by Admin | 1 October 2019 08:46 am10
Shalom, Mtu wa Mungu, karibu tujifunze biblia, Jukumu kubwa tulilopewa miongoni mwa mengi ni jukumu la kumfahamu sana YESU KRISTO, Na lengo kuu la kumfahamu sio kwasababu yeye anauhitaji sana wa Utukufu, au uhitaji sana wa kutafuta ajulikane, hapana! Hilo sio lengo…kwasababu pale tu alipo tayari anajulikana…Lakini bado anatuasa tunapaswa tumfahamu sana yeye…Hivyo hiyo ikimaanisha kuwa kwa jinsi tunavyomfahamu yeye ni tofauti na yeye anavyotaka sisi tumfahamu…
Kwasasa Mtu maarufu kuliko wote duniani kwa wakati wote ni YESU KRISTO, hakuna mwanadamu yeyote aliyewahi kufikia kiwango cha umaarufu alionao Bwana Yesu Kristo, ukienda kwa wachina, wahindu, wabudha wote wanamjua Yesu Kristo…Hata watu ambao sio wakristo kwa namna moja au nyingine walishawahi kumsikia Yesu Kristo katika Maisha yao..kwahiyo yeye ni maarufu tayari.
Biblia inasema katika…Waefeso 4: 13 “ …hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”
Na kwanini anataka sisi tumfahamu sana yeye? Mstari wa 14, hapo juu umetupa majibu… Ni ili tusiendelee kuwa Watoto wachanga, tukitupwa huku na huko, tukidanganywa na kila upepo wa elimu, na kuishia kuzifuata njia za udanganyifu.
Kwahiyo hakuna Elimu nyingine itakayoweza kutufanya tusiweze kudanganyika na elimu ya mashetani, isipokuwa Elimu ya kumfahamu Yesu Kristo, hakuna namna yoyote utakayoweza kuifahamu na kuidhibiti noti bandia pasipo kwanza kuijua noti halali ilivyo, ukishaifahamu noti halali ilivyo na tabia zake ndivyo utakavyoweza kuijua noti bandia..Kadhalika tunajukumu kubwa sana la kumfahamu Yesu Kristo kwa undani ili tuweze kuyadhibiti mafundisho ya mashetani na wapinga Kristo.
Leo tutajifunza kwanini Yesu Kristo, anajulikana kama Mwana wa Daudi na kwanini ni MFALME.
Sasa ni Dhahiri kabisa tunajua kuwa Yesu hakuwa na Baba wa kimwili, lakini kuna mahali kwenye maandiko kajitambulisha kuwa Mwana wa Daudi.. Sasa kwanini alijiita hivyo?
Sababu pekee ya Bwana Yesu kujulikana kama mwana wa Daudi, ni kutokana na Baraka Daudi alizozibeba, lakini si kutokana na undugu wa kidamu..Wewe unaitwa mwana wa Baba yako kutokana na uhusiano wa kidamu..lakini unaweza ukaitwa mwana wa Raisi wako, ila si kwa uhusiano wa kidamu bali wa pengine wa kiitikadi fulani….
Kwamfano pia sisi wakristo tunaitwa Wana wa Mungu, si kwasababu tumezaliwa familia moja na Muumba wetu,hapana au kwamba tuna damu moja na Mungu, hapana ni kutokana na Baraka za kimbinguni zinavyohusiana na sisi ndio maana tunaitwa wana wa Mungu.
Vivyo hivyo tunajulikana kwamba ni wana wa Ibrahimu , sio kwasababu sisi tuna damu moja na Ibrahimu, hapana bali ni kwasababu ni warithi wa Ahadi zile zile alizopewa Ibarahimu na Mungu, ndio maana na sisi tunajulikana kama wana wa Ibrahimu, Na Bwana Yesu ndio hivyo hivyo, Baraka alizopewa Daudi na mnyororo wa ukoo wake wote zilimhusu pia Bwana wetu Yesu Kristo…Daudi alikusudia kumjengea Mungu, Nyumba na hivyo Mungu akambarikia yeye na uzao wake kuwa uzao wa kifalme milele.(soma 2 Samweli 7:1-12)
kwasababu alizaliwa katika nyumba ya Yusufu ambaye alikuwa ni wa ukoo wa Daudi uliobarikiwa (ukoo wa kifalme),..Moja ya Baraka za ukoo wa Daudi ni kwamba utakuwa ni ukoo wa kifalme, kwamba wazao wote wa Kwanza wa Daudi walipakwa Mafuta na Mungu wawe wafalme soma (2 Wafalme 8:19,). Na ndio maana Bwana Yesu alipozaliwa katika nyumba ya Yusufu kama mzaliwa wa kwanza, roho ya kifalme ilikuwa juu yake. Kwahiyo kwa namna yoyote ile ni lazima angekuja tu kuwa Mfalme..
Je! Unajua kuwa Yusufu baba yake Yesu angepaswa awe mfalme wa Israeli kwa kipindi kile, kulingana na ahadi Mungu aliyomahidia Daudi?…Lakini kutokana na dhambi zao, Taifa la Israeli lilikatwa na uzao wa Daudi wa kifalme ukasimamishwa katika kutawala na ulisimamishwa kipindi gani?..
Kama ukisoma kitabu cha Wafalme, baada ya Daudi kufa, akafuata mwanawe Sulemani akawa mfalme kweli kulingana na ile Ahadi lakini naye pia akafa, na ikaendelea hivyo hivyo, kwa wajukuu na vitukuu vya Daudi, mpaka mfalme wa mwisho aliyetawala Yuda aliyeitwa Sedekia, ambaye alikuwa ni kitukuu cha 20 cha Daudi, huyu ndiye mfalme wa Mwisho kutawala Yuda, baada yake yeye, ndio Watu wakapelekwa Utumwani Babeli, hiyo ndiyo siku waliokatwa na waliporudi kukawa hakuna mfalme tena katika Israeli…vitukuu vya Daudi vilivyozaliwa baada ya Sedekia Mfalme wa Mwisho kufa, wakawa ni watu tu wa kawaida, kama watu wengine…
Ndio maana Yusufu baba yake Yesu alikuwa ni mtu wa kawaida tu maskini, ingawa alikuwa ni mwana wa kifalme…(Kwa urefu fuatilia ukoo huu wa Yesu kwenye kitabu cha Mathayo 1:1-17), laiti Israeli asingeasi na kupelekwa utumwani, Yusufu baba yake Yesu angekuwa mfalme wa Yuda, na Kristo angezaliwa huko…
Hivyo Israeli iliendelea kuwa kama mti uliokatwa baada ya kutoka Babeli…Wayahudi wakakaa mamia ya miaka bila mfalme….kukawa hakuna dalili yoyote ya Mfalme kunyanyuka katika uzao wa Daudi,..kwani Utawala wa Rumi ulikuwa umekamata dunia nzima, na Warumi waliwaweka watu wao kwenye makoloni yao yote, mpaka Israeli ilikuwa ni koloni la Warumi..Hivyo mtawala aliyetawala koloni la Israeli alikuwa ni Mrumi…jambo hilo liliendelea kwa miaka mingi…lakini Biblia ilitabiri katika Isaya Mlango wa 11 kuwa litatoka chipukizi katika shina la Yese….Kumbuka Yese alikuwa ni Baba yake Daudi, kwahiyo ni sawa na kusema litatoka chipukizi katika shina la Daudi au katika uzao wa Daudi. Tunasoma hayo katika…
Isaya11:1 “ Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana”.
Kama ni msomaji mzuri wa maandiko utagundua kuwa…hilo shina linalozungumziwa hapo si lingine Zaidi ya BWANA YESU KRISTO mwenyewe…Biblia inasema litatoka shina, ikiwa na maana kuwa ni kutoka katika mti uliokatwa, nalo litazaa sana matunda… Kama ulishawahi kuona mti mkubwa uliokatiwa chini kabisa..linakuwa linabaki tu kama gogo…halafu baada ya kipindi fulani unaona kitawi kidogo cha kijani kinajitokeza ubavuni mwa lile gogo, na kama hakitakatwa na chenyewe, baada ya kipindi fulani kitakuwa kikubwa na hatimaye kuwa tena mti mkubwa kama ulivyokuwa mwanzo…
Ndicho kilichotokea baada ya uzao wa Daudi kukatwa na kupelekwa Babeli…ni sawa na mti uliokatwa…lakini chipukizi likatoka, katika uzao huo huo wa Daudi..
Bwana Yesu, Mwana wa Daudi, mzao wa kifalme, mwenye ahadi ya kifalme juu yake, alizaliwa huko Bethlehemu, alikuwa ni mfalme aliyetoka katika shina lililokatwa ndio maana utaona alizaliwa katika zizi la ng’ombe, familia ya kimaskini, laiti Yusufu baba yeke angekuwa mfalme basi naye pia angezaliwa katika familia ya kifalme..Lakini kinyume chake alizaliwa katika ufalme uliokatwa…
Lakini maandiko yanatabiri, huyo atakuja kuwa mti mkubwa na utazaa sana matunda, na ufalme wake utaenea duniani kote…kipindi alichokuja miaka 2000 iliyopita, roho ya Bwana ilikuwa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana” Kwa hekima, na maarifa aliyoyabeba alituletea sisi Wokovu…ambao mpaka sasa tunanufaika nao…., Lakini katika utawala wa miaka 1000 ijayo, ndio tutamwona vizuri kama Mfalme, aliyeketi katika kiti cha Kifalme…katika wakati huo, yeye pamoja na sisi ambao sasa tumemwamini, tutatawala naye, sisi tutakuwa wafalme nay eye atakuwa kama Mfalme wa wafalme.
Wakati huo Mamlaka yote ya kifalme atakuwa nayo yeye, utakuwa sio wakati wa wokovu tena bali wakati wa utawala, sasa hivi ndio tupo wakati wa wokovu, nyakati hizo zitakuwa ni nyakati za utawala mkuu wa Yesu Kristo. Dunia yote itajawa na kumcha Bwana, kutakuwa hakuna vurugu, kutakuwa na Amani isiyo ya kawaida..simba na kondoo watakaa pamoja na hawatadhuriana, mtoto atacheza na nyoka, na hakutakuwa na madhara yoyote.
Tusome tena Isaya hii 11 Mpaka mwisho..
“1 Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;
3 na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;
4 bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.
5 Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.
6 Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.
10 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu”.
Ufunuo 3:20 “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 YEYE ASHINDAYE, NITAMPA KUKETI PAMOJA NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI, KAMA MIMI NILIVYOSHINDA NIKAKETI PAMOJA NA BABA YANGU KATIKA KITI CHAKE CHA ENZI.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”
Na pia alisema..
Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.
15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.
16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.
17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”
Kama hujampa Yesu Kristo Maisha yako, jua umechelewa sana, lakini mlango bado hujafungwa ingia kabla mlango hujafungwa..mwisho wa mambo yote umekaribia, na Kristo yupo Mlangoni kurudi, atakaporudi nyakati hii ya mwisho atakuja kama mfalme na mtawala mkuu hatakuja tena kama mwokozi.
Bwana akubariki.
Tafadhali share kwa wengine
Mada Nyinginezo:
JE! MTU KUSIKIA SAUTI ZA WATU WALIO MBALI, KUNAWEZA TOKANA NA MUNGU?
BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA “HERI WALIOTASA, NA MATUMBO YASIYOZAA, NA MAZIWA YASIYONYONYESHA”?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/01/kwanini-yesu-kristo-ni-mwana-wa-daudi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.