by Admin | 3 September 2019 08:46 pm09
SWALI: Huyu AZAZELI ni nani? Kwa sababu ukisoma maandiko naye aikuwa anapewa kafara? (Walawi 16:8).
JIBU: Neno Azazeli linaonekana likitajwa mara moja tu katika kitabu cha Mambo ya Walawi sura ya 16, Azazeli sio mtu au kuhani bali ni mbuzi aliyetengwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi za Wana wa Israeli ndiye aliyejulikana kwa jina hilo, ambaye yeye hakuwa anachinjwa kwa ajili ya dhambi kama mbuzi wengine hapana bali yeye alikuwa anachukuliwa akiwa hai mpaka jangwani na kutelekezwa huko.
Maagizo hayo Mungu aliwapa wana wa Israeli, wayafanye katika siku ile kuu ya Upatanisho ambayo ilikuwa inafanyika mara moja tu kwa mwaka, tarehe 10 mwezi wa 7 wa kalenda ya Kiyahudi, wakati huo ndio ule Kuhani Mkuu anakwenda kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za wayahudi wote siku hiyo kila mtu alipaswa asifanye kazi yoyote, bali unatulia nyumbani kwake ukiitesa nafsi yake kwa dhambi zake.
Sasa katika siku hii Kuhani Mkuu kwanza anawajibika kufanya upatanisho kwanza kwa ajili ya nafsi yake yeye mwenyewe na ya watu wake (wa nyumbani kwake), kisha ndio aende kufanya upatanisho wa dhambi za watu wengine, vinginevyo atakufa. Sasa katika kufanya upatanisho wa wana wa Israeli aliagizwa atwae mbuzi wawili kutoka katika mkusanyiko wa Wayahudi kwa sadaka ya dhambi na kondoo mmoja mume kwa sadaka ya kuteketezwa (Walawi 16:5), baada ya hapo kuhani mkuu anasimama mbele ya hema na kupiga kura kati ya wale mbuzi wawili.
Walawi 16:7 “Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania.
8 Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.”
Akishamaliza mmoja anachukuliwa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa dhambi za watu wote,
kisha damu yake inachukuliwa na kwenda kunyunyizwa katika hema ya kukutania na madhabahu, na yule wa pili hauliwi bali kuhani mkuu anamchukua na kuweka mikono yake yote miwili juu ya pembe za Yule mbuzi ambaye ndio anaitwa Azazeli kisha kuhani anaungama makosa yote na dhambi zote za wana wa Waisraeli walizozifanya juu ya mbuzi Yule,..baada ya hapo mbuzi huyo anakabidhiwa kwa mtu mmojawapo kisha anapelekwa jangwani mbali kabisa na makazi ya watu na kutelekezwa huko. Ndipo ouvu wa Israeli unafunikwa.
Walawi 16:21 “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.22 Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.”
Ni picha kamili tunayoiona katika agano jipya, Kristo akiwa kama Azazeli wetu alichukua dhambi zetu na mashutumu yetu yote, akasulibiwa nje ya mji, alihesabiwa kuwa si Kitu kwa ajili yetu.. Na kwa kupitia yeye dhambi zetu zinaondolewa moja kwa moja, tofauti na mbuzi Yule ambaye ikifika mwakani anapaswa atolewe mwingine…Ni raha kiasi gani ukikombolewa na Kristo,.Ukisamehewa dhambi zako, umesamehewa milele. Haleluya.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?
SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?
SANDUKU LA AGANO LILIKUWA LINAWAKILISHA NINI KATIKA AGANO JIPYA?
NAOMBA KUJUA WATAKAOENDA MBINGUNI JE! NI WENGI AU WACHACHE?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/03/huyu-azazeli-ni-nani-tunayemsoma-katikawalawi-168/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.