Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09

SWALI: Biblia inaposema “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. (Mathayo 5:3)”je hatuna ruhusa ya kuwa matajiri katika roho?.

JIBU: Maskini ni mtu ambaye yupo katika hali ya kutojitosheleza, Sasa Bwana aliposema “heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao”, hakumaanisha kuwa HERI wale wasio na maarifa yoyote au ufahamu wa mambo ya rohoni (yaani watu wasiomjua Mungu), hapana bali alimaanisha heri wale ambao kila siku wapo katika hali ya uhitaji wa kufahamu mambo ya ufalme wa mbinguni, watu ambao hawajajikinai, watu ambao kila siku wanatamani kuongeza kitu kipya katika maisha yao ya rohoni, watu wenye kiu na njaa ya kumjua Mungu kila siku…

Hao ndio Mungu anawaona ni maskini wa roho ambao kila siku wanamlilia yeye BABA, tupe! Tupe! Chakula cha rohoni..Lakini kuna wengine hawana haja tena ya kujua zaidi mambo ya rohoni, tayari wameshahitimu, pengine labda kwa kuwa walipitia vyuo vya biblia, au wameshasoma sana maandiko, hivyo wanajiona sasa wanajua kila kitu, hawana haja tena ya kujifunza, hata wakiletewa habari ya mpya wanadharau moyoni mwao wanaona kwamba hakuna chochote huyu mtu anaweza kuniongezea? Ndivyo ilivyokuwa kwa wale waandishi na mafarisayo.

Hawakutaka kukaa chini kuyasikiliza maneno ya YESU walimdharau na kumwona si kitu tofauti na yale makutano walimsikiliza kwasababu ndani yao kulikuwa na kiu na njaa na shauku ya kumjua Mungu zaidi na zaidi, na ndio maana Bwana Yesu akazungumza maneno yale.Ikiwa wewe unajiona hapo katika dhehebu lako ndio umefika, na hivyo huna haja ya kuambiwa chochote hata kama kinatoka kwenye maandiko basi fahamu kabisa kuwa upo mbali sana na ufalme wa mbinguni.

Ufunuo 3:17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”

Mtume Paulo mpaka anafikia uzee wake, anakaribia kufa pamoja na kwamba Mungu alimfanya kuwa askofu wa mataifa yote, mwenye heshima duniani kote katikati ya waaminio, mtu ambaye Mungu alimpa mafunuo makubwa ambaye hata sasa nyaraka zake tunazitumia kama mwongozo lakini mpaka dakika ya mwisho anamwagiza Timotheo kwamba siku akimfuata vifungoni mwake asiache kumpelekea vile vitabu vya ngozi ili azidi kujifunze zaidi,(2Timotheo 4:13) inatupasaje sisi?…

Huo ni mfano mzuri wa mtu aliye maskini wa roho, haridhiki sehemu alipo, haridhiki na kile alichonacho au alichopewa katika dhehebu lake au dini yake, kila siku anataka zaidi na zaidi amjue Mungu…Sio ajabu mtume Paulo aliandika hivi:1Wakorintho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”Hivyo tupende kila siku kutamani kupiga hatua moja zaidi rohoni, na hiyo inakuja kwa kutokukinai kujifunza Neno la Mungu kila siku.

Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

NOTI YA UFALME WA MBINGUNI

UPONYAJI WA YESU.

NI NANI ANAYEUFUNGA MLANGO WA MAARIFA?

LULU YA THAMANI.

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/biblia-inaposema-heri-walio-maskini-wa-roho-maana-ufalme-wa-mbinguni-ni-waoje-hatuna-ruhusa-ya-kuwa-matajiri-katika-roho/