SIKUKUU YA VIBANDA.

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01

Moja ya sikuku saba ambazo Mungu aliwaagiza Wana wa Israeli wazishike ni SIKUKUU YA VIBANDA..Nyingne sita ni 1) Sikuku ya Pasaka,

2) Sikukuu ya Mikate isiyotiwa chachu,

3) Sikukuu ya Malimbuko ya Mavuno,

4) Sikukuu ya Majuma au Pentekoste

5) Sikukuu za kupiga Baragumu

6) Sikukuu ya siku ya Upatanisho na

7) Sikukuu ya Vibanda ndiyo ya Mwisho na ya saba.

Kila sikukuu ilikuwa na umuhimu wake na maana yake kubwa kimaandiko, Kwahiyo wana wa Israeli waliambiwa wazishike sikukuu hizi kwa faida zao wenyewe.Kumbuka sikukuu hizi hazikuwa kwa ajili ya kunywa na kula kama zinavyofanyika leo..Sikukuu hizi zilikuwa ni kwaajili ya kufanya sala na ibada tu! Na kukumbuka Mambo makuu ambayo Mungu aliwatendea walipotoka Misri na walipokuwa jangwani..na Mungu alionya siku hizo zifanywe kuwa takatifu daima.

Leo tutaitazama hii sikukuu ya mwisho inayojulikana kama sikukuu ya Vibanda na umuhimu wake kwa Wana wa Israeli na umuhimu wake kwetu sisi watu wa agano jipya.

Zamani wakati Mungu anawatoa Wana wa Israeli katika nchi ya utumwa Misri, aliwapitisha njia ya JANGWA ndefu ili kuwafundisha huko, kumbuka sio kwamba hapakuwa na njia ya mkato wa kufika nchi ya Ahadi, hapana ilikuwepo tena nzuri tu lakini Bwana aliamua kuwapitisha njia ya jangwa, iliyo ngumu, ili kuwanyeyekeza mioyo yao na kuwafundisha wamtegemee yeye kwa kila kitu, wamfahamu yeye kuwa sio Mungu tu wa mahali penye kijani bali pia ni Mungu wa jangwani, na kwamba mtu hataishi tu kwa vilimo, na katika milima mizuri yenye chemchemi, au katika fukwe nzuri zenye maji baridi, au katika nchi laini yenye udongo mzuri bali anaweza akaishi pia katika jangwa lisilokuwa na chakula, wala msimu wa mvua, wala maji wala upepo mwanana na bado akawa na afya nzuri, akawa na raha, na asichakae, asiugue endapo tu atatembea na Mungu..hilo ndilo somo Bwana alilokuwa anataka watoto wake wafahamu wakiwa kule jangwani.

Kumbukumbu 8: 1 “Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.

2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili

akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.

3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua;

APATE KUKUJULISHA YA KUWA MWANADAMU HAISHI KWA MKATE TU, BALI HUISHI KWA KILA LITOKALO KATIKA KINYWA CHA BWANA.

4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini.

5 Nawe fikiri moyoni mwakoya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako akurudivyo.

6 Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha”.

Sasa kule jangwani kama tunavyojua Jangwani hakuna misitu, wala makazi wala wafanya biashara wala chochote kile..walikuwa ni wao kama wao tu! hakukuwa na nyumba za kukaa hivyo suluhisho pekee la kutatua changamoto hiyo ilikuwa ni kwenda kutengeneza vibanda vidogo vidogo vitakavyowahifadhi wakiwa kule jangwani..vibanda hivyo walivitengeneza kiasi cha kwamba havikuwa vya kudumu..bali vya muda mfupi tu, kwasababu wao walikuwa ni watu wa kusafiri, leo wapo hapa kesho wapo kule..kwahiyo waliishi ndani ya hivyo vibanda kwa miaka 40, Na walipofika nchi ya Ahadi Bwana aliwaahidia hawatakaa tena katika vibanda kama walivyokuwa jangwani, wala hawatakula tena chakula cha aina moja (mana)..bali watakula vyakula vingi vya aina nyingi tofauti tofauti kwasababu hiyo nchi itawazalia yenyewe pindi watakapofika na pia watakaa kwenye majumba makubwa ambayo hata hawajayajenga wao, kadhalika mataifa yote yatawaogopa nao watakuwa watu wakufanikiwa sana.

Lakini kwasababu Bwana anaijua mioyo yao mbeleni, alijua watakapokula na kushiba watamsahau yeye, wataacha kuyashika maagizo yake, na kumsahau Mungu ambaye aliwapigania katika hali ngumu za jangwani, na kumsahau Mungu wao kuwa ndiye Mungu pekee aliyewasaidia wakati wa matatizo..Hivyo Bwana Mungu kwa kulifahamu hilo, aliwaagiza watakapoingia hiyo nchi ya ahadi kila mwaka wafanye sikukuu ya siku saba kuadhimisha jinsi Mungu alivyotembea nao jangwani.

Aliwaagiza kila mwisho wa Mwaka wa saba wa kalenda ya kiyahudi, watu wote watoke katika nyumba zao za kifahari wanazokaa…waende milimani wakachukua fito na matawi ya miti kila mtu akajenge kibanda kidogo pembezoni mwa nyumba yake kama vile walivyotengeneza walipokuwa kule jangwani..kila mtu au familia akalale ndani ya hicho kibanda ndani ya siku saba..wakumbuke Uweza wa Mungu na matendo yake aliyowatendea jangwani miaka 40, kwamba walikaa ndani ya vibanda na walikuwa wanalishwa na kunyweshwa ndani ya lile jangwa nene kimiujiza, na wala walikuwa hawaugui wala mavazi yao kuchakaa.

Kwahiyo sheria hiyo Mungu aliiagiza ifanyike kwa vizazi vyote..Kwamba kila mwaka mwezi wa saba ni lazima ishikwe..kumbuka haikuwa sherehe ya kula na kunywa, wala watu walikuwa hawaendi kwenye kumbi za starehe kusheherekea..ilikuwa ni sherehe ya kumwimbia Mungu,kumsifu na kukaa katika vyumba vya ndani katika uwepo wake na kutafakari kwa muda mrefu matendo yake makuu. Ulikuwa ni wakati wa kuisoma torati yote upya na kujikumbusha mambo yaliyoandikwa kule, na pia ulikuwa ni wakati wa kuwafundisha watoto wale waliozaliwa hivi karibuni sheria za Bwana na torati. Hiyo ndiyo tafsiri ya sikukuu mbele za Mungu. Tunasoma:

Kumbukumbu 31: 10 “Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, WAKATI ULIOAMRIWA WA SIKUKUU YA VIBANDA,

11 Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao.

12 Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii;

13 na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki”.

Nehemia 8: 14 “Wakaona ya kuwa imeandikwa katika torati, jinsi Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, ya kwamba wana wa Israeli WAKAE KATIKA VIBANDA, katika sikukuu ya mwezi wa saba;

15 na ya kwamba wahubiri na kutangaza katika miji yao yote, na katika Yerusalemu, kusema, Enendeni mlimani, mkalete matawi ya mzeituni, na matawi ya mzeituni-mwitu, na matawi ya mihadasi, na matawi ya mitende, na matawi ya miti minene, ili kufanya vibanda, kama ilivyoandikwa.

16 Basi watu wote wakatoka, wakayaleta, wakajifanyizia vibanda, kila mtu juu ya dari ya nyumba yake, na katika nyua zao, na katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja wa lango la maji, na katika uwanja wa lango la Efraimu.

17 Na mkutano wote wa watu, waliorudi kutoka nchi ya uhamisho wao, wakafanyiza vibanda, wakakaa katika vibanda hivyo; maana tokea siku za Yoshua, mwana wa Nuni, hata siku ile, wana wa Israeli hawakufanya hivyo. Pakawa na furaha kubwa sana.

18 Tena siku baada ya siku, tangu siku ya kwanza hata siku ya mwisho, akasoma katika kitabu cha torati ya Mungu. Wakafanya sikukuu muda wa siku saba; na siku ya nane palikuwa na kusanyiko la makini, kama ilivyoagizwa”.

Sasa mambo haya ni kivuli cha mambo yaliyopo sasahivi, kwasababu agano la kale ni kivuli cha agano jipya, mambo yaliyokuwa yanafanyika agano la kale kwa namna ya mwilini yanafanyika leo katika agano jipya kwa namna ya roho. Kama Bwana alivyowatoa wana wa Israeli kutoka nchi ya utumwa Misri, na sisi pia Bwana ametutoa katika nchi ya utumwa wa dhambi, na kama vile wana wa Israeli walivyobatizwa wote katika Bahari ya Shamu (1 Wakoritho 10:2) na kuwa huru na majeshi ya kimisri kikabisa kabisa na sisi pia kupitia ubatizo wa maji mengi kwa jina la Yesu tunawekwa huru mbali na dhambi kikabisa kabisa.

Na kama wana wa Israeli walivyofundishwa katika jangwa zito, na sisi pia Bwana ametupitisha katika majaribu mbali mbali kuijaribu imani yetu, na kama tutakuwa waaminifu Basi Bwana atatuingiza katika kaanani yake ya rohoni ambayo ni mbingu mpya na nchi mpya..Lakini kabla hajatuingiza katika hiyo Kaanani ya milele mahali pasipo kuwa na tabu wala shida..atatuingiza pia katika Kaanani ya miili yetu hii. Atatupa mara mia katika ulimwengu huu kama alivyoahidi katika Neno lake.

Na atakapokuingiza katika hiyo nchi, Ni wajibu wako kumfanyia Mungu sikukuu ndani ya moyo wako..Tenga siku, au wiki, au mwezi..funga yatafakari mambo yote makuu Mungu aliyokutendea wakati upo katika madarasa ya Mungu, Kipindi hauna chochote lakini Bwana anakupigania..kipindi unaumwa na huna msaada lakini Bwana anakuponya..kipindi ambacho ungestahili kufa kwenye lile jangwa la mateso lakini hukufa, kipindi ambacho ulipitia kila aina ya jaribu lakini Bwana hakukuacha..Zikumbuke hizo siku usizisahau, ibada ya kumbukumbu ya hizo siku ndiyo SIKUKUU INAYOMPENDEZA MUNGU.

Inayofananishwa na SIKU KUU YA VIBANDA, Unapozitafakari hizo siku, inakusaidia kutozisahau fadhili za Mungu alizokutendea nyuma, na hivyo siku zote unajikuta unaishi katika mstari wa Mungu…Kama wana wa Israeli ilikuwa ni amri kuishika sikukuu ya Bwana na sisi pia ni amri kukumbuka fadhili za Mungu na kuzitafakari siku zote za maisha yetu.

Kumbuka mema yote Mungu aliyokufanyia nyuma kwa kumfanyia ibada ya shukrani naye Mungu atakuangazia rehema zake daima.

Bwana akubariki sana, tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

SIKU KUU YA PURIMU

PENTEKOSTE NI NINI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/sikukuu-ya-vibanda/