UPONYAJI WA YESU.

by Admin | 20 March 2019 08:46 pm03

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, libarikiwe.

Karibu tujifunze Neno la Mungu, na leo tutajikumbusha kazi mojawapo ya Yesu Kristo iliyomleta Duniani…Tukiachilia mbali kazi ya UKOMBOZI na KUTUONYESHA NJIA YA KUMWELEKEA BABA..kazi nyingine iliyomleta Bwana duniani ni UPONYAJI. Na uponyaji upo wa rohoni na mwilini. Leo kwa ufupi tutajifunza juu ya uponyaji wa mwili.

Yesu Kristo sio daktari, ingawa tukimwita ni daktari mkuu tutakuwa hatujakosea sana..lakini yeye ni zaidi ya hapo…yeye ni mwumbaji..daktari atamtibu mtu, lakini litabaki kovu (hana uwezo wa kukirudisha kitu kama kilivyokuwa katika uhalisia wake)..Lakini Mungu ni zaidi ya hapo hatibu bali anaponya..

Katika huduma yake, Tangazo lake la kwanza alilowatangazia wayahudi ni hili.

Luka 4: 18 “ROHO WA BWANA YU JUU YANGU, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,

19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.

20 Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.

21 AKAANZA KUWAAMBIA, LEO MAANDIKO HAYA YAMETIMIA MASIKIONI MWENU”.

Huyo ni Bwana Yesu aliyezungumza maneno hayo baada ya miaka mingi wana wa Israeli kusubiria tumaini kutoka kwa Mungu, na sasa tumaini hilo limewafikia, Na tunaona ni Bwana pekee ndiye aliyeanza kufanya miujiza isiyo ya kawaida ambayo haikuwahi kutokea katika historia ya mwanadamu kwa vizazi vyote. Vipofu walikuwa wanaona, viwete wanatembea..na wenye magonjwa ya kila namna yalikuwa yanaponywa.

Ndugu nataka nikuambie Kristo Yesu mpaka leo anaishi, na kazi alizozifanya wakati akiwa hapa duniani bado anazifanya hata leo, kwa kupitia watu wake. Na yeye sio mwongo kama sisi wanadamu. Maneno yake ni ya ukweli wote. Tumeshuhudia mara nyingi kwa macho yetu watu wakiponya papo kwa hapo. Na mimi mwenyewe alishawahi kuniponya papo kwa hapo na sio mara moja.

Nimewahi kusikia shuhuda kadha za watu kuponywa magonjwa ambayo yamewatesa muda mrefu na wamekosa suluhisho kila walikokwenda, nimewahi kuwaombea watu kadhaa na Bwana akawaponya magonjwa ambayo yamewatesa kwa miaka mingi, na nimewahi kusikia shuhuda kadha za watu ambao Mungu kawaponya watu pasipo hata kuombewa. Hayo yote ni kuthibitisha kuwa Yesu Kristo si mwongo.

Sasa ni muhimu kufahamu ni jinsi gani uponyaji wa kimungu unashuka juu ya mtu. Wengi wetu tunadhani Mungu anatuponya au anatupa afya kwa utakatifu wetu tulionao….hiyo kwa sehemu Fulani ina ukweli kwa baadhi ya watu…kwasababu kama mtu anaisikia injili kwa miaka na miaka na hataki kubadilika, na anakuwa ni mtu wa kusitasita, leo anakwenda mbele, kesho anarudi nyuma, leo anakwenda kanisani kesho ni mwasherati, mtu wa namna hiyo ulinzi wa kimungu umeondoka juu yake, hivyo inakuwa ni rahisi kwake kuvamiwa na roho za uharibifu, ndio unakuta zitakazomsababishia magonjwa ya ajabu na hata wakati mwingine mauti.

Lakini kama mtu ni mwaminifu kwa Mungu au hakuwahi kuisikia kabisa INJILI au yupo katika hatua za awali za kumpa Yesu maisha yake halafu baadhi ya mambo yamemtokea, kama vile magonjwa pengine yasiyojulikana hata chanzo chake ni nini, na akaenda kutafuta uponyaji kutoka kwa Mungu kwa moyo wa kumgeukia yeye..Nataka nikuambie Ipo dawa!!, YESU NDIYE DAWA!!. Biblia inasema Yesu ni yeye Yule jana, leo na hata milele ikimaanisha kuwa anao uwezo wa kukirudisha kitu kiwe kama kilivyokuwa jana, na anao uwezo wa kukileta kitu leo kiwe kama kitakavyokuwa miaka 100 mbele au milele ijayo..Kwahiyo yeye hana muda wala hajachelewa…wanadamu sisi ndio tunao usemi unaosema “basi tena haiwezekani” lakini Yesu sio hivyo yeye hana muda, anaponya sasahivi na anarudisha kitu kama kilivyokuwa jana.. aliirudisha ngozi ya Naamani iliyokuwa na ukoma ikawa kama ngozi ya mtoto mchanga….

2 Wafalme 5: 13 “Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?

14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; NAYO NYAMA YA MWILI WAKE IKARUDI IKAWA KAMA NYAMA YA MWILI WA MTOTO MCHANGA, AKAWA SAFI.

15 Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake;”

Sasa kama wewe ni mgonjwa na huo ugonjwa umekutesa sana kwa muda mrefu, labda ni UKIMWI, au CANCER, au KISUKARI au ugonjwa wowote ule na unakuogopesha na hujui huo ugonjwa sababu yake ni nini, unachotakiwa kufanya sasahivi, ni kutulia, usiogope wala usikuogopeshe wala usipanic, tenga dakika chache mahali ulipo, tubu dhambi zako na maovu yako, na umwahidi Bwana endapo akikuponya huo ugonjwa utamfanyia nini…

Baada ya kutubu na kumwahidi…nataka utafakari mfano huu kisha uutumie huo kupokea uponyaji wako sasahivi. Hebu tafakari siku ulipojikata na kisu na baada ya muda Fulani kile kidonda kikapona..je! ulitumia utakatifu gani hapo kufanya ngozi yako ijirudie kama ilivyokuwa kwanza?…au siku upele ulipokuota kwenye ngozi yako na kesho asubuhi ukaukuta umepotea ulitumia utakatifu gani kuufanya upotee…hebu tafakari siku ulipojisikia kichwa kinauma na baada ya muda kikaisha chenyewe labda baada ya kulala na kuamka asubuhi, ulitumia utakatifu gani kukiponya? Kama hukutumia utakatifu wowote kijiponya kadhalika na ugonjwa ulio nao sasahivi hauhitaji utakatifu wowote…Siku ile ni Mungu alikiponya kichwa chako bure kwa Neema yake pasipo hata wewe kujijua, ukadhani ni mwili wako umejiponya mwenyewe, kumbe hujui ni Mungu ndiye aliyekuponya. na kila siku anauponya mwili wako pasipo hata wewe kujijua wala kumwomba, anakuponya kwa neema zake tu! Bureee…ngozi ya mguu wako kila siku inachubuka lakini kila siku Bwana anakutengenezea ngozi mpya ndio maana kiatu chako kinachakaa na unakibadilisha viatu kila siku lakini mguu wako hauchakai na wala haubadilishi, ndio maana nguo zako zinachakaa lakini mwili wako uko vile vile siku zote. Huo ni uponyaji wa kiMungu unaoendelea mwilini mwako pasipo matendo ya sheria.

Hivyo kwa kanuni hiyo hiyo ya kuponywa pasipo matendo, basi itumie hiyo hiyo kwa ugonjwa ulionao hapo ulipo, kama una HIV, au KISUKARI, au KANSA, au UTASA au Vidonda vya tumbo, au tatizo la figo, au ini, au moyo, au ni kiziwi, au kipofu, au ni kiwete, au tatizo lolote lile katika mwili wako. Kinachohitajika kwako ni IMANI tu!!..Usianze kujishaurishauri wala kuwa na mashaka mashaka, yakatae hayo mashaka, hata kama wakati mwingine bado unaona kuna udhaifu mwilini, hapo ulipo simama juu sema nimeshapona kwa jina la YESU. Kifo kimeshaingia kwenye huo ugonjwa..haupo tena huo ugonjwa, hata kama bado unahisi maumivu yasikuogopeshe tayari kifo kimeshaingia kwenye huo ugonjwa..unaukumbuka ule mtini Bwana Yesu alioulaani?…haukunyauka palepale lakini tayari ulikuwa umeshakufa ndani kwa ndani, hauna uzima tena, mizizi ilikuwa imeshaoza, baada ya masaa kadhaa wanafunzi wanafunzi walipouona umenyauka ndipo wakaelewa kuwa kumbe mti ulikuwa umeshakufa tangu jana Bwana alipoulaani, na sio leo, na ndivyo itakavyokuwa leo kwako na huo ugonjwa ulio ndani yako, usiangalie hali uliyo nayo hapo, amini kwamba tayari kiini cha ugonjwa hakipo…

Sasa kwa ajili ya kuwathibitishia wengine uponyaji wako..Nenda sehemu ambayo unafanyaga check/up ukifika waambie nimekuja kuchukua cheti ya uzima wangu, waambie wakupime na wakupe majibu ili ukatangaze matendo makuu ya Mungu, na watakupa majibu ambayo wao wenyewe watashangaa, yachukue hayo nenda mtaani kwako waonyeshe watu wengine kuwa YESU KRISTO SIO MZIMU YUPO HAI na anatenda kazi zake hadharani.

Nakuombea kwa Mungu, imani yako isitetereke, mwamini Bwana Yesu, fanya kama nilivyokwambia na wewe mwenyewe utashuhudia kwa macho yako matendo makuu ya Mungu. Alifanya kwa wengine, alifanya kwangu, atafanya na kwako, na atafanya kwa wengine kwa kupita ushuhuda wako wewe.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

YESU MPONYAJI WA KWELI.

TUNAYE MWOMBEZI.

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/03/20/uponyaji-wa-yesu/