KWANINI MAISHA MAGUMU?

by Admin | 11 October 2019 08:46 am10

Jibu jepesi la swali hili ni kwasababu hapo nyuma tulitoka nje ya kusudi la Mungu.

Tangu mwanzo Mungu hakumuumba mwanadamu ateseke wala asumbuke kwa namna ambayo tunaiona sasa hivi, Mungu alikuwa tayari ameshamwandalia mazingira marahisi sana ya kuishi kiasi kwamba siku zake zote tangu kuumbwa kwake hadi milele na milele asingewahi kujua kama kuna kitu kinachoitwa jasho, wala maumivu kwenye mwili wake…lakini kwasababu wazazi wetu wa kwanza waliasi, ndio ikawa chanzo cha kuvurugika mpango mzima au mfumo mzima wa maisha ambayo  Mungu alitupangia sisi tuuishi.

Mwanzo 3:17 “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;

18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;

19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”

Unaona hapo? Leo hii unahangaika huku na kule, chakula unakula cha shida, nguvu unayoitumia kutafuta pesa haiendani na unachokipata, kujenga tu nyumba 1 inakuchukua miaka 20 kumalizika kana kwamba unajenga mji wa New York, bado matibabu yanakuumiza kichwa, bado elimu, bado familia, bado ndugu, bado jamii inayokuzunguka, n.k. vyote hivyo vinakufanya uone kama haya maisha hayakupendi, mpaka unaliza swali kama hilo, unafika mpaka kwenye ukurasa huu..Fahamu kuwa ni Mungu ndiye kakuleta hapa anataka kusema na wewe.

Lakini pamoja na kuwa tulitoka nje ya mpango wake, hakutuacha yatima, aliahidi kutandalia makao mengine mapya ambayo raha yetu ile ya mwanzo tuliyokuwa nayo itarejea na hata pengine zaidi ya pale na hiyo inakuja mara  baada ya maisha haya kuisha, lakini pia aliahidi hata tukiwa hapa hapa duniani kwenye dhiki hizi nyingi, bado atakuwa na sisi kuhakikisha kuwa anatupa WEPESI wa maisha …Lakini neema hiyo ameahidi kuitoa tu kwa wale ambao watakuwa tayari kumpokea..

Bwana Yesu alisema maneno haya:

Mathayo 11:28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

Unaona Ni YESU tu pekee ndiye anayekuahidia PUMZIKO LA MAISHA YAKO. Hakuna mwanadamu yoyote anaweza kukuahidi kitu kama hicho, ukiwa ndani ya Kristo atakupa AMANI ambayo hata kama mfukoni huna kitu, utajiona wewe ni zaidi ya tajiri yeyote duniani, utakupa tumaini ambalo, litakufanya usione haya maisha kuwa ni kitu cha kukisumbukia sana..atakutunza atakulinda atakuhifadhi..

Unachopaswa ni kumpa tu maisha yako, kuanzia leo aanze kuyaongoza nawe utaona wema wake

Anasema:

 Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. (Zaburi 34:8).

Na hiyo inakuja kwa kutubu kabisa kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote…Na baada ya hapo atakuja ndani yako, lakini sharti ukabatizwe katika ubatizo wa kuzamishwa katika maji mengi, kwa Jina la YESU KRISTO upate ondoleo la dhambi zako, kama hukuwahi kufanya hivyo na yeye wenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu atakaye kulinda, na kukupa wepesi wa maisha haya. Mpaka siku ile ya kwenda mbinguni.

Mathayo 6:25 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

26 Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

27 Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?

28 Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti

29 nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.

30 Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?

31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?

32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.

33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Ubarikiwe.


 

Mada Nyinginezo:

JAWABU LA MAISHA YA MTU.

JE! KUBET NI DHAMBI?

JEHANAMU NI NINI?

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA.

JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/11/kwanini-maisha-magumu/