ZIFAHAMU HOJA SABA ZENYE NGUVU MBELE ZA MUNGU.

by Admin | 6 October 2019 08:46 am10

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe..Karibu tujifunze Neno la Mungu…Bwana Mungu wetu anatuambia tupeleke hoja zenye nguvu mbele zake?.
 
Isaya 41:21 “Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo”.
 
Sasa swali hizi hoja zenye nguvu ni zipi?
 
Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa anaposema tupeleke hoja, tunapaswa tuzipeleke vipi?…ni wazi kuwa hakuna njia nyingine ya kupeleka Zaidi ya kwenye maombi…maombi ndiyo njia pekee ya sisi kuzungumza na Mungu moja kwa moja!….Na pia kama anasema tupeleke hoja zenye nguvu…maana yake zipo pia hoja ambazo ni dhaifu!…Hivyo kwa kufupisha sentensi hiyo tunaweza kuiweka hivi “ tupeleke maombi yanayougusa moyo wa Mungu, au yanayoleta maana” kiasi kwamba yatamsukuma Mungu au kumshawishi kutupa majibu ya maombi yetu.
Sasa maombi hayo ni yapi?..Je ni ya kuomba muda mrefu?, au kupangilia maneno mazuri, au kuombewa na wengine? Au kufunga muda mrefu?…Hayo yote ni maombi ya hoja lakini si ya hoja zenye nguvu.
Maombi ya hoja zenye nguvu yapo SABA, Na hayo si mengine Zaidi ya yale tuliyofundishwa na Bwana wetu Yesu Kristo…alisema..
 
Mathayo 6:6 “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
 
7 Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
 
8 Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.
 
9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.
 
11 Utupe leo riziki yetu.
 
12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
 
13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina”.
Hizo ndio hoja zenye nguvu…Katika kusali/kuomba unahakikisha Unautambua kwanza uwepo wa Mungu, pale unaposema Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, hapo unaliadhimisha moja kwa moja jina la Mwanawe mpendwa Yesu Kristo ambalo ndio jina la Baba alilompa Yesu(soma Yohana 17:6, 17:11) na kwa kupitia hilo, ndilo tunaokolewa kwalo, kwahiyo Unaliadhimisha na kutangaza kuwa linastahili kutukuzwa… Hii ni hoja ya kwanza yenye nguvu mbele za Mungu, Bwana anatamani sana tujue uwezo uliopo kwenye jina lake, si kwa kukariri wala kwa ushabiki, bali kwa ufunuo..Tukijua kuwa hakuna jina lingine, iwe la Raisi, au la Nchi, au la Mfalme, au la Kitu, au la Malaika ambalo sisi wanadamu tumepewa, isipokuwa jina la Yesu…Hii ni hoja moja yenye nguvu sana inayoleta majibu pasipo vipingamizi..
 
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”
 
Hivyo katika sala pia, tunapaswa tuanze kwa kuliadhimisha na kulitukuza Jina la Yesu.
 
Hoja ya Pili: yenye nguvu ni Kuomba UFALME WAKE UJE!..
Ufalme wa Mungu unakuja kwa namna mbili, 1) Unakuja juu ya mtu, huu unaingia pale mtu anapochukua muda kumtafuta Mungu 2) Namna ya pili ufalme wa Mungu unakuja juu ya dunia nzima, watakatifu watakapofikia kilele cha kumfahamu Mungu, ndipo ufalme wa Mungu utashuka.
Sasa namna zote hizi mbili ni lazima mtu aziombe mbele za Mungu.
 
Wengi hawapendi kuomba ufalme wa MUNGU uje juu ya huu ulimwengu kwasababu wanaupenda bado ulimwengu huu…hivyo hawapendezwi sana wanaposikia tunaishi katika siku za mwisho, na hawapendi kuona siku za mwisho zinafika, kwasababu hawataenda tena disko, hawataenda tena vilabuni,n.k hawajui kuwa Kutokutamani au kutokuomba Ufalme wa Mungu uje ni kumhuzunisha Mungu…Hawajui kuwa kuomba ufalme wa Mungu uje ni hoja yenye nguvu ambayo Mungu anaithamini sana juu ya mtu, na hivyo kumsukuma Mungu kuuleta ufalme wake ndani ya huyo mtu mwenyewe na katika dunia nzima.
 
Hoja ya tatu: Ni kumwomba Mungu, mapenzi yake yatimizwe huku duniani kama huko mbinguni…Kwanini mbinguni kuna utukufu na tunatamani sana kwenda?…Ni kwasababu kule kila siku mapenzi ya Mungu yanatimizwa, ndio maana ni kuzuri na kuna utaratibu.. Wengi hawapendi kumwambia “Mungu mapenzi yako yatimizwe baada ya sala”..Utasikia nataka hiki nataka kile..hiyo sio hoja yenye nguvu na haileti majibu yeyote! Hoja yenye nguvu ni ile inayomalizia na “Baba mapenzi yako yatimizwe, si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe” Bwana Yesu mwenyewe alikuwa na mapenzi yake siku ile kabla ya kusulibishwa kwamba kikombe kile kimwepuke lakini alimalizia na kusema “baba mapenzi yako yatimizwe” wewe na mimi ni nani..tuamrishe mambo kana kwamba dunia ni yetu!…hiyo ni hoja yenye nguvu sana. (SomaYakobo 4:13-16).
 
Hoja ya Nne: Ni kumwomba Mungu atupe riziki zetu, hakusema tumwombe atupe fedha!…sio vibaya kumwomba fedha lakini hapo hakusema tumwombe atupe fedha! Bali riziki…Wengi ndio wanarudi nyuma katika hili Eneo, Wanapomwomba Mungu awape riziki, na riziki ile wanaitafsiri katika fedha tu peke yake, mtu wa Mungu, Mungu anaweza kukupa nyumba pasipo hata kuwa na shilingi 10 mfukoni mwako, anaweza kukupa chakula pasipo hata kuwa na fedha…Kwamfano Mtu anaweza kumwomba Bwana anahitaji wanawe wakasome pengine nje ya nchi, wakati anatazamia Mungu ampe mamilioni ya fedha ya kuwapeleka huko nje ya nchi, Mungu anafungua mlango wale Watoto wanafanya vizuri na kwenda kusomeshwa na serikali na yule mzazi bado akawa hana fedha vile vile…
 
Sasa tayari kashajibiwa maombi yake, ingawa yeye anaweza asione amejibiwa kwasababu alitazamia Mungu ampe mamilioni ya fedha..Mungu hafanyi kazi kwa njia hiyo tu peke yake…
Hebu tafakari wewe mwanao akija na bajeti, na kukwambia baba naomba milioni moja anataka kwenda kununua vitu vya shule utampa?..jibu ni kwamba hutampa badala yake utamwambia aorodheshe anavyohitaji..ndipo uende ukamnunulie..vinginevyo ukimpa hela utampoteza badala ya kumpata, na Mungu wetu hataki tupotee… Usiende kamwe kumwambia Mungu ninashida ya milioni 5 ya ada, au ya nyumba, au ya kiwanja….
 
Nenda kamwambie Mungu nina shida ya kiwanja basi!! Au nina shida ya chakula….Usimtamkie pesa! Kwasababu Mungu haangalii tunahitaji pesa kiasi gani bali anaangalia tunamahitaji kiasi gani?… Utashangaa anakupa hicho kiwanja, au hicho chakula, au hicho kiwanja pengine hata pasipo kutumia hiyo fedha unayoitegemea (Yeye ana njia nyingi sio hiyo wewe unayoifikiria kichwani kwako)…Hebu leo mwulize Mkristo anahitaji nini atakwambia anataka kuwa na hela nyingi, mwulize hizo hela ni za nini?, atakwambia basi tu akaunti yangu iwe inasoma..(sio vibaya kuomba hivyo lakini si hoja yenye nguvu mbele za Mungu)…
 
Usiende kumwomba Mungu fedha ya kitu fulani, kamwombe hicho kitu unachokihitaji, ili atakapofungua njia zake usizozitegemea ukakipata usije ukasema huyo sio Mungu.
Hoja ya tano: Ni kumwomba atusamehe makosa yetu, kama sisi tunavyowasamehe wengine..Zingatia hilo Neno… “kama sisi tunavyowasamehe wengine”…Hii ni hoja ya sita yenye nguvu, usitengeneze desturi ya kuomba pasipo kutubu, wala pasipo kuwasamehe wengine, maombi yako hayatasikilizwa kabisa, kama uliseng’enywa kumbuka na wewe ulishawahi kusengenya hivyo unamsamehe kwanza huyu au Yule ndipo unaendelea mbele.
 
Hoja ya sita: Ni kumwomba Mungu asitutie katika majaribu, lakini atuokoe na yule mwovu…Kutiwa katika majaribu hapo ni hali ambayo Mungu anaruhusu mtu aingie chini ya mikono ya shetani…Na hiyo inaweza kutokana na dhambi za Mtu au ukamilifu wa Mtu…Ayubu aliingia majaribuni kutokana na ukamilifu wake, Lakini Petro aliingia majaribuni kujaribiwa na Ibilisi amkane Bwana Yesu kutokana na Ubishi wake wa kukataa kuomba…Hivyo kwa ufahamu huo kuomba Mungu atuepushe na adui zetu kwa namna yoyote ile ni hoja Mungu anayotaka sisi tuiombe mbele zake na anaiheshimu sana.
 
Hoja ya saba na ya Mwisho: Ni kutambua ya kuwa Ufalme, na Nguvu na Utukufu una Yeye MUNGU wetu Milele na Milele. Kwanini Mbinguni kuna utukufu mwingi?..Ni kwasababu Malaika usiku na mchana wana ukiri Ukuu wa Mungu…
 
Ufunuo 7:11 “Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,
 
12 wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina”.
 
Kama malaika watakatifu wamepata ufunuo huo, na wanaheshimiwa na Mungu, nasi pia hatuna budi kukiri kuwa ni kweli heshima, utukufu, na nguvu zina yeye Milele na Milele siku zote katika Maisha yetu.Hoja hii ni hoja ya mwisho yenye nguvu..
 
Ndugu, iwapo kwenye maombi usisahau kila kipengele cha mambo hayo!, Na maombi yaliyomfanya Bwana kila saa asikiwe na Baba yake alipokuwa hapa duniani, na hivyo akatufundisha na sisi kusali kwa namna hiyo hiyo, tukizingatia hilo tutaona majibu yasiyo ya kawaida katika dua zetu na sala zetu za kila siku.
 
Bwana akubariki sana. Kama hujampa Kristo Maisha yako, unangoja nini?..Hizi ni siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi.

Mada Nyinginezo:

FAIDA ZA MAOMBI.

NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU.

WEWE SI MALI YAKO MWENYEWE!

UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/06/zifahamu-hoja-saba-zenye-nguvu-mbele-za-mungu/