DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?

by Admin | 2 January 2019 08:46 am01

Je Damu ya yesu inanenaje mema kuliko ya habili?..Nini madhara ya kuidharau sauti ya Damu ya thamani ya Yesu Kristo?

Shalom! karibu tujifunze Neno la Mungu kwa pamoja, Leo tutajifunza juu ya damu ya YESU kwa ufupi. Naamini utaongeza kitu juu ya vile ulivyojaliwa kuvijua na Bwana..

Tukisoma katika kile kitabu cha Mwanzo, tunamsoma Kaini aliyemwua ndugu yake Habili, kwasababu sadaka yake haikukubaliwa na Mungu, na ya ndugu yake kukubaliwa..Habari hiyo tunaisoma katika kitabu cha…

Mwanzo 4: 8 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.

9 Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?

10 Akasema, Umefanya nini? SAUTI YA DAMU YA NDUGU YAKO INANILILIA KUTOKA KATIKA ARDHI.

11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;

12 utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao”.

Tunaona hapo Bwana alimwambia Kaini “sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.”..kumbuka haikusema “sauti ya roho ya ndugu yako”, hapana bali ilisema “sauti ya damu”..ikiwa na maana kuwa damu ina sauti na inanena.

Pia haikusema “sauti ya damu inanililia kutoka mbinguni”..bali ilisema “sauti inanililia kutoka katika ardhi”..kwahiyo kuna uhusiano pia wa damu na ardhi..tutakuja kuiona huko mbeleni..

Lakini pia tukisoma kitabu cha Waebrani Mlango 12: 24 inasema “Na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, INENAYO MEMA kuliko ile ya Habili”.

Hapa tunaona kuna damu mbili ya Kwanza ni ya Habili na ya pili ni ya Bwana Yesu…Lakini tunasoma damu ya YESU KRISTO inanena mema kuliko ile ya Habili.

SASA DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?
Habili tunamsoma alikuwa ni mtu wa Haki, na alienda katika ukamilifu, hata akapata ufunuo bora wa kumtolea Mungu sadaka, na zaidi ya yote alimtolea katika sehemu zilizonona na katika wazaliwa wa kwanza wa wanyama wake…Ikionyesha kabisa kuwa alikuwa ni mtu wa Haki aliyemjali Mungu, na kumfanya Mungu kuwa wa kwanza katika maisha yake..Na pia alikuwa anakwenda katika maagizo yake na sheria zake…Na hivyo mpaka kufikia wakati anauawa na ndugu yake, hakuwa na hatia yoyote na hivyo damu yake ikawa ni kama damu ya mtu asiyekuwa na hatia..Na ilipofika ardhini ikaanza kutoa sauti ikimlilia Mungu..

Na kadhalika Bwana Yesu Kristo, aliuawa pasipo hatia yoyote, yeye hakuwa na kosa lolote hata kuuawa pale Kalvari,

Matendo 4: 25 “Nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili?
26 Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.
27 Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu YESU, ULIYEMTIA MAFUTA,”

damu ya Yesu

 Lakini Tunaona matokeo ya damu ya Habili kumlilia Mungu kutoka katika ardhi ni ndugu yake Kaini kulaaniwa juu ya ardhi na kuwa mtu mtoro asiyekuwa na kikao….Kwahiyo kwa ufupi damu ya Habili ilinena hukumu juu ya Kaini juu ya nchi.

Lakini tukirudi kwa upande wa Yesu Kristo, tunaona matokeo ya Damu ya Yesu Kristo hayakuwa hukumu kwa wale waliomwua..Bali yalikuwa ni rehema na msamaha, na kuhesabiwa haki bure kwa Neema..Na ndio maana Bwana kabla hajakata roho alimaliza na Kusema “Baba wasamehe” kwakuwa hawajui watendalo…lakini Habili hakusema hivyo, na zaidi ya yote Bwana Yesu alisema “Imekwisha” lakini Habili hakusema hivyo…Kwahiyo damu ya Yesu ni Bora kuliko ya Habili, Damu ya Yesu imetuletea msamaha wa dhambi badala ya hukumu, Damu ya Yesu imetuletea Baraka badala ya Laana..Kwahiyo Inanena mema sana..

Kwa ufupi wale wote waliomsulibisha Bwana Yesu Kristo pale msalabani, pamoja na sisi sote tunaomsulibisha sasa Yesu Kristo kwa matendo yetu, tulistahili kulaaniwa juu ya ardhi kama alivyolaaniwa Kaini na hata zaidi ya pale, kwasababu tulimwua Mwana wa Mungu asiyekuwa na hatia…Lakini kwasababu Damu yake inanena mema kuliko ya Habili..tumepata rehema badala ya Hukumu, ardhi imebarikiwa kwa ajili yetu badala ya kulaaniwa..zaidi sana tumepewa tumaini la uzima wa milele Haleluya!.

Huo ni msamaha wa kipekee sana, Hakuna mwanadamu yoyote duniani leo ambaye mwanawe mpendwa auawe kikatili tena pasipo hatia, halafu badala ya kuwalipizia kisasi wale wauaji,na kuwalaani anawabariki kupitia mauti ya mwanae..Huo ni upendo usio kuwa na kipimo.

Damu ya Yesu ilimwagwa juu ya ardhi hapa duniani, miaka 2,000 iliyopita na si mbinguni..ili inene mema kwa wanadamu wa vizazi vyote vya duniani. Kwa kupitia damu ya Bwana isiyoharibika, mambo yote yanafanyika kuwa mapya, na kwa kupitia damu ya Bwana tunakikaribia kiti cha Neema kwa ujasiri.

Tukiyajua hayo, ni wakati wa kujichunguza na kuogopa, na kutetemeka kwasababu kama tulistahili kulaaniwa kama Kaini lakini Bwana hajatulaani, sio wakati tena wa kuidharau hii DAMU YA THAMANI YA YESU KRISTO, sio wakati wa kujisifu kuwa tunajua..Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu ni kwamba Neema yote tunayoiona leo hii duniani ni kwasababu damu ya YESU bado inafanya kazi juu ya NCHI. Mvua tunazozipata kwa wakati ni kwasababu ya Damu ya thamani ya Yesu bado inafanya kazi, majanga tunayoepushwa nayo duniani ni kwasababu Damu ya Yesu bado inafanya kazi licha ya kwamba maasi ya sasa yamezidi yale ya Sodoma na Gomora lakini bado tunafaidika na neema hii kwa kitambo.,

tunavipindi vizuri vya usiku na mchana, na hewa safi ni kwasababu damu ya thamani ya Yesu ipo inayonena Mema.Unafuu wowote tunaouona duniani ni kwasababu ya Damu ya Yesu. Utafika wakati Hii damu itafikia mwisho wa kufanya kazi yake ya kunena na mambo mengine yatafunguliwa, kwasababu kumbuka sio wakati wote Mungu atakuwa anafanya kazi ya kuokoa, upo wakati wa mambo mengine kufunguliwa..hapo ndipo ile dhiki kuu itakapoanza…wakati huo hakuna mtu atakayeweza kununua wala kuuza pasipokuwa na chapa ya mnyama…wakati huo maji ya dunia nzima, na chemichemi zote zitakapogeuzwa kuwa damu, wakati huo ambao Jua litatiwa giza na nyota za mbinguni zitakapoanguka, wakati huo ambao gonjwa zito ya ajabu yataikumba dunia nzima,

Kipindi hicho sio cha kutamani kufika, ni kheri ujisalimishe Kwa Yesu Kristo leo kama hujafanya hivyo, kabla ya nyakati hizo, ukatubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi zako, usiidharau hii Neema iliyopo leo na kufanya dhambi kwa makusudi, na kama ulikuwa hujasimama imara katika wokovu wako huu ni wakati wa kuweka mambo yako sawa..Biblia inasema katika..

Waebrania 10: 26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, HAIBAKI TENA DHABIHU KWA AJILI YA DHAMBI;

27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.

28 Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 MWAONAJE? HAIKUMPASA ADHABU ILIYO KUBWA ZAIDI MTU YULE ALIYEMKANYAGA MWANA WA MUNGU, NA KUIHESABU DAMU YA AGANO ALIYOTAKASWA KWAYO KUWA NI KITU OVYO, NA KUMFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?

30 Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.
31 NI JAMBO LA KUTISHA KUANGUKA KATIKA MIKONO YA MUNGU ALIYE HAI.”

Ndugu yangu/kaka yangu unayesoma haya ambaye ni mlevi, ni mwasherati, unafanya anasa, unakula rushwa, unatazama pornography, n.k mambo hayo yote ni njia panda ya kuelekea kuzimu,Dada unayesoma haya..unayevaa vimini na suruali, unayepaka lipstick na wanja, unayevaa hereni na wigi na unayesokota dread, unayesikiliza na kushabikia miziki na fashion za kidunia..mambo yote hayo kama hautaamua kuyaacha yatakupeleka kuzimu.

Mkabidhi Bwana leo maisha yako kikamilifu, pasipo kuwa vuguvugu..ili damu ile izidi kunena Mema juu yako.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki,

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JE! MWANADAMU WA KWANZA KUUMBWA NI YUPI MZUNGU MWAFRIKA AU MCHINA NA KAMA NI MMOJAWAPO KATI YA HAO JE HAO WENGINE WAMETOKA WAPI?

JE!, INAKUBALIKA KUMTOLEA MTU MWENGINE DAMU?(BLOOD TRANSFUSION).

JE! ADAMU ALIWASALIANA NA MUNGU KWA LUGHA IPI PALE BUSTANINI?

BONDE LA KUKATA MANENO.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/02/damu-ya-yesu-inanenaje-mema-kuliko-ya-habili/