Wale Watakatifu waliofufuka na Bwana Yesu WALIKUWA WAPI KABLA YA KUFUFUKA kwao je! walikuwa Peponi au ni wapi?.

by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09

JIBU: Wafu wote waliokufa kabla ya Kristo kuja duniani walikuwa makaburini, au sehemu za wafu, mahali pengine katika biblia panapaita Kuzimu, Daudi aliomba katika roho akisema “Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.” (Zaburi 16:10) Aliomba asiende sehemu za wafu iliyo njia ya wote, lakini tunasoma alikufa na akakusanywa na baba zake huko, Lakini kumbe Unabii huo ulikuwa haumuhusu yeye bali Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni yeye pekee nafsi yake haikubaki huko. 

Hivyo biblia haielezi kwa mapana walikuwa wanaishije ishije huko..lakini ni mahali ambapo hatuwezi kusema palikuwa ni salama sana, kwa maana shetani naye kwa sehemu Fulani alikuwa anao uwezo wa kuwasiliana na hata watu wenye haki waliokuwa wamekufa zamani, tunalithibitisha jambo hilo kwa Samweli, (1 Samweli 28)…Na hiyo ni kwasababu ya kuasi kwetu ndipo kulipompa shetani baadhi ya funguo za kututawala sisi hata mpaka baada ya kufa kwetu..japo alikuwa hana uwezo wa kuwaondoa mahali walipokuwepo…Lakini Kristo alipokuja na kushinda vyote pale msalabani, ndipo akachukua funguo zote za kuzimu na mauti na sasa wafu wote anawamiliki yeye.

Ufunuo 1: 17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,

18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

Hivyo leo hii hakuna mtu au pepo lolote, au shetani anayeweza kuwasiliana na mtu wa aina yoyote yule aliyekufa ile awe mwenye dhambi au asiye na dhambi isipokuwa YESU peke yake..Ukiona mtu anakuambia mzimu wa baba yangu, au bibi yangu umenijia basi ujue kuwa hilo ni PEPO lililojigueza na kuvaa sura ya yule mtu,na wala si yule mtu halisi..Sasa kukaa kwake Bwana kaburini zile siku tatu, kulikuwa ni kushuka kuzimu huko wafu wote walipo ili kuwatenga wale wafu waovu na wema kwa injili aliyokwenda kuwahubiria.

1Petro 3:18 “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,

19 AMBAYO KWA HIYO ALIWAENDEA ROHO WALIOKAA KIFUNGONI, AKAWAHUBIRI;

20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”. 

Sasa wale wema ambao waliishi maisha ya haki duniani na ya kumcha Mungu walihamishwa na kupelekwa mahali pa raha zaidi, ambapo panajulikana kama PEPONI/PARADISO (Kule alipomwambia yule mwizi aliyesulibiwa kuwa atakuwepo naye siku hiyo hiyo peponi)…Lakini wale waovu waliosalia walisogezwa mahali pa shida zaidi huko huko kuzimu…. Na katikati yao kukawekwa SHIMO kubwa ili wa kule wasiweze kuja huku na wa huku kwenda kule katika Roho,..Wale wema walipandishwa juu, lakini waovu walizidi kukaa chini na ndio maana yule tajiri katika habari ya Lazaro utamwona akinyanyua macho yake na kumwona Lazaro upande wa pili kule kuzimu.

 Luka 16:19 “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.

20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,

21 naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.

22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.

23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.

24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.

25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.

26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.

27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,

28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.

29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.

30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.

31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”.

 Sasa tukirudi kwenye swali wale wafu walikuwa wapi, ndio hapo siku ile Bwana aliyofufuka utawaona wafu watakatifu wakitoka makaburini, na kuhamishiwa Peponi,..Hivyo mtu akifa leo katika haki moja kwa moja anapanda peponi/paradiso akisubiria UFUFUO wa Haki siku ile ya unyakuo..lakini atakayekufa katika dhambi, naye moja kwa moja atateremka Jehanum, kwenye mateso makali akingojea naye kufufuliwa siku ile ya hukumu mbele ya kiti kile cheupe cha Enzi cha Mwanakondoo ahukumiwe kisha atupwe kwenye lile ziwa la moto

 Hivyo huu ni wakati wa kuweka mambo yetu sawa, yasije yakatukuta kama yale ya yule tajiri, biblia inasema itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima na mwisho wa siku tupate hasara ya nafsi zetu.?. Kiburi cha mwanadamu ni maua leo kipo kesho kinanyauka, ikiwa leo utajikuta haupo tena duniani..Huko uendako utakuwa mgeni wa nani? Huko hakuna nafasi ya pili.

Wokovu unapatikana bure sasa, ukikupita leo kesho utautafuta kwa kilio na kusaga meno na hautauona.. Ni maombi ikiwa maisha yako yapo mbali na Kristo basi leo fanya uamuzi wa kumkabidhi yeye maisha yako na yeye ana upendo na ni mpole na ameahidi kukupokea, na kuwapokea wote wanaomkimbilia yeye.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.

UPONYAJI WA YESU.

HERI, WALE MUNGU ASIOWAHESABIA MAKOSA YAO.

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

MNGOJEE BWANA

VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA

TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?


 

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/wale-watakatifu-waliofufuka-na-bwana-yesu-walikuwa-wapi-kabla-ya-kufufuka-kwao-je-walikuwa-peponi-au-ni-wapi/