UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.

UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.

Kutoka 34:29 “Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema naye.

30 Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia.

31 Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.

32 Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai.

33 Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake.

34 Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa.

35 Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.”.

Itakuwa hata wewe ulishawahi kugundua kitu hichi mfano ukikaa karibu na mtu ambaye amejipulizia marashi makali kwa muda mrefu, halafu ukaondoka utagundua kuwa vimelea vya yale marashi kwa sehemu Fulani vimebaki kwenye mwili wako,..Na ndivyo ilivyokuwa kuwa kwa Musa, baada ya kukaa uweponi mwa Mungu kwa muda wa siku nyingi, siku zaidi ya 80, ukijumlisha na zile 40 za Kwanza, alizokwenda kupewa amri na hukumu na zile mbao 2 za mawe, kwa wakati huo wote alipokuwa uweponi mwa Mungu kumbe kidogo kidogo utukufu wa Mungu ulikuwa unajiambukiza ndani yake pasipo yeye kujijua..Hadi siku aliposhuka chini na kuona watu wanamwogopa ndipo alipogundua kuwa Uso wake uling’aa sana kwa kule kumtazama Mungu.

Japo biblia haituambii ulikuwa unang’aa kwa namna gani hadi watu kumwogopa, lakini tunajua uling’aa kwa utukufu wa Mungu, pengine ulikuwa unameta meta kama almasi, mpaka watu wakaona huyu anaweza akawa asiwe mtu wa kawaida, pengine tukimgusa tunaweza tukafa..Ndipo Musa alipoona hivyo, akachukua utaji akaufunika uso wake, kupunguza makali ya utukufu ule, ili aweze kusimama mbele ya watu na kungumza nao.

Lakini japo uso wake uling’aa sana kwa namna ile, bado utukufu ule ulikuwa sio wa kudumu, kwasababu ulikuwa na wa kuhakisi tu, na sio kitu kilichotoka ndani yake, hivyo alipoondoka katika uwepo wa Mungu, kidogo kidogo ulikuwa unapungua hadi mwishowe ukatoweka kabisa…Japo biblia haituambii ni kwa kipindi gani utukufu huo ulidumu kwenye uso wake, pengine ulichukua siku, au wiki, au mwezi, au miezi, hatujui, lakini tunachojua ni kuwa ulikuwa ni utukufu usiodumu…Ulihitaji kuu-chaji, Na ndio maana ukisoma hapo juu utaona kila wakati Musa alipotoka kuzungumza na Mungu aliuvaa utaji ule, kwasababu utukufu wa Mungu ulijiakisi kwenye uso wake tena kwa wakati huo.

Hivyo ule utaji uliwazuia wana wa Israeli kuona hatma ya ule utukufu jinsi unavyokwisha, kwasababu Musa alikuwa anavaa utaji muda wote, Na ndio maana mtume Paulo, aliandika katika 2Wakorintho 3:13-16, kuwa hata leo hii wana wa Israeli utaji huo upo mbele yao, kwamba hawawezi kuona jinsi utukufu wake Torati ya Musa usivyokuwa wa kudumu..

“13 nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika;

14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; 

15 ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao.

16 Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.”

Swali linakuja je! mwanadamu afanye nini ili awe na utukufu usio batilika kutoka kwa Mungu? Apate Utukufu unaodumu wakati wote?.

Jibu lipo pale pale juu, tunapaswa tusiuakisi utukufu wa Mungu, bali tugeuzwe tuwe kama yeye. Hiyo ndio dawa pekee. Kwa kuelewa zaidi angalia mfano wa mwezi na nyota, utagundua kuwa nyota siku zote zinaangaza tu, huwezi kuta zinaonekana nusu, lakini mwezi, leo utauona unaonekana wote, kesho nusu, kesho kutwa theluthi, ni kwasababu gani?, ni kwasababu wenyewe unategemea mwanga wa jua kuangaza, unalihakisi jua, lakini nyota hazihakishi chochote kutoka katika jua kwani watafiti wanasema Nyota ni ma-jua mengine, isipokuwa tu yapo mbali na dunia na ndio maana kuangaza kwa nyota hakubadiliki badiliki.

Vivyo hivyo, ili sisi tuangaze utukufu kamili wa Mungu, tunapaswa tuguezwe tuwe miungu duniani, na anayeweza kufanya hii kazi si mwingine zaidi ya YESU KRISTO mwenyewe.

Pale tunapoiamini injili kweli kweli kwa kudhamiria kumwishia Mungu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, tunapotubu dhambi zetu, kuanzia hapo Kristo anachofanya ni kutubadilisha asili zetu, na kuwa kama Mungu,..kuanzia huo wakati utukufu wa Mungu unakuwa unamulika ndani yetu milele NON-STOP..Kazi yako itakuwa ni kujiweka mbele zake katika hali ya utakatifu na usafi zaidi, na kulitii Neno lake, ili uzidi kuangaza kwa utukufu mwingi zaidi, hapo ndipo unapokuwa kutoka utukufu hadi utukufu, kwasababu kumbuka hata nyota zinatofautiana utukufu(1Wakorintho 15:41)..Isipokuwa tu utukufu wa zote hauwezi kuisha kabisa kama mwezi, kwasababu tayari ndani yao kuna Nuru ya jua, lakini ni wajibu wa kila mwaminio, atoke utukufu hadi utukufu.

2 Wakorintho 3:7 “Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika;

8 je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?

9 Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.

10 Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana.

11 Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu.

12 Basi, kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi;

13 nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika;

14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; 

15 ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao.

16 Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.

17 Basi <Bwana> ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.

18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, TUNABADILISHWA TUFANANE NA MFANO UO HUO, TOKA UTUKUFU HATA UTUKUFU, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho”.

Unaona ni faida gani, mtu aliyonayo aliyedhamiria kweli kumwamini Kristo, na sio kigeugeu,? Mtu wa namna hii hata katika ulimwengu wa roho mashetani na mapepo wanachokiona ni miale ya moto tu inapita, uchawi utampatae mtu kama huyo? Au LAANA?. Na ndio maana Shetani anachofanya sasa katika hichi kipindi cha mwisho ni kupofusha tu fikra za watu wapuuzie mambo haya ya msingi:

2Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;

4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, ISIWAZUKIE NURU YA INJILI YA UTUKUFU WAKE KRISTO ALIYE SURA YAKE MUNGU.”

Mfikirie Kristo kwa jicho lingine, Yule huwa akimbadilisha mtu, anambadilisha kweli kweli, hasemi uongo kama sisi wanadamu tulivyo, Hakuja kufanya kazi ya kubahatisha duniani, kazi yake ni thabiti kabisa.

Bwana akubariki sana. 

Kwa Maombezi, Ushauri au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +255789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.

MADHAIFU

WATU WASIOJIZUIA.

UNAFANYA NINI HAPO?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments