka kwenda mbinguni.

Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”

Tule asali sana maadamu tuna njaa, lakini ole wetu endapo tumeshiba, kwani ni jambo gani litakalotuburudisha lenye utamu zaidi ya asali?.

Dumu katika Neno la Mungu.

Ubarikiwe DAIMA wewe umtafutaye BWANA.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

UBATILI.

WANA WA MAJOKA.

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/01/njaa-ipo-usiache-kula-asali/