MTAIFAHAMU KWELI NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU.

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01


Mtu anayevamiwa na nguvu za giza, kama hajaamua yeye mwenyewe kutaka kuwa huru na hizo roho, hata aombeweje hawezi kuwa huru na hizo roho, hakuna nguvu yoyote iliyokubwa ndani ya mwanadamu kama nguvu ya maamuzi, Hata Roho Mtakatifu mwenyewe hawezi kuyateka maamuzi ya mtu, ingawa anao huo uwezo, lakini hafanyi hivyo…si zaidi shetani? Mwanadamu akiamua kujifunga kwa maamuzi yake, amejifunga, hakuna sala yoyote wala dua yoyote, itakayoweza kumtoa kwa nguvu katika kile alichokiamua. Kwahiyo mtu yoyote ambaye hataki kumpokea Kristo, anakuwa chini ya nguvu za giza kwa maamuzi yake mwenyewe na hivyo hakuna chochote kitakachoweza kuyashinda maamuzi yake.

Sasa Bwana Mungu anachokifanya kwa Yule mtu asiyemwamini ni kumletea nguvu ya ushawishi, itakayomfanya abadilishe maamuzi yake na kumgeukia yeye, lakini sio kumletea nguvu ya kumpindua kwa nguvu kwa kile anachokiamini. Ndio hapo atamletea wahubiri, atazungumza naye moyoni kwa sauti ya faraja na matumaini n.k.Na Yule mtu akishashawishika vya kutosha kumwamini na kumgeukia Mungu, ndipo Roho ya Mungu inaingia ndani yake na kumgeuza kuwa mtu mwingine..Lakini kama Yule mtu hataki ataendelea kubaki vilevile..roho ya shetani iliyo ndani yake itaendelea kuwa na nguvu..Na haiwezi kutolewa kwa kuombewa wala kuwekewa mikono.

Kama maandiko yanavyosema “tena mtaifahamu kweli, NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU Yohana 8.32”.

Na biblia inatafsiri nini maana ya kweli katika kitabu cha

Yohana 17: 14 

“14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyowa ulimwengu.

15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.

16 Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.

17 Uwatakase kwa ile kweli; NENO LAKO NDIYO KWELI”

Kwahiyo tunaona NENO LA MUNGU ndiyo kweli, ikiwa na maana kuwa kwa kupitia Neno la Mungu mtu ndipo anaweza kuwekwa huru, kwa kupitia Neno la Mungu mtu ndio anaweza kufunguliwa na vifungo vya dhambi na shida na mauti, na sio kupitia kumwombea mtu ndio mtu aweze kufunguliwa na kuwekwa huru.

Ndio maana Bwana Yesu alikuja duniani, na Injili ya kumweka mtu huru, alisema “Tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia”, alisema “aniaminiye mimi anao uzima wa milele na nitamfufua siku za mwisho”…alisema “wapendeni adui zetu, waombeeni wale wanaowaudhi,”..alisema “tusamehe wale waliotukosea ili na Baba yetu wa mbinguni atusamehe sisi makosa yetu”. Hayo ndiyo maneno ya kutuweka sisi huru.

Hebu fikiri leo hii mtu kamkosea Mungu labda kaua, au kaiba, au kafanya mabaya mengi,na anakwenda kuomba au kuombewa kanisani kwamba Mungu amsamehe makosa yake, na kupewa matumaini kwamba dhambi zake zimeondolewa na huku analo kundi la watu wengi kichwani mwake ambao hajawasamehe ambao walimwibia naye pia au walimwulia ndugu yake au walimfanyia ubaya fulani? Je! Huyo mtu kasamehewa dhambi zake kweli?, huyo mtu ni kweli kawekwa huru?… Ni wazi kuwa huyo mtu bado kafungwa na yupo chini ya laana na ghadhabu ya Mungu, kwasababu Neno linasema “Msipowasamehe watu makosa yao na Baba yetu wa mbinguni hatatusamehe sisi makosa yetu”..Kwahiyo hakuna maombi yoyote yanayoweza kumfanya huyo mtu asamehewe makosa yake na Mungu, hata afunge miezi na miaka, hata aombewe na kasisi mkuu wa dunia. Hakuna dawa ya makosa yake…Dawa ni moja tu! Kulifahamu NENO LA MUNGU, ambalo ndilo kweli ya Mungu itakayomweka huru…na neno hilo linasema “samehe kwanza watu waliokukosea ndipo na Bwana atakapokusamehe makosa yako”..Hilo Neno ndilo litakalomweka Huru mbali na dhambi, hakuna njia ya mkato au mbadala.                     (MTAIFAHAMU KWELI NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU).

Hiyo ndiyo sababu Bwana alipopaa duniani aliturithisha NENO LAKE(Biblia Takatifu) badala ya sura yake, sura yake haikuwa na umuhimu sana kwetu kuliko maneno yake. Hakuturithisha  mali, wala chochote kile bali aliturithisha Neno lake, kwasababu kwa kupitia hilo ndio litakalotuweka huru.

Kwahiyo kaka/Dada unayesoma ujumbe huu, tafuta sana kuisoma Biblia, kwa nia ya kujifunza…usipendelee sana kusubiria kufundishwa kanisani au kwenye mikutano, soma mwenyewe biblia, sura baada ya sura, habari baada ya habari na Roho Mtakatifu atakusaidia na kukuongozakatika kweli yote, kwasababu hiyo ndiyo kazi yake…Huko ndiko utakapofunguliwa vifungo vya giza na kuwekwa huru siku baada ya siku. Roho Mtakatifu sio kwa baadhi ya watu tu! Hapana biblia inasema ni kwa watu wote waliomjia yeye…

“Matendo 2:38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Vinginevyo usipoijua Biblia, utapelekwa na kila aina ya upepo, utakuwa na hofu na mashaka, utatanga tanga huku na kule, leo utaambiwa usile chakula hichi ni cha wachawi, kesho utaambiwa kata mti Fulani nyumbani kwako ni wa kichawi, baadaye utaambiwa kuota unasoma, upo darasani basi nyota yako imechukuliwa ipo sehemu fulani, baada ya siku chache tena utaambiwa jina lako liko kwa wachawi, kesho kutwa utaingizwa kwenye maombi ya kutengeneza nyota, na kusambaratisha maadui zako,.utafundishwa kila aina ya elimu, na nyingi ya hizo ni elimu za kuzimu, ambazo biblia inaziita MAFUNDISHO YA MASHETANI!! Ambayo dhumuni kubwa ya mafundisho hayo ni kuwatia watu hofu, na kuwatoa katika mstari wa kujifunza Neno la Mungu na kuanza kujifunza elimu za ufalme wa giza (Ni agenda kamili kutoka kuzimu). Ili watu wakimbilie kuombewa na WASILIJUE NENO LA MUNGU, ambalo ndilo hilo tumeambiwa LITATUWEKA HURU!.

Kwahiyo ndugu, jifunze Biblia kwa bidii zote,tenga kila siku muda wa kusoma maandiko mwenyewe, usisubiri mtu akutolee kipengele Fulani cha maandiko na kukutafsiria na kukutengenezea somo, asipokuwa na mrejeo mwingine wa habari inayofanana na huo mstari.

Epuka sana injili za Mafanikio, unachukuliwa mstari mmoja unatengenezewa somo refu, kusapoti kupata mali/ utajiri, kila mstari unaofundishwa ni kurejeshwa wewe  kwenye mali, na kesho tena utahubiriwa mali, na kesho kutwa tena hivyo hivyo, (zichunguze hizo roho), utakuta zinagusia kidogo sana, au hazigusii kabisa habari za Msalaba,toba,wala utakatifu ambao Biblia imesema hakuna mtu atayemwona Mungu asipokuwa nao (Waebrania 12:14).

Injili ambazo zinakuambia utapokea utajiri/mali ndani ya muda mfupi..Hizo ni injili za Yule Mjaribu; LUSIFA za kumfanya umsujudie yeye. Ambaye alimjaribu Bwana kwa kumwonyesha Milki zote za dunia ndani ya DAKIKA MOJA, na kumwambia Ageuze Jiwe liwe Mkate ndani ya dakika moja. Na kumtumainisha kwamba akijitupa chini ya mnara malaika watatumwa waje kumwokoa, Na shetani anatumia maandiko kuwaonyesha watu milki za dunia ndani ya dakika moja, anatumia maandiko kuwaambia watu wanaweza kugeuza sadaka zao kuwa utajiri dakika hiyohiyo, huku wanapandikiziwa chuki dhidi ya ndugu zao, na kufundishwa kila mtu ni adui yao.

Kama ulishawahi kuingia huko, jiokoe nafsi yako ndugu toka haraka sana, hebu jiulize ni lini kati ya hizo siku ulizoingizwa kwenye hizo injili za mafanikio, baada ya kutoka na kurudi nyumbani ULISIKIA HAMU YA KWENDA KUJITAKASA ZAIDI MBELE ZA MUNGU NA HAMU YA KWENDA KUSOMA NENO?? Kama ulishawahi kusikia hiyo hamu basi baki hapo, maana Mungu yupo, lakini kama hujawahi kusikia hiyo hamu ya kujisogeza zaidi mbele za Mungu badala yake unasikia hamu ya kwenda kumkomoa adui yake, na kutaka ajionee unavyobarikiwa…Hilo ni jaribu ndugu!! Ondoka kabisa! Jiokoe nafsi yako na wala usigeuke nyuma!!. Bwana alizikataa zile mali shetani alizokuwa anataka kumpa ndani ya dakika moja, kwasababu aliona utajiri usioelezeka unaokuja huko mbele.. Na biblia inasema katika Mithali 13: 11 “ Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”

Bwana akujalie kuyaona hayo mtu wa Mungu, Kama hujampa Bwana Yesu Maisha yako, huu ndio wakati wa kufanya hivyo kwasababu huijui kesho, mgeukie leo, utubu dhambi zako zote kwasababu yeye ni mwaminifu atakusamehe sawasawa na Neno lake, na pia Hakikisha utakwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38 ili upate ondoleo la dhambi zako, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukutia katika kweli yote ya Biblia.

(MTAIFAHAMU KWELI NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU).

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MANABII WALISEMA “NENO LA MUNGU LIKANIJIA” ..MAANA YA HILI NENO NI NINI?

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/mtaifahamu-kweli-nayo-hiyo-kweli-itawaweka-huru/