Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?

by Admin | 3 September 2019 08:46 pm09

Swali ambalo ni wajibu wetu sote kulijua ni juu ya Roho saba za Mungu, kwamba zenyewe ni nini na zinatendaje kazi. Na pia ni muhimu kufahamu juu ya makanisa saba

JIBU: Tukisoma mandiko yanatuambia kuwa Mungu ni mmoja, agano la kale linatuthibitishia hilo, (Kumb 6:4), vile vile agano jipya linatuthibitishia hilo, tukisoma katika (Marko 12:29) pale Bwana Yesu alipofuatwa na Yule mwandishi na kuulizwa ni amri ipi iliyo ya kwanza alijibu..


“….Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; 30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.”

Hivyo maagano yote mawili yanathitisha kuwa Mungu ni mmoja, lakini sasa kwanini tunamwona YESU kama Mungu, kwanini tunamwona Roho kama Mungu, tena tukiendelea kusoma tunaziona kuna Roho nyingine saba za Mungu, swali ni je! hawa wote wametokea wapi, ikiwa Mungu ni mmoja?.Hili ni moja ya swali lililoleta migawanyiko mikubwa sana sio tu katika ukristo, bali hata kwa wale wasioamini limewafanya wazidi kwenda mbali zaidi kwa kushindwa kuelewa utendaji kazi wa Mungu.

Tukiweza kujua kuwa kitu kinachoitwa Dhambi na kutengwa mbali na uso wa Mungu ndicho chanzo kilichopelekea tumwone Mungu katika taswira nyingi tofauti tofauti, tukilifahamu hilo basi hatutashindwa kumwelewa Mungu katika nafasi yake ya Uungu.. Na ameamua kufanya hivyo makusudi kwa lengo la kuturejesha sisi asingefanya hivyo leo hii tungekuwa makapi sisi. Laiti kama tusingeanguka katika dhambi, tungemwona Mungu na kuzungmza na Mungu kama yeye tu tusingejua kitu kingine cha ziada kumuhusu yeye, tabia zake zilivyo.

Kwamfano kulikuwa hakuna sababu ya Mungu kuutafuta mwili na kuiweka Roho yake mwenyewe ndani yake aje asulibiwe ili atupatanishe sisi na yeye kama tusingepotea katika dhambi, vile vile kulikuwa hakuna haja ya Roho Mtakatifu kuwa msaidizi wetu kama tungekuwa tunazungumza na Mungu uso kwa uso kama ilivyokuwa pale Edeni Adamu alipokuwa anazungumza na Mungu..

Ni sawa tu ni kifaa kinachoitwa simu, kama sio suala la umbali kati ya mtu mmoja na mwingine, simu isingehitajika katika jamii, kusingekuwa na haja ya wewe kuisikia sauti yangu kwenye kifaa kinachoitwa simu..Lakini je! Fikiria pia siku ile uliposikia mimi ninazungumza ndani ya kifaa kile, je ulisema nimegawanyika?, na kuwa wawili, kwamba mimi unayeniona tukizungumza uso kwa uso ni tofauti na Yule unayenisikia kwenye kifaa-simu? Ukweli ni kuwa utasema ni kifaa tu lakini mimi ni Yule Yule..Na ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu kuja kwake duniani, ..yule ni Mungu yule yule kauvaa mwili lakini sio MUNGU wa pili katika UUNGU, kama wengi wanavyodhani…YESU na Mungu BABA, sio Mtu na Mtu mwenzake, Ni Mungu yule Yule mmoja isipokuwa amekuja kwetu katika vazi lingine.
Kwa maelezo marefu ya kufahamu kwanini Yesu alikuja duniani, tutumie ujumbe inbox tukutumie somo lake..

Vivyo hivyo na Roho wake Mtakatifu, Yule sio Nafsi ya Tatu katika uungu bali ni ofisi ya tatu ya Mungu Yule Yule mmoja katika hatua zake za kuturejesha sisi katika mstari wake wa ukamilifu..Kama tusingekuwa katika hali ya dhambi na kumsahau Mungu, basi hakukuwa na haja ya sisi kupewa msaidizi, lakini Mungu aliona ajitoe sehemu ya nafsi yake iliyo moja aje kwetu kama Roho Mtakatifu ili atukumbushe yale yote Bwana Yesu aliyotuagiza.(Yohana 14:26).

Vile vile Roho Mtakatifu alipoachiwa pale Pentekoste, hakuachiwa kwa mtu mmoja mmoja tu peke yake kama wengi wanavyodhani, bali aliachiwa pia na kwa kanisa kwa ujumla..Hivyo kulikuwa na makanisa tofauti tofauti kulingana na wakati na majira..Sasa Roho huyu huyu aliyetenda pia kazi tofauti tofauti kulingana na kanisa husika..Ndio yale makanisa saba tunayoyasoma katika kitabu cha ufunuo sura ya 2&3, ..


Ufunuo 1:4 Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;

makanisa saba

Sasa biblia inaposema Roho saba za Mungu nadhani utakuwa umeelewa kuwa hakuna tena Roho nyingine 7 zilizo mbele za Mungu, bali ni Roho Yule Yule mmoja akitenda kazi katika yale makanisa saba, Biblia inasema pia ndio macho 7 ya Mungu (Ufunuo 5:6), Na Taa 7 za moto (Ufunuo 4:5).
Kwa maelezo marefu juu ya nyakati saba za Kanisa,pia tutumie ujumbe inbox tukutumie somo lake..

Hivyo hizo zote ni hatua za Mungu za utendaji kazi lakini ni yeye Yule Yule, Mungu mmoja, hajagawanyika..


Lakini Swali lingine mtu anaweza kuuliza je! Tunafanya makosa kumwabudu YESU au Roho Mtakatifu? Jibu ni hapana, unapomwabudu Bwana YESU umemwabudu Mungu Yule Yule mmoja, Unapomwabudu Roho Umemwabudu Mungu Yule Yule mmoja, ni ofisi tu imebadilika, lakini Mungu ni Yule Yule umwabuduye..

Hivyo YESU ni Mungu mwenyewe katika mwili (1Timotheo 3:16), Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe katika roho, vile vile zile Roho 7 za Mungu ndio Yule Yule Roho mmoja na ndio Mungu mwenyewe YEHOVA muumba wa mbingu na nchi, Hana mwanzo wala hana mwisho, ALFA NA OMEGA. Haleluya!

Je unampenda kwa moyo wako wote? Jibu unalo.


Ubarikiwe.


Mada zinazoendana:

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

JINA LA MUNGU NI LIPI?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

MJUE SANA YESU KRISTO.

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/03/je-hizi-roho-saba-za-mungu-ni-zipi-na-je-zinatofautiana-na-roho-mtakatifu/