DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.

by Admin | 21 June 2019 08:46 am06

Biblia inatueleza kuwa kuna aina mbili za dhambi, zipo dhambi zinazomtangulia mtu kwenda hukumuni na zipo dhambi zinazomfuata mtu hukumuni. Na leo tutaona hizi dhambi ni zipi:

1Timotheo 5:24 ‘Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata’.

Unajua ni heri kitu kinachokutangulia kuliko kile kinachokufuata, kwasababu kinachokutangulia siku zote kipo mbele yako unakiona, na hivyo kuona madhara yake na kutafuta njia ya kukikwepa ni rahisi, lakini kile kinachokufuata kipo nyuma yako, na wakati mwingine unaweza hata usijue kama kuna hatari nyuma yako mpaka pale kitakapokuletea madhara ndipo utakapojua. Mfano leo hii ukaenda porini kwa bahati mbaya ukakutana na mnyama DUBU, ikatokea ukafanikiwa kumponyoka na kukimbia mbali kidogo kwenda kupumzika labda tuseme umbali wa kilometa moja, Ni rahisi kudhani kuwa umempoteza, ni kweli kwa wakati huo utakuwa umempoteza hayupo pamoja na wewe, lakini Dubu ni mnyama mwenye uwezo mkubwa wa kunusa kuliko wanyama wote porini, anao uwezo wa kunusa chakula chake mahali kilipo zaidi ya kilometa 30 na kukifuata. Huo ni umbali kutoka Daresalaam mpaka Kibaha.. Hivyo haijalishi atachukua siku ngapi kukufikia, atakuwa anakufuatilia taratibu mpaka mwisho wa siku atafika pale ulipo na madhara yatakukuta.

Ndivyo ilivyo asili ya dhambi, zipo dhambi ambazo ni dhahiri kabisa zipo mbele ya mtu zinaonekana, hizo tayari zimeshafika hukumuni na kumurudishia majibu yake kuwa anastahili jehanamu. Kwamfano mtu anapokuwa msagaji au shoga, hana haja ya kujihakiki mara mbili kama yeye ataenda motoni au la! Ni dhahiri kuwa anachofanya si Mungu tu kakitaa bali hata jamii imekikataa, vivyo hivyo na anayezini, anayeua, anayefanya kazi ya ujambazi,anayetoa mimba, mchawi, mshirikina, n.k. hizi ni dhambi zilizodhahiri kabisa haihitaji mtu kusubiri kupandishwa kizimbani achunguzwe ndio ahukumiwe, akiwa hapa hapa duniani ameshajua yeye ni wa motoni tu moja kwa moja. Na hizi ni rahisi kuziepuka ikiwa unafanya mfano wa vitu kama hivyo, nakushauri utubu haraka sana ndugu umgeukie Mungu.

Lakini zile zinazomfauta mtu, ni dhambi za siri, ambazo kwa macho ya kawaida ni ngumu kuziona na dhambi hizi huwa mtu ni rahisi sana kuzifanya na rahisi pia kuzisahau, kwamfano mtu anapozungumza maneno yasiyokuwa na maana, mizaha kumuhusu Mungu, kama vile Yesu alivyosema katika Mathayo 12:36 “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. 37 Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

Sasa Siku ile ya hukumu anaweza kudhani atahukumiwa kwa mambo yaliyodhahiri tu, lakini mazungumzo yote yatawekwa wazi Hizo ndio dhambi zinazokufuata.. Vitu vingine ni kama vinyongo, kutokusamehe, visasi, usengenyaji,uzishi, n.k.Yote haya mtu anaweza akawa navyo watu wasijue, au pengine yeye mwenyewe asijue kuwa ni makosa, siku ile ya hukumu ndipo atakaposhangaa ni nini hiki.?..Mfano dhambi ya kutokusamehe hii ndio itakayowashitusha wengi sana siku ile…watasema mbona mimi niliomba toba zote kwa Mungu, iweje Mungu hakunisamehe dhambi zangu..Lakini hakujua kuwa Bwana alisema ‘msipowasamehe watu makossa yao na Baba yenu wa mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu’.

Lakini vile vile Kumbuka “kifungu hicho hicho” kinatuambia yapo MATENDO MEMA yanayomtangulia mtu hukumu na yale yatakayomfuata.

1Timotheo 5:24 ‘Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.

25 VIVYO HIVYO MATENDO YALIYO MAZURI YA DHAHIRI; WALA YALE YASIYO DHAHIRI HAYAWEZI KUSITIRIKA’.

Unaona, mtu pia akitenda matendo mema iwe ni kwa siri au kwa dhahiri hakuna lolote litakalosahaulika, kama tu vile dhambi ya siri na isiyo ya siri isivyosahaulika.

Mhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, LIKIWA JEMA AU LIKIWA BAYA.”

Sasa Matendo yaliyo dhahiri ni kama yapi?, mfano kama kufanya kazi ya Mungu, kusaidia ndugu,na kusaidia yatima, kuwa mtetezi wa watu, kupatanisha, n.k…

Lakini pia yapo matendo mema yaliyositirika, ambayo kwa macho ya kawaida mtu yeyote hawezi kuyaona, na rahisi pia kuyatenda na kuyasahau, mfano wa hayo ni kama vile kuombea wengine na kubariki, kuwaombea watakatifu na kanisa la Mungu kwa ujumla, kumtetea mtu Fulani aliyeonewa, kumsamehe mtu Fulani n.k..

Hivi ni vitu ambavyo siku ile ya hukumu huyu mtu aliyekuwa anavitenda atasimama akidhani hakuna lolote alilolifanya kwa Mungu..Lakini atashangaa siku hiyo thawabu zake zinakuja mahali asipojua atauliza hizi zinatoka wapi? ndio hapo Bwana atamkumbusha, kwa yale maombi yako ya kila siku aliyokuwa analiombea kanisa na watakatifu wote, Fulani na Fulani aliokoka kwa hayo…Fulani na Fulani alisimama kwa kupitia hayo..Fulani na Fulani aliponywa kupitia hayo.(Yakobo 5:16). Ipo faida kubwa sana kutenda mema bila kutarajia malipo au kuonekana na watu kwasababu siku ile matendo yako mema yatakufuata.

Ufunuo 14.13 ‘Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao’.

Hivyo ndugu kila mmoja wetu atasimama hukumuni, lakini lipo tumaini zuri kwa wewe ambaye bado upo kwenye dhambi, njia pekee ya kufutiwa hilo deni la mzizi wa dhambi zako, iwe ni zile zilizokutangulia au zinazokufuata dawa ni moja tu, Ni kumkabidhi leo Bwana YESU maisha yako. Huo ndio mwanzo wa Uzima.

Yeye atakusamehe kabisa, na siku ile, hakutakuwa na shitaka lolote juu yako. Wala hakutakuwa na harufu yoyote ya dhambi itakayokufuata, kwasababu sasahivi jambo atakalolifanya ikiwa utamruhusu aje ndani ya maisha yako ni kuhakikisha anaweka dhambi zako zote mbali na wewe kama vile Mashariki ilivyo mbali na Magharibi. Kwasababu anakuhurumia na kukupenda. Hapo ndipo tunaopoona faida ya DAMU ya YESU isiyoweza kuharibika.Haleluya!!

Zaburi 103: 11 “Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.

12 Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.

13 Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.

14 Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi”.

Hiyo yote ni ukiwa tayari kutii.

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

DHAMBI YA MAUTI

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

JE! KUBET NI DHAMBI?

MSHAHARA WA DHAMBI:

DHAMBI YA ULIMWENGU.

NGUVU YA UPOTEVU.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/06/21/dhambi-zinazotangulia-na-zinazofuata/