KWANINI YESU ALIMUITA BABA YAKE “ABA”?

by Admin | 30 June 2019 08:46 pm06

Hili Neno Aba kwa mara ya kwanza katika biblia lilisikika likitamkwa na Bwana wetu Yesu, Hili ni Neno la Kiaremi(Aramiac), moja ya lugha ambayo Bwana Yesu alionekana akiizungumza mara kwa mara, maneno mengine yaliyorekodiwa ambayo Yesu alionekana akiyatamka yanayotokana na lugha hii hii ni pamoja na “Talitha kumi (Marko 5:41), Efatha (Marko 7:34), Eloi Eloi lama sabakthani (Mathayo 27:46) na hili Neno Aba lenyewe.”. Hivyo hii Lugha ya kiaremi ni lugha iliyokuwa imekaribiana sana na lugha ya kiyahudi isipokuwa hii ilikuwa imetohoa maneno mengi kutoka katika lugha za tamaduni nyingine kama vile Babeli n.k.. Hivyo kwa ujumla lugha hizi tatu yaani kiyahudi, kiaremi na kigiriki, Ni lugha ambazo Bwana Yesu alionekana akiziongea..

Sasa hili Neno Aba lina maana ya Baba katika lugha hiyo, Ni neno lenye uzito zaidi ya kusema Baba tu peke yake, Tukitumia mfano wa lugha ya kiingereza tunaweza kuelezea hali hiyo ikoje..kwamfano mtu anayemwita Baba yake, Father na yule anayemwita baba yake “Daddy”,kuna tofauti kubwa sana hapo. Utagundua huyu anayemwita Baba yake daddy anamahusiano ya karibu sana kuliko Yule anayemwita father,. Father anaweza akawa ni baba anayekupenda, anayekujali, anayehakikisha unapata mahitaji yako yote ya muhimu, chakula, nguo, shule, anakujengea nyumba, na n.k..lakini mtoto ambaye anamwona baba yake kama Daddy, licha tu ya kutimiziwa mahitaji yake muhimu, lakini juu ya hilo utamwona mtoto anamfurahia baba yake na anaoujasiri mwingi kwake, akimwona anaweza hata akaenda kumrukia, anaweza akamshirikisha mambo yake yote kama vile rafiki yake, hata wakitembea barabarani mtu anaweza asijue kama ni mtu na Baba yake wanatembea lakini kiuhalisi ni Baba yake tena anayemuheshimu sana. Hiyo ndio Daddy.

Sasa ndivyo hili Neno Aba lilivyomaanisha, Aba ni bonus+ ya BABA.. Kwa ule uhusiano ambao Bwana Yesu aliokuwa nao kwa Baba yake, hakukuwahi kutokea mtu yoyote duniani kuwa na uhusiano mkuu wa namna ile, utaona mpaka dakika ya mwisho anapitia majaribu mazito namna ile, akijua kabisa na Baba yake ndiye aliyempitisha katika hali ile mbaya ya dhiki, lakini bado utaona anamwita ABA..

Embu leo hii Mungu ayakorofishe mambo yetu yasiende vizuri, au tupungukiwe kidogo tu, utaona kila aina ya malalamiko na manung’uniko yatakayotoka katika vinywa vyetu kana kwamba Mungu anafurahia wewe uwe hivyo.

Marko 14:36 “Akasema, ABA, BABA, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”

Hivyo unaweza pia ukaona lengo kuu la Yesu kuja duniani na kuishi maisha ya dizaini ile lilikuwa ni kututhibitishia sisi ni kwa jinsi gani Mungu anaweza akawa karibu na wanadamu kama mtoto na Daddy wake kwa viwango vya hali ya juu sana lakini ikiwa atukuwa tayari kutii.. Mambo ambayo hapo nyuma yalikuwa hayawezekani, na ndio maana hata wayahudi walimwona kama anakufuru kumuita Mungu Baba yake mpaka wakataka kumuua kwasababu hiyo (soma Yohana 5:18).

Mambo ambayo hata sasa bado yanawakera watu wengi hususani wale wa upande wa pili ( dini ya kiislamu), wanasema ni kufuru kumwita Mungu Baba kwani Mungu hajazaa, wala hana mshirika, sisi ni viumbe vyake basi, mengine zaidi ya hapo ni kufuru…Ni kweli kabisa wanachokisema ni sahihi, kwasababu mtu kufanywa kuwa mwana wa Mungu si jambo jepesi jepesi na la kujiamulia tu kwamba na mimi leo ni mwana wa Mungu, hiyo haipo hivyo huo ni UWEZO unatoka kwa Mungu mwenyewe..Na uwezo huo wanapewa wale tu wanampokea YESU kwa kumaanisha kabisa kumgeukia yeye. Sio kwa kukiri tu katika vinywa vyao, hapana bali ni kwa kukiri na kuamua kumfuata yeye.

1Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Na ndio maana sisi tuliookolewa tuna ujasiri mwingi wa kumwendea Mungu, kwasababu yeye kwetu sio baba tu bali ni “ABA Baba”. Na Roho Yule Mtakatifu tuliyepewa anatushuhudia kuwa sisi tu watoto wa Mungu.Hivyo ujasiri wetu katika hilo ni mwingi.

Warumi 8:15 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.

16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;

17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

Unaona, ukiwa mtoto wa Mungu huna hofu yoyote, Ni wazi kuwa ujasiri utakuja wenyewe tu kwasababu Daddy yupo!!. Hii ni neema kubwa ambayo hatukustahili kuipata, ni neema ambayo mpaka kwa wengine inaonekana ni kufuru, kwanini tusiithamini.?

Wagalatia 4:6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ABA, YAANI, BABA.

7 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”

Pengine na wewe tangu zamani umekuwa mkristo-jina tu, Na ndio maana Huuoni u-baba wowote wa Mungu ndani yako, hiyo yote ni kwasababu umekuwa mtu wa nia mbili, huku unataka dunia huku na bado unamtaka Mungu..Na Bwana amesema huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja, ikiwa na maana huwezi kuwa na MA-BABA wawili kwa wakati mmoja. Ikiwa leo utachukua uamuzi wa kusimama upenda wa Kristo moja kwa moja nataka nikuambie ukweli Mungu hutamwona kama BABA tu, bali kama ABA…Kama Daddy ndani yako. Hilo ndio lengo Yesu lililomleta duniani ni ili akufanye wewe kuwa hivyo.

Tubu dhambi zako leo, kama hujaanya hivyo..na chukua uamuzi wa kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na katika jina la YESU KRISTO, kama hukubatizwa, kisha baada ya kutii maagizo hayo Mungu atakushushia mwenyewe Roho wake ndani yako atakaye lia Aba, Hiyo ni kukushuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mungu, kweli kweli kuanzia huo wakati na kuendelea.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

  1. MWANA WA MUNGU.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

JE! WEWE NI MWANA WA IBRAHIMU?

JE! WEWE NI MBEGU HALISI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/06/30/kwanini-yesu-alimuita-baba-yake-aba/