by Admin | 9 October 2019 08:46 am10
Shalom, mtu Mungu nakukaribisha tujikumbushe tena Neno la Mungu kwa yale ambayo tulishawahi kujifunza huko nyuma lakini leo tutaangalia kwa upana zaidi, na naamini utaongeza kitu kipya katika ukristo wako(Wafilipi 3:1), Biblia inaufananisha utendaji kazi wa Mungu na vitu viwili cha kwanza ni Moto na cha pili ni Upepo. Bwana Yesu alipomuhubiria Nikodemo habari za kuzaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu, Nekodemu alistaajabia sana na kusema inawezekanikaje mtu kuzaliwa mara ya pili lakini Bwana Yesu akamwambia maneno haya:
Yohana 3:7 “Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.
8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho’’.
Sasa kama ukiichunguza tabia ya Upepo, wataalamu wanasema kuwa Upepo hauna sauti yoyote, Na Kama ni hivyo basi kile tunachokisikia ni nini?, wakati mwingine upepo ukivuma utasikia kama mluzi Fulani hivi unajipiga, au maporomoko Fulani au vitu Fulani vidogo vidogo vinadondoka,n.k. jibu ni kuwa ule upepo wakati unapovuma unakutana na vitu vingi katika safari yake, sasa pale unaposuguana na vitu hivyo inasababisha kutokee sauti fulani, au ule upepo ukisukuma vile vitu inasababisha vile vitu kugongana vyenyewe kwa vyenyewe na kusababisha sauti pia, kwamfano upepo ukikutana na mti, ukipita katikati yake unasababisha matawi kugongana gongana yenyewe kwa yenyewe na hapo hapo kelele ya matawi inasikika, vivyo hivyo unapokutana na vipande vidogo vidogo vya mawe na uchafu, vinapogongana gongana ndio sauti hapo hapo inatokea na hapo ndipo mtu anapogundua kuwa eneo hilo lina upepo mkali au mdogo..Lakini kama upepo ukiwa unapita tu hewani na haukutani na kizuizi au kipingamizi chochote basi kamwe hutakaa usikie au ujue kama kuna upepo wowote unapita hapo iwe ni mkali au mdogo..Eneo hilo litakuwa kimya na tulivu kuliko hata kitu chochote ulichowahi kukisikia.
Na ndiyo maana Bwana Yesu alimfananisha Roho Mtakatifu kama Upepo uvumao ndani ya mtu aliyezaliwa mara ya pili..Hawezi kumwona Roho jinsi anavyokuja juu yake wala huwezi kumchunguza jinsi anavyofanya kazi ndani yake, lakini kitu kitakachomtambulisha kama anavuma juu yake au la ni ile sauti anayoitoa yeye mwenyewe.. Na sauti hiyo ni tabia yako na mwenendo wako baada ya kuzaliwa mara ya pili.
Kwa jinsi utakavyoanza kuonyesha tabia nyingine ghafla, ulimwengu utajiuliza mtu huyu ni kitu gani kimemkumba kinachomfanya aishi hivi, au onyeshe tabia za namna hii, lakini kwamwe hawatapata jibu wala kukiona..Kwasababu Roho Mtakatifu ni kama upepo hautambuliki na ulimwengu, wala ulimwengu hauwezi kumtambua.
Yohana 14:16 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
17 ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.
1Wakorintho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.”
Hivyo ikiwa wewe umezaliwa mara ya pili kweli kweli kuna mambo utagundua Mungu ameyageuza ndani yako, utashangaa ile kiu ya kutamani mambo maovu imekufa ndani yako, utashangaa unapenda kila wakati kujifunza Neno la Mungu jambo ambalo hapo kwanza ulikuwa huwezi, utajikuta hupendi tena kukaa karibu na watu wabaya au waovu au zile kampani mbaya ulizokuwa nazo hapo nyuma, watu wataanza kukushangaa umekuwaje au umeingiliwa na nini. Sasa ukishaona hivyo ujue ni upepo wa Roho unavuma ndani yako, usihangaike kuwathibitishia kuwa huyo ni Mungu hawatakuelewa, ni rahisi wao kukutafsiri umedanganywa na walokole, au umepotoshwa…usiwasikilize hapo fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani yako, wewe itii tu, usiichunguze sana, kwasababu hata wewe ukiichunguza ni ngumu kujua chanzo chake ni wapi na mwisho wake ni wapi, lakini wewe itii hiyo na uifuate maadamu inakupeleka kumpenda na kumtafuta Mungu zaidi..
Na ndio maana tunasema, mtu hawezi kudai amezaliwa mara ya pili na huku nyuma bado maisha yake kwa nje yapo vile vile hayajabadilika, ni wazi kuwa Roho Mtakatifu bado hajaanza kupita juu ya huyo mtu.
Tabia nyingine ya Roho Mtakafu ni Moto, Kama vile biblia inavyosema..
Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto”.
Moto nao vile vile unatabia kama ya upepo huwa hautoi sauti, sauti yake huwa inakuja kutoka katika vile vitu unavyovichoma, kichaka kikiwashwa moto hapo nje, hata kama upo ndani utajua tu nje kuna moto unawaka kwa jinsi kile kichaka kitakavyokuwa kinatoa kelele zake. Na sauti inaweza kuwa kubwa kulingana na kitu kinachochomwa, kwamfano kama inachomwa nazi pale inapopasuka utasikia inapasuka inatoa mlimo mkubwa kama bomu tofauti na karatasi.. lakini pia tabia nyingine ya moto ni kwamba sio vitu vyote inaviteketeza, kwa mfano ukiweka karatasi na dhahabu pamoja, halafu vyote ukavichoma, mwisho wa siku utagundua lile karatasi limeteketea lote lakini ile dhahabu imezidi kuwa mpya ziadi.
Na ndivyo ilivyo Roho Mtakatifu anavyombatiza mtu kwa moto, ni ngumu kumwona, lakini kazi zake utaziona, vile vitu vyote dhaifu ambavyo ni uovu vilivyokuwa ndani yake ataviteketeza mara moja, lakini vile vitu imara na vizuri ndani ya mtu ni kama dhahabu hivyo vinazidi kuwa imara.
Vile vile Roho Makatifu hawabatizi tu watu wema, bali pia na watu waovu, biblia inasema hivyo katika Mathayo 5:45 “kwamba huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”. lakini kwao inakuwa ni kinyume chake, badala ya kuimarishwa wanateketezwa, biblia inasema..
Waebrania 12:29 “maana Mungu wetu ni moto ulao.”
Na kibaya zaidi moto huu unapowateketeza hawajui kama unawateketeza kwasababu huwa hautoi sauti, utajua tu unawateketeza kwa kule kulalamika kwao na kutaabika kwao kiroho huo ndio uthibisho kuwa moto wa Mungu unapita juu yao kuwala. Na moto huo huo hauishii hapa duniani ndio ule unaoendelea mpaka kwenye ziwa la moto.
Usiulaumu moto na kuuona kuwa ni mbaya kwasababu ulikuchomea nyumba yako, ukasahau kuwa moto huo huo ndio unaokupikia chakula kila siku, ndio unaotumia kuchome taka, ndio unaokupa nishati kila siku, unaweza kukufanya kutazama tv,radio, unaoweza kukufanya kuchaji simu yako na kusoma ujumbe huu, unaweza kupigia pasi nguo zako ukawa mtanashaji, unaweza kusafiri kwa kutumia chombo chako cha moto n.k..
Vivyo hivyo usilaumu kwanini watu waovu watateketezwa kwa moto, kikubwa tu ni kujiepusha na ghadhabu na hasira ya Mungu kwasababu ni kawaida ukienda kinyume na sheria ya moto, utakuunguza hata wewe mwenyewe, moto unahitaji umakini wa hali ya juu kuendana nao. Kadhalika Moto wa Roho Mtakatifu unahitaji umakini wa hali ya juu kuendana nao vinginevyo ni rahisi kujikuta tunajipeleka wenyewe jehanamu ya moto.
Ukiyajua hayo na huku bado upo nje ya Kristo hakuna sababu ya wewe kuendelea kuwa hivyo,..Kwanini usimruhusu Roho Mtakatifu ayaumbe maisha yako upya?, kwanini usiruhusu moto wake na upepo wake uanzee kupita juu yako na kukuimarisha na kukupeleka kule atakapo? Jambo hilo la heri na neema ni bure kabisa.. Tubu hapo ulipo kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako zote, kumbuka kutubu ni kugeuka, na kuacha kile ulichokuwa unakifanya ambacho sio sahihi.. Na Bwana akishaona umedhamiria kabisa kwa moyo wako wote wote kugeuka basi yeye ataanza jukumu la moja kwa moja kukugeuza, na bila kuchelewa nenda katafute mahali ubatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la Yesu Kristo kukamilisha wokovu wako, naye atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, kulingana na Matendo 2:38..Na kuanzia huo wakati na kuendelea utakuwa umehesabiwa kuwa mojawapo wa kondoo wa Bwana unayestahili uzima wa milele, na kuhesabiwa haki bure kwa Imani yako.
Bwana akubariki sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine. Na Bwana atakubariki.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/09/kwanini-moto-na-upepo-vinawakilisha-tabia-za-mungu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.