JAWABU LA MAISHA YA MTU.

by Admin | 2 January 2019 08:46 am01

Kwa muda mrefu Mfalme Sulemani aliingia katika kuchunguza hekima ya viumbe vyote duniani, mimea yote na kazi zote za wanadamu zinazofanywa chini ya jua hili ili kutoa jawabu moja ambalo kwa hilo litamfanya mwanadamu aweze kufungua milango yote ya BARAKA,na MAARIFA na UZIMA na AMANI katika siku zake zote aishizo hapa duniani. Mfalme Sulemani aliingia katika utafiti huo wa hali ya juu kwa wa muda mrefu sana, tangu ujana wake akiongozwa na ile hekima iliyokuwa ndani yake, biblia inasema alijaribu hata “upumbavu” mambo yasiyopaswa kufanywa na mtu yeyote wa Mungu, lakini yeye alifanya kwa kusudi tu la kulivumbua hilo jawabu pengine linaweza likawa limejificha ndani yake.. Jawabu ambalo litampa mwanadamu wepesi wa maisha, amani, furaha ya kudumu, utulivu, kuridhika,uzima, upendo n.k.

Uchunguzi huu wa Sulemani tunaweza kuusoma katika kitabu cha Mhubiri tukianzia mwanzoni kabisa tunaona Sulemani akieleza jinsi alivyoutia moyo wake kutafuta na kuchunguza hekima ili kupata jawabu hilo moja, hivyo ilimgharimu kujaribu kitu kimoja kimoja kinachoweza kutamanika hapa duniani, na kila alichokijaribu na kuona sio chenyewe chenye ufunguo wa maisha kwa kwa mwanadamu alisema ni UBATILI, hivyo akaendelea na kingine, kadhalika alipoona hicho nacho hakiwezi kumsaidia mwanadamu alisema ni UBATILI..hivyo akakiacha akaendelea na kingine, hivyo hivyo mpaka alipofanikiwa kujaribu kila kitu unachoweza kukifahamu hapa chini ya jua, hakuna ambacho hakukijaribu, mpaka kwa wachawi na miungu migeni alifika, hakuna kitu ambacho hakukijaribu Sulemani, alijaribu vyote, lakini vyote aliona ni ubatili na upotevu ni sawa na kuufuata na kujilisha Upepo, mpaka tunapokuja kusoma sasa kwenye sura ya mwisho kabisa ya kitabu cha Mhubiri baada ya Sulemani kwenda huku na kule, kufanya hichi na kile, kujaribu hichi na kile, ndipo mwisho wa siku anakuja kulipata JAWABU lenyewe alilokuwa analitafuta kwa muda mrefu, tangu ujana wake, lililomgharimu hata kuipoteza nafsi yake katika mambo yasiyompasa kuyafanya ili tu alipate na hatimaye akalipata jawabu hilo..Haikuwa kazi rahisi..

Ni sawa na wewe leo unakwenda kutafuta nguo yenye nyuzi za rangi 10 iliyoandikwa karatu katika soko la mitumba, itakugharimu kuchambua mtumba mmoja hadi mwingine mpaka uipate, na hiyo haitakuwa kazi ya kuisha ndani ya siku moja, utafukua mitumba na mitumba soko zima na pengine unaweza usiipate.

Ndicho kilichomgharimu Sulemani kuipata hiyo kanuni ya mwanadamu ya kuishi hapa duniani kwa wepesi na furaha na amani, kwa lugha ya kisayansi tunaweza kusema FORMULA ya maisha ya mwanadamu ambayo katika hiyo mwanadamu atakuwa na uwezo wa kufungua milango yote migumu ya maisha yake ya sasa na ya baadaye ambayo hapo kwanza kwa kuikosa hiyo ndio iliyomfanya mwanadamu awe mtu wa kutangatanga huko na kule, ajisumbue kwa hili na lile, ajitese kwa hichi na kile. Lakini sasa akishaifahamu hii kanuni basi maisha yake yatakuwa matamu yenye raha na mafanikio.

Na jawabu hili tunakuja kuliona mwishoni kabisa mwa kitabu alichokiandika SULEMANI cha Mhubiri..Sulemani anasema

Mhubiri 12: 13 “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, MAANA KWA JUMLA NDIYO IMPASAYO MTU.

14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni KILA KAZI, pamoja na KILA NENO LA SIRI, likiwa jema au likiwa baya”.

Unaona jumla mambo yote yampasayo mtu ni hii KUMCHA MUNGU, NA KUZISHIKA AMRI ZAKE.Basi!!..kwa hilo kila mlango utafunguka, ambao mwanadamu alikuwa anajitesa kwayo.

Sasa sisi tunaoishi kizazi hiki, tumesharahisishiwa mambo yote, leo hii unahangaika kutafuta mali ukidhani kuwa huko ndiko utapata jawabu la maisha yako, ndugu Sulemani alizitafuta sana tena kwa lengo la kupata jawabu kama hilo hilo unalolitafuta wewe, lakini hakuliona mwisho wa siku akasema ni UBATILI na UONGO..

Mhubiri 7: 27 “Tazama, asema Mhubiri, mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha hili na hili, ili kuitafuta jumla;

28 ambayo bado nafsi yangu nikali nikiitafuta, nisiione;….”

Leo hii unatafuta kuzitii tamaa zako za macho na anasa,kila mwanamke mzuri unataka awe wako, kila mwanaume mwenye utajiri unataka awe mume wako, ukidhani kuwa utapata raha nafsini mwako, na hivyo maisha yako yatakuwa mepesi ukidhani kuwa hiyo ndio maana ya maisha. dada/kaka Sulemani alishalijaribu hilo nalo kwa ajili yetu, ili aone kama kweli humo ndani yake kuna jambo la maana sana la kumfaa mwanadamu lakini alingundua ndani yake kuna ubatili na mauti, yeye alikuwa na mamia ya wake na Masuria lakini hata kimoja hakuona kama kinao uwezo wa kutoa jawabu la maisha ya mtu hapa duniani.

Unadhani siku ukishajenga nyumba na kuwa na familia nzuri ndio siku utakayofurahia maisha yako?. Na hivyo leo hii unazunguka huku na kule unajitabisha kwa hili na lile ili uifikie hiyo furaha?. Ndugu ni vizuri kufanya hivyo lakini fahamu kuwa hilo sio jawabu la maisha yako.

Unaona kuwa ulevi ndio furaha ya maisha ya mwanadamu, hilo nalo lilishajaribiwa lakini alisema halina manufaa yoyote ya kumwokoa mwanadamu. Embu sikiliza walau kidogo maneno haya ya Sulemani aliyosema:

Mhubiri MLANGO 2

“1 Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa ANASA. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.

2 Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?

3 Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili KWA MVINYO, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, HATA NIYAONE YALIYO MEMA YA KUWAFAA WANADAMU, ILI WAYAFANYE HAYO CHINI YA MBINGU SIKU ZOTE ZA MAISHA YAO.

4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;

5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;

6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.

7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;

8 TENA NIKAJIKUSANYIA FEDHA NA DHAHABU, NA TUNU ZA KIFALME NA ZA KUTOKA KATIKA MAJIMBO. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.

9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.

10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.

11 Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, YOTE NI UBATILI NA KUJILISHA UPEPO, WALA FAIDA HAKUNA CHINI YA JUA”.

Unaona hapo ndugu mimi na wewe hatupaswi kuyajaribu hayo yote ambayo tayari yalishajaribiwa na kuonekana kwamba hayawezi kutupatia sisi furaha na uzima wowote ndani yetu. Tuufuate ushauri wa wenye hekima, tuufuate ushauri wa mababa, tuufuate ushauri wa walitutanguliza zamani wazee wetu ambao kwa hekima za Mungu waliona na kufundishwa mengi Ndio maana Suleimani akaitwa akaitwa MUHUBIRI.. Usidanganyike na wahubiri wengine wanaokutumainisha katika mambo ya ulimwengu huu, Tumsikilize Muhubiri huyu aliyetiwa mafuta na Mungu mwenyewe na kuitwa MUHUBIRI,na ndio maana Sulemani alisisitiza sana katika mithali zake akisema..

Mithali 7: 1 “Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako.

2 Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako.

3 Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako”.

Mithali 4: 10 “Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.

11 Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.

12 Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa”.

Yesu pekee ndio jawabu la maisha yako, haijalishi utahangaika wapi, utasumbuka wapi, utajitaabisha na nini, leo ni rahisi kupuuzia lakini utafika wakati ambao utaona hivyo vitu ulivyovitaabikia havikukupa jawabu la maisha yako hapo ndipo utapozikumbuka zile hekima ulizopewa na mababa ukazikataa. Na kumbuka ukishafika huo wakati huwezi tena kuwa na raha, utajikuta tu unayachukia maisha yako. Kwasababu umeshachelewa, na wala huna nguvu tena ya kumshinda yule mwovu kwasababu siku za maisha yako zimeshakwenda..

Mwanadamu huwa akishafika hatua hiyo ni ngumu tena kumgeukia Mungu kwasababu anakuwa ameshachanganyikiwa rohoni hajui ni wapi tena pa kuanzia,ni wapi pa kumalizia, japo atajifanya kuwa anafuraha kwa nje lakini ndani yake huzuni na hofu vimemjaa kwasababu alipuuzia hekima za mababa angali akiwa kijana, hakumkumbuka muumba wake siku za ujana wake, hata hekima za kidunia zinasema Samaki mkunje angali mbichi..Akishakauka ukijaribu kufanya hivyo atavunjika kama kijiti badala ya kukunjika..ndivyo itakavyokuwa hali yake mtu yule anayeupuuzia wokovu sasa..

Sulemani anasema tena “1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.(Mhubiri 12:1)”.

Unaona hapo zipo siku ZILIZO MBAYA, kadhalika zipo siku ZISIZO NA RAHA ndani yake zitakuja huko mbeleni kwa kila mwanadamu ambaye hamkumbuki muumba wake katika siku za ujana wake.

Wewe ni kijana unayesoma hii habari, yatafakari yote ambayo yalimgharimu Sulemani kuyafanya wakati mwingine hata mambo yasiyompendeza Mungu ili kusudi kwamba tu avumbue jumla ya maisha yako, unende katika kanuni ya maisha iliyo sahihi..

Na sasa JUMLA hiyo ipo wazi mbele ya macho yetu, siku ile hutakuwa na udhuru tena, ukisema nilitanga tanga kutafuta raha na amani na ndio maana niliingia katika anasa na ushirikina, Sulemani atakuhukumu siku ile kwa kutokutii sauti ya Mungu inayozungumza na wewe kupitia injili yake.

TUBU sasa, mpe YESU KRISTO maisha yako, acha dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kutozifanya tena na sio kimazoea, kisha ukabatizwe katika ubatizo ulio sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi katika jina la YESU ili upate ondoleo la dhambi zako, kisha kuanzia hapo Bwana mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu kukusaidia kuushinda ulimwengu na kumcha Yeye kila siku. Na maisha yako yatakuwa SALAMA katika mikono yake yeye aliyekupa huo uzima, siku zako zilizobakia hapa duniani.

Ni maombi yangu utafanya hivyo leo.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

UMEFUNULIWA AKILI?

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

TUSIFUNGWE NIRA PAMOJA NA WASIOAMINI.

KWANINI TUWE WENYE BUSARA KAMA NYOKA?

DHAMBI YA ULIMWENGU


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/02/jawabu-la-maisha-ya-mtu/