TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?

TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?

Kuna hatua za kupitia, ambazo ni lazima kila mkristo azipitie ili aweze kumzalia Bwana matunda, Bwana alizifananisha hatua hizi na ule mfano wa MPANZI;

Tukisoma

Mathayo 13:2-9 ” Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. 

3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.

 4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; 

5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;

 6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. 

7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; 

8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. 9 Mwenye masikio na asikie. “

TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?

Katika mfano huu tunaona huyu mkulima alienda kupanda mbegu, kumbuka hizi hazikuwa mbegu za kuchimbiwa ardhini, bali zilikuwa ni mbegu nyepesi ndogo za kurusha, na alipokuwa akizirusha alizielekeza zote ziende kwenye udongo mzuri, ili zikue na kuzaa matunda, hizi tofauti na mbegu zile za kupanda ambapo mkulima huenda moja kwa moja kwenye udongo mzuri na kuzifukia ardhini, lakini hizi ni tofauti, tunaona zilipewa nguvu ya kutembea kwa kurushwa ili zifike katika eneo lililokusudiwa la udongo mzuri. Lakini  kuna nyingine zilikwama kwenye hatua tofauti tofauti katika safari zao kuelekea kwenye udongo mzuri.

Katika mfano huu hapa mbegu zilipitia katika hatua kuu NNE (4), ambazo ni; NJIANI, kwenye MIAMBA, Kwenye MIIBA, na kwenye UDONGO MZURI. Na hizi ndizo hatua NNE za mkristo katika safari ya maisha yake tangu siku ile ya kwanza anayompa Bwana maisha yake. Tuzitazame hatua hizi kwa ufupi;

HATUA YA KWANZA: NJIANI

Unaposikia injili (NENO) kwa mara ya kwanza, wewe unakuwa ni mbegu iliyorushwa na mkulima ambaye ni YESU KRISTO katika shamba lake, Kumbua Bwana alikusudia wewe ufike kwenye udongo mzuri, lakini mbeleni kuna vikwazo sasa hatua ya kwanza ni wewe kurushwa kutokea NJIANI, hapa unajikuta umeshapokea neno la Mungu (yaani kumpokea Kristo) katika namna ya kawaida unajikuta bado haulielewi lile NENO vizuri, ndani yako unasikia kiu ya kutaka kuendelea kumjua Mungu, hivyo unajikuta hauridhiki katika hali uliyopo ndani kunachemka kutaka kuendelea kujua zaidi, unaenda huku na kule kutafuta majibu ya maswali yako ya rohoni, na unakuwa na kiu pia ya kusoma NENO la Mungu.

Ukiona hali kama hiyo ujue ni ile nguvu ya Roho wa Mungu inakusukuma kusonga mbele kuelekea kwenye udongo mzuri ili ukamee. Lakini kwa upande mwingine unakuta mtu amesikia injili na ile nguvu ya kumfanya aendelee kusonga mbele yaani kutaka kumjua Mungu zaidi haipo ndani yake. anaridhika na hali aliyopo, akikuta kitu kwenye NENO la Mungu asichokielewa hajishuhulishi kutafuta jibu la maswali yake , hivyo anatulia njiani, hapo ndipo shetani anapopata nafasi kuchukua kile kilichopo ndani yake, hapo ndipo linakuja lile neno “aliyenacho ataongezewa na asiyenacho hata kile kidogo alichonacho atanyang’anya”.

Hivyo unamkuta mtu anajiita mkristo lakini matendo yake hayaendani na ukristo, hanufaiki na jambo lolote katika NENO la Mungu ,japo anaenda kanisani kila siku, anaimba kwaya, anasema ameokoka pasipo kujua ibilisi ameshamwondolea ile nguvu ya Roho Mtakatifu na kiu ndani yake imekufa, anakuwa hana tofauti na mtu asiyeamini.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema

Mathayo 13: 19″ Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.”

HATUA YA PILI: KWENYE MIAMBA

Mathayo 13:20-21 “Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. “

Kumbuka hii ni hatua ya pili, ambayo inakuja baada ya kushinda ile hatua ya kwanza, shetani akishaona una kiu, hamu, shauku na bidii nyingi ya kutaka kumjua Mungu, na  kutafuta kuujua ukweli na hatma ya maisha yako ya milele, na maisha ya kumpendeza Bwana, hapo ndipo majaribu yanapoanza, Kumbuka kila mkristo lazima ajaribiwe imani yake, Mungu mwenyewe ndiye aliyeruhusu iwe hivyo, maana ndivyo wana wa Mungu wote walivyopitia huko nyuma.

Sasa katika hali hii, ile nguvu ya Roho Mtakatifu inakusukuma uikabili hatua inayofuata, hapo ndipo unakutana na majaribu kwa ajili ya NENO la Mungu, pengine utapitia, kuchukiwa na ndugu, kutengwa na marafiki, misiba, magonjwa, kufungwa kwa ajili ya Neno la Mungu, kudharauliwa, kuchukiwa kisa tu umeamua kuifuata hiyo imani, wakati mwingine mambo yako mengine kuharibika kwahiyo hali hii inapotokea usiogope ni IMANI yako inajaribiwa ni uthibitisho kwamba ile mbegu bado ipo safarini kuelekea kwenye udongo mzuri, usichukizwe, shika sana ulichonacho.

Bwana hatakuacha hali hii inaweza ikadumu kwa muda mrefu lakini usikate tamaa Bwana hatakuacha yupo nawe. Kumbuka jambo hili litakuja kwa yule tu mtu ambaye hatua ya kwanza ameivuka kikamilifu. lakini safari bado inaendelea.

Lakini wapo watu wengi wakifika kwenye hii hatua wanaizimisha ile nguvu ya kuendelea mbele kwa kuogopa udhia na dhiki na aibu hivyo wanakwazika na kuiacha imani, hawa ndio wale waliokwama katika miamba natamani ndugu yangu wewe usiwe hivyo. kumbuka Bwana Yesu alisema mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

HATUA YA TATU: KWENYE MIIBA

Mathayo 13:22 “Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. “

Shetani akishajua bado unang’ang’ana na NENO na kuzidi kutamaini kufikia utimilifu, na kumtumaini Bwana kuelekea udongo mzuri, japo kuwa unapitia dhiki, udhia, lakini bado upo na Bwana, safari hii hatumii nguvu tena, anakuja na ushawishi, na anafahamu ni mahali gani pa kumkamatia mtu na si pengine zaidi ya Tamaa ya mambo ya ulimwengu huu..hivyo atakuletea nguvu kubwa ya ushawishi ili utamani kuwa kama watu wa ulimwengu huu, kupenda kuwa mali nyingi, kuubadilisha muda wako wa kuwa karibu na Mungu na u-bize, mihangaiko, anasa, Starehe, biashara, ili tu uridhike  na hali uliyopo umzimishe Roho,  Hali kama hii inapokuja wewe umtazame Bwana na ahadi zake usitamani kufanana na watu wa ulimwengu huu, yeye mwenye alisema “sitakuacha wala kukupungukia kabisa” kumbuka Bwana Yesu alichokisema katika mathayo 6.

Hivyo usipunguze muda wako wa kusoma NENO, kusali, kumtafakari Mungu, kutangaza Neno la Mungu, kisa tu! ya kusongwa na mahangaiko ya maisha, bali kinyume chake uongeze muda wako na Bwana, hayo mengine yaweke kando utafute kwanza ufalme wake na haki yake na hayo mengine yote utazidishiwa.

Lakini katika hatua hii wakristo wengi ndipo waliponasiwa na mwovu, walianza vizuri lakini pesa, shughuli, mahangaiko, yamewasonga wamwache Mungu na kupoa hivyo ile Nguvu ya ROHO wa Mungu ndani yao inapoa, wanaacha kutazamia mambo ya ulimwengu ujao badala yake wanaangalia mambo ya ulimwengu huu, wakidhani katika hali yao ya uvuguvugu ya ukristo waliyopo ndiyo wanamzalia Mungu matunda kumbe bado hawajafika.

HATUA YA NNE: UDONGO MZURI

Luka 8:15 “Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa KUVUMILIA. “

Hatua hii ndipo mtu anapokamilishwa kwenye udongo mzuri ili kumzalia Mungu matunda. Kumbuka hatua hii mtu ataifikia kwa KUVUMILIA hari zote tatu zilizopita nyuma, yaani njiani,kwenye miamba, na kwenye miiba, pale mkristo anapolipokea NENO kwa uthabiti wa moyo, kila siku akiendelea kutafuta na kumjua Mungu bila kuchoka japo kuwa adui yupo njiani na majaribu yote, dhiki, udhia, shida, taabu, misiba, kuvunjwa moyo, kukatishwa tamaa, kutengwa, ukame, kufungwa, kuchukiwa kwa ajili ya Kristo, kukana mambo yote ya ulimwengu, naam hata nafsi yake mwenyewe, kwa ajili ya Bwana akizidi kuvumilia hayo yote anakuwa dhahabu iliyosafishwa kwenye moto tayari kwa kusudi na kazi ya Mungu aliyomweka duniani.

Mtu huyu anakuwa ameingia KAANANI yake, Utukufu wa Mungu unafunuliwa juu yake, ili kumzalia Bwana matunda ya haki yaliyokubaliwa. kama alivyosema huyu thelathini, huyu sitini, huyu mia, kulingana na kipimo cha neema alichopimiwa huyo mtu. Wakati huu pia Bwana anambariki kwa vitu vyake vyote alivyovipoteza kwa ajili yake mara mia zaidi kama alivyoahidi katika NENO lake. Na mtu wa namna hii anakuwa na uhusiano wa kipekee na Mungu, na kupewa nafasi za kipekee katika ufalme wa Mungu angalia akiwa hapa hapa duniani.

Kumbuka kuhubiri au kufanya kazi yoyote ya Mungu, kama haujazivuka hizi hatua NNE, hauwezi kumzalia Mungu matunda maana sasa utakuwa umepandwa kwenye udongo gani?. Yatupasa tuyashinde ndipo tumzalie Mungu matunda, kumbuka Yesu alishinda hivyo na sisi pia yatupasa tushinde. BWANA anasema

Ufunuo 3:21 “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. “

Hivyo ndugu tujitahidi mimi na wewe, tufikie hapo ili tumzalie Bwana wetu matunda, tujiangalie maisha yetu tujiulize je tupo katika hatua gani?. je ni njiani? au kwenye kwenye miamba,? au kwenye miiba? au kwenye udongo mzuri?. tupige mbio tuufikie utimilifu na jambo lolote lisitusonge au lisitutenge sisi na upendo wa Mungu, iwe ni njaa, dhiki, udhia, taabu, raha, uzima, mauti, lolote lile, TUZIDI KUIITI ILE NGUVU YA ROHO MTAKATIFU ITAKAYOTUFIKISHA KATIKA UDONGO MZURI. Naye Bwana ataturuzukia baraka zake tukishinda.

Mungu akubariki!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa msaada wa maombi/Ushauri/ubatizo/mafundisho/Whatsapp: Namba zetu ni hizi: 

+255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

MAFUMBO YA MUNGU.

TOFAUTI KATI YA SHERIA YA ROHO WA UZIMA NA SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI!

SHETANI ANATOLEA WAPI FEDHA, ANGALI TUNAJUA FEDHA NA DHAHABU NI MALI YA BWANA?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Jamani Mungu wa Mbinguni awabariki kwa sababu mnakuwa baraka kwangu na kwa wengi pia..🙏🙏🙌🤝