ZIFAHAMU KAZI KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

by Admin | 13 May 2019 08:46 am05

Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu…”

Hakika tukilifahamu Neno la Mungu kama mtu mmoja alivyosema, hata tukifungiwa katika chumba chenye giza tukapewa mshumaa na Biblia tu tutaweza kukuleza mambo yote yanayoendelea na kazi zote za shetani azifanyazo duniani bila hata kuhadithiwa na mtu yeyote,..Kumbe hatuhitaji shuhuda kutoka kuzimu ili kutusaidia sisi kufahamu utendaji kazi wa shetani, Biblia imeweka wazi mambo yote, na leo hii tutaziona hizo kazi kubwa shetani anazojishughulisha nazo kwa msaada wa Neno la Mungu:

1) KUSHITAKI WATAKATIFU:

Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni,ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, YEYE AWASHITAKIYE mbele za Mungu wetu, mchana na usiku..

11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Leo umekuwa mtakatifu kwa kumwamini mwana wa Mungu, lakini fahamu kuwa shetani bado hajakata tamaa ya kukufutilia, nyendo zako, na akipata kosa tu kazi yake ni kulipeleka mbele za Mungu ili uhukumiwe, anapeleka mashtaka usiku na mchana, lakini ashukuruwe Mungu sisi tulio ndani ya Kristo, pale anapokwenda kutushitaki, hapo hapo ameketi mwombezi wetu Yesu Kristo, kututetea sisi. Hivyo ni jukumu letu  kuziweka njia zetu katika mstari ulioonyooka ili adui akose la kutushitaki.

2) KUZUIA KAZI YA MUNGU: 1Wathesalonike 2.18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia”.

Ni jambo la kawaida kukutana na shetani uso kwa uso unapojaribu kuieneza kazi ya Mungu, Hiyo ni moja ya huduma yake duniani, Paulo alizuiwa na jeshi la mapepo alipokuwa akienda kuhubiri Injili Thesalonike,.Hata sasa mambo hayo hayo anayafanya,.Hivyo nawe pia ukiwa umevaa zile silaha zote zinazozungumziwa katika Waefeso 6, usiogope, kusimama, kwasababu aliyesimama upande wetu ni mkuu kuliko aliyeupande wao..Utakutana na visa na mawimbi ya ajabu njiani lakini usiogope..Aliyekutuma atakuwa pembeni yako.

3) KULETA MAJARIBU: Hii pia ni kazi anayoifanya shetani kwa maaminio kila siku, ili kuwadondosha , na kuwafanya wauone ukristo kuwa ni mgumu na mwisho wa siku wakate tamaa, na waiache njia ya wokovu,Tunaona yalitokea kwa Ayubu, Yalitokea kwa Bwana wetu Yesu Kristo, yalitokea kwa mitume, na yatatokea na kwetu,

Waebrania 11: 36 “wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;”

Lakini ashukuriwe Mungu, ambaye anatupa nguvu ya kuyashinda,.kwasababu biblia inaweka wazi kabisa mtu yeyote atakayeingia katika PENDO la Kristo, hakuna kitu chochote kitakachoweza kumtenganisha nalo.

Lakini kumbuka pia mtu yeyote aliye nje ya Kristo hajaribiwi, wala asijidanganye kusema anapitia majaribu, atajaribiwa na nini wakati yupo tayari kwenye dhambi?.kinyume chake yeye ndiye anafanyika chombo cha shetani kuwajaribu watu wa Mungu..

4) KULETA MAGONJWA: Luka 13:16 “Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?”

Huyu ni mwanamke aliyefunguliwa na Bwana Yesu ambapo Pepo la udhaifu lilimsababishia ulemavu wa kudumu wa mgongo (yaani kibiongo). Hii ni kutuonyesha kuwa sababu ya magonjwa mengi yanayowapata watu leo hii ni kazi ya shetani. Yeye ndiye anayehusika na magonjwa na matatizo yote, Lakini tumaini lipo na tiba na kinga vile vile ipo kwa yeyote amwaminiye Kristo leo, kwasababu maandiko yanasema (Isaya 53: 4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu;..Na kwa kupigwa kwake sisi tulipona)..HALELUYA!!

5) KUUA:

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; ..”

Hii ni kazi nyingine kubwa ya shetani kuangamiza kotekote yaani mwilini na rohoni. Ndugu fahamu kuwa shetani hakupendi hata kidogo, ni Rehema za Mungu tu zinatushikilia wewe na mimi, zinakushikilia wewe ambaye bado upo kwenye dhambi, ungeshakufa siku nyingi biblia inasema shetani asili yake ni uuaji tangu mwanzo alikuwa hivyo, na ndio chanzo cha mauaji unayoyaona yanaendelea sasahivi duniani, na atakuja kutekeleza vizuri katika kipindi cha ile dhiki kuu, lakini yeye aliye ndani ya Kristo, amefichwa ndani ya ule mwamba imara wala mwovu hawezi kumgusa, na hata akimgusa basi ni kwa ajili ya kutimiza kusudi la Mungu kama Ayubu, na sio kuuliwa ovyo ovyo kama tu kuku.

6) KUDANGANYA:

Yohana 8:44“…..wala hakusimama katika kweli [shetani], kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”.

Unaona?. Kazi ya upotoshaji ni kazi inayomletea shetani matunda makubwa sana, Anachofanya yeye, hakuzuii kumwabudu Mungu wala kwenda kanisani, bali anakuhubiria njia zake za uongo, ili umwabudu yeye pasipo wewe kujua ukidhani unamwabudu Mungu, au anakushawishi ufanye kitu Fulani ukidhani ni chema kumbe unamkosea Mungu, na mwisho wa siku unakufa unajikuta upo kuzimu, mpango wake umekamilika juu yako. Na ndio maana tumeonywa kila siku tuijue kweli ili tuwe huru, na KWELI ni NENO LA MAUNGU, katika zama tulizopo udanganyifu wa ibilisi umezidi kuongezeka, tuombe Mungu atusaidie, huku na sisi wenyewe tukionyesha bidii kumtafuta Mungu.

7) KUPOFUSHA:

2Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;

4 ambao ndani yao MUNGU WA DUNIA HII AMEPOFUSHA FIKIRA ZAO WASIOAMINI, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.

Leo hii unaweza ukajiuliza ni kwanini watu wengi wanasikia injili, wanaziona kazi za Mungu waziwazi akifanya ishara na miujiza, wanajua kabisa Mungu yupo lakini bado hawataki kubadilika,..ni kwasababu wametaka wenyewe kuwa chini ya shetani, hivyo na shetani naye akatumia fursa hiyo kuwapofusha fikira zao moja kwa moja wasiiamini Injili wakapona.. Na anafanya hayo akishirikiana na wakuu wake wa giza hili pamoja na mapepo yote,.Hivyo ndugu ikiwa wewe ni mmojawapo wa watu wasiosikia injili, jichunguze tena, na uamue kubadilika, Mgeukie Bwana akupake dawa kwenye macho yako upate kuona.

Bwana anasema katika

Ufunuo 3:17-20 “…Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, NA KIPOFU, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.”

8) KUNYAKUA NENO LA MUNGU:

Mathayo 13:18 “Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.

19 Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.”

Hapa napo shetani amewekeza sana, na amefanikiwa pakubwa..Akishaona mtu Fulani anaonyesha uelekeo wa kutaka kuamini, alipohubiriwa injili, ilipomchoma, sasa yeye anachohakikisha ni kuwa anapambana kwa kila namna kuliondoa lile Neno ndani ya mtu yule, ndio hapo utakuta mtu anakosa Muda wa kutafari lile Neno alilofundishwa, badala yake shetani atamletea vitu mbadala vya kujishuhulisha navyo, kama vile movies, mpira, michezo, tv, kuchati, mihangaiko, miziki n.k..mwisho wa siku anasahau kile alichopandiwa ndani yake, na baadaye anarudia hali yake ya mwanzo na kuwa kama vile mtu ambaye hajawahi kusikia Neno la Mungu kabisa..

Hiyo ni njama kubwa sana shetani anayoitumia kuiondoa mbegu iliyopandwa ndani ya mtu, hata katika mambo ya dunia, mwanafunzi akitaka kuondoa kitu alichokipata darasani, aanze tu kungalia movie muda mrefu, au kuchat au kusikiliza miziki…mwanafunzi wa namna hiyo ndani ya muda mfupi sana, utakuta kashazika kila kitu katika akili yake kuhusu kitu alichojifunza muda mfupi au siku chache nyuma..Na shetani ndio anatumia vitu hivyo hivyo kuiba mbegu iliyopandwa ndani ya mtu.

Embu jiulize injili imehubiriwa kwako mara ngapi, na bado upo vilevile, Neno la Mungu lilivyo na nguvu ilipaswa usikie mara moja tu na kugeuka moja kwa moja, lakini kwasababu shetani umempa nafasi basi amekuwa akiifanya hii kazi ndani yako kila siku pasipo hata wewe kujijua, Hivyo chukua hatua ubadilike mara kwa kuitii Injili inapohubiriwa kwako weka mbali miziki ya kidunia, filamu, tamthilia, novels zisizokuwa na maana na mambo mengine yote yanayofanana na hayo.

9) KUJIGEUZA NA KUWA MFANO WA MALAIKA WA NURU:

2Wakorintho11:13 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.

14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

15 Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”

Ni tabia ya shetani kujigeuza na kujifanya malaika mtakatifu, hivyo anawarithisha na watoto wake kazi hiyo hiyo, na ndio maana katikati ya kanisa la Mungu leo hii utaona manabii wengi wa uongo na mitume na watumishi wa uongo humo humo. Hiyo ni kazi ya shetani ili kulikoroga kanisa la Mungu lisisimame. Lakini sasa wewe kama mkristo ni jukumu lako kuwatambua, kwasababu biblia inasema mtawatambua kwa matunda yao.. je! Wanayatenda mapenzi ya baba yao aliye mbinguni?..Hilo tu.

Unafundishwa Neno la Mungu na utakatifu? Au mambo mengine, je! Tangu uwepo mahali hapo maisha yako ya kiroho yalishawahi kubadilika au ndio yanazidi kuteterekea?. Unapata matumaini ya utajiri na mali lakini je! Juu ya hayo ulishapata matumaini ya uzima wa milele yanayopatikana kwa kuishi maisha ya utakatifu na kujitenga na dhambi?

10) KUFANYA ISHARA NA MIUJIZA YA UONGO:

Ufunuo 13:13 “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.

14 Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.”

Mambo haya haya yalifanyika wakati wa kipindi cha Musa, wakati wale Yane na Yambre, walipokuja na wao kutoa ishara zao mbele za Musa ili kuwachanganya watu wa Mungu,.hata sasa anafanya hayo hayo, kwa kutumia uchawi wake, anaowapa watumishi wake wa uongo.

Tunaweza kuona kulikuwa na mtu mwingine aliyeitwa Simoni kwenye Biblia, naye alikuwa vivyo hivyo.

Matendo 8:9 “Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.

10 Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.

11 Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake”.

Hivyo kwa kuyafahamu hayo tutaweza kujua ni jinsi gani shetani anavyotuwinda kuliko tunavyodhani, hofu ni kwako wewe uliye nje ya wokovu, nje ya YESU KRISTO utawezaji kuviruka viunzi vyote hivyo vya adui?. Upo katika hatari kubwa sana ya kuangamia na kuishia kuzimu. Kinga tulishapewa nayo ni YESU KRISTO, Amwaminiye yeye shetani kwake ni kama KIKARAGOSI!! Kisichoweza kumfanya lolote, wala kumdhuru. Lakini ukiwa nje ya Kristo shetani kwako ni mungu wako, atakufanya anachotaka.

Uamuzi ni wako, TUBU leo ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kimaandiko upate ondoleo la dhambi zako, uingie katika familia ya wana wa Mungu, furahani kwa Bwana, mahali ambapo chemchemi ya maji ya uzima inapobubujika. Mahali ambapo hakuna aliyemfuata akajuta. Tulikuwa na sisi katika dhambi kuliko wewe lakini sasa tunapata raha ndani ya Kristo Yesu, Ingia na wewe ujionee mwenyewe..

Ubarikiwe …

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SHETANI NI NANI?

HUDUMU YA MALAIKA WATAKATIFU.

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

KAENI NDANI YANGU NAMI NDANI YENU.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/05/13/zifahamu-huduma-kuu-10-za-shetani-duniani/