UMUHIMU WA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUZAA MATUNDA.

by Admin | 19 September 2019 08:46 pm09

Shalom mtu wa Mungu, karibu tutafakari maandiko pamoja.
 
Biblia inasema katika Kitabu cha Yohana 15:16 kwamba “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni”
 
Tumepewa jukumu la kuzaa matunda, na matunda hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza ni matunda ya Haki, ambayo hayo yanatokana na utakatifu, tunayasoma hayo katika
Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.
 
Na aina ya pili ya Matunda, ni matunda ya KAZI, ambayo hayo yanatokana na kuwaleta watu kwa Kristo,
 
Wafilipi 1:21 “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
 
22 Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui.”
 
Hivyo Kristo ametuweka tuzae aina hizi mbili za matunda…Matunda ya HAKI na Matunda ya KAZI..Hivi viwili vinakwenda pamoja…Na vyote vinahitaji Mafuta ya Roho Mtakatifu ili viweze kufanyika. Ili tuwe watakatifu tunahitaji Mafuta ya Roho Mtakatifu…Kwasababu kama jina lake lenyewe lilivyo..Roho Mtakatifu, hivyo kila ampataye yeye ni lazima atakuwa mtakatifu tu.
 
Kadhalika ili tuweze kuleta matunda mengi kwa Kristo tunamhitaji Roho Mtakatifu, kwasababu yeye ndiye anayehusika katika kumshawishi mtu ndani ya moyo wake amgeukie Kristo.. 1 Wakorintho 2:4 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu”
Na leo tutajifunza umuhimu wa Roho Mtakatifu katika kuzaa matunda katika hizi siku za mwisho.
Kazi ya kuwavuta watu kwa Kristo imefananishwa na kazi ya uvuvi…Sharti ni kwamba ili mtu akavue samaki ni lazima atimize masharti makuu 5..
 
Sharti la kwanza ni lazima awe na mtumbwi unaoelea, sharti la pili ni lazima awe anajua kuogolea, sharti la tatu ni lazima awe na nyavu au ndoano, sharti la 4 Ni lazima aende usiku na sharti la 5 na la mwisho ni lazima awe na TAA..Akitimiza masharti hayo 5 basi ni lazima apate samaki..hawezi kukosa chochote aendapo anavua baharini…
 
Masharti hayo hayo pia yanatumika katika roho kwa uvuvi wa watu…
 
Sharti la kwanza: Kama vile mvuvi ni lazima awe na mtumbwi unaoelea na ni lazima akae juu ya huo mtumbwi ili aweze kuvua…vivyo hivyo katika Uvuvi wa watu ni lazima mtu awe juu ya Mtumbwi unaoitwa YESU KRISTO, na ni lazima mtu awe juu ya huo mtumbwi sio mbali au nje ya huo mtumbwi…huko nje ni kwa watu wasiomjua Mungu, ulimwengu unafananishwa na bahari ambayo imejaa watu wasiomjua Mungu ambao wanahitajika kuvuliwa..Hivyo haiwezekani mtu aliye nje ya Kristo kuwahubiria watu waje kwa Kristo kama vile ilivyo ngumu mvuvi kuwa nje ya mtumbwi na kuvua samaki.
 
Sharti la pili: Ni lazima mvuvi awe anajua kuogelea kabla hajaenda kuvua samaki…awe na uwezo endapo ikitokea ajali akaanguka ghafla majini awe na uwezo wa kurudi tena mtumbwini…sio endapo Kazama ndio anapotelea huko moja kwa moja…Kadhalika na mvuvi wa Roho za Watu ni lazima awe na uwezo wa kujihadhari na dunia, kwasababu dunia ni kama bahari, ukizama na ukiwa hujui namna ya kujitoa huko unazama moja kwa moja na kufia huko…Kwahiyo Ni kama tunaonywa kamwe tusidhubutu kwenda kuhubiri injili kama tunajua hatujaacha sisi wenyewe mambo ya ulimwengu huu, kama tunajua hatuwezi kuushinda na kujinusuru na ulimwengu…ni afadhali tusiende kuhubiri injili kabisa kuliko kwenda na kuzama huko… kwasababu endapo tukianguka tunakuwa tumeanguka moja kwa moja hakuna kurudi tena..
 
2 Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
 
21 Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa”
 
Sharti la Tatu: Ni lazima mvuvi awe na ndoano au nyavu…Ndoano au nyavu zinawakilisha Neno la Mungu, pamoja na ishara na miujiza…Vitu hivi biblia inasema waaminio wote vitaambatana nao…Ni lazima tulifahamu Neno ndipo tuende kuwahubiria wengine…
 
Sharti la Nne: Ni lazima mvuvi aende usiku kuvua, wavuvi wote wanaomaanisha kupata samaki huwa hawaendi mchana kwani wanajua hawatapata kitu, ni lazima aende usiku, kadhalika hata wakati huu wa sasa tunapaswa tuende ulimwenguni kote kulikojaa giza…Matendo ya dhambi yote ni matendo ya giza, na dunia yote imejaa giza kutokana na dhambi za wanadamu…lakini leo Utashangaa mtu anapambania awe mhubiri kanisani kila siku, lakini hataki kwenda mitaani mahali ambapo makahaba wapo, mahali penye giza…tukihubiri kanisani mahali ambapo kuna mwanga ni sawa tunaingia na mshumaa ndani ya nyumba ambayo tayari ina bulb inayowaka sana..Hivyo ni lazima tuenda na mitumbwi yetu, na nyavu zetu sehemu zenye giza mbali sana huko kuvua roho za watu. Na sisi wenyewe tukijihadhari tusipotelee huko.
 
Na Sharti la Tano Na la mwisho: Ni lazima mvuvi aende na TAA..Nyavu peke yake haitoshi kuwaleta samaki, ndoano peke yake haitoshi inahitajika taa…Wataalamu wa masuala ya uvuvi wanasema wakati wa usiku samaki wanapenda kufuata mahali penye mwangaza, hivyo wavuvi wengi hutwaa taa zao juu na kwenda nazo vilindini na hivyo samaki wanapoiona ile Nuru wanaisogelea na hivyo kunaswa…Na sisi tunahitaji Taa yenye Mafuta ili kuwavuta samaki wengi kwenye nyavu zetu, NA Mafuta yanawakilisha Roho Mtakatifu. Hivyo tunahitaji Roho Mtakatifu sana ili Taa zetu ziwe zinawaka sana, katika dunia hii ya giza ili waovu waonapo wamgeukie Bwana.
 
Wafilipi 2:15 “….mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao MNAONEKANA KUWA KAMA MIANGA KATIKA ULIMWENGU”
 
Ukiwa na Mtumbwi, ukiwa na ndoano, ukiwa na nyavu, na ukiwa na ujuzi wote wa kuogelea, kama huna TAA ni kazi bure…utakuwa umwekwenda baharini kubarizi tu na si kuvua..Kadhalika hata tukiwa na tumempa Bwana Maisha yetu, hata tukiwa tunalijua Neno vizuri na kujiepusha na dunia vizuri kama hatuna Roho Mtakatifu, kamwe shughuli ya kuwaleta wengine kwa Kristo itakuwa ngumu sana kwetu.
Hivyo leo tunajifunza tumtafute sana Roho Mtakatifu ajae ndani yetu, kwa maana pasipo yeye hakuna mtu yeyote atakaye vutwa kwa Mungu.
 
Yohana 6: 44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.
Bwana akubariki sana. Wahubirie na wengine habari njema, waujue wokovu wa Bwana Yesu.
 
Bwana akubariki.



Mada nyinginezo:

TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

MUNGU MWENYE HAKI.

MLINZI, NI HABARI GANI ZA USIKU?

LILE TUMAINI LILILO NDANI YETU LINAPOULIZIWA.

NGUVU YA UPOTEVU.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/19/umuhimu-wa-roho-mtakatifu-katika-kuzaa-matunda/