HAMJAFAHAMU BADO?

by Admin | 16 October 2019 08:46 pm10

 Moja ya mambo ya muhimu sana ambayo Roho Mtakatifu anayafanya ndani ya mtu baada ya kukata shauri la kumfuata Yesu Kristo, kwa moyo wote ni “KUMWONDOLEA HOFU YA MAISHA HAYA” Karibia kila mwamini katika hatua za kwanza kwanza kabisa, Roho Mtakatifu ni lazima ampitishe katika madarasa ya kumwondolea hofu ya Maisha haya…Kwasababu katika hali ya kawaida wanadamu wote tukishafikisha umri fulani, tayari hofu ya Maisha inakuja yenyewe ndani yetu…Hofu ya Kesho itakuwaje! Mwakani nitaishije! Nitakula nini wiki zijazo, nitaishije ishije! Na mambo mengine mengi…Hofu hii haijalishi wewe ni nani, maadamu umeshaitwa mtu, tena mwenye Akili timamu lazima ije ndani yako…Ni hofu ambayo inamfanya mtu awe mtumwa wa Kesho! Ni hofu ambayo inamfanya mtu asiwe anaridhika na mwisho wa siku anakuwa katika mkandamizo mkubwa wa mawazo..

Sasa Roho Mtakatifu anajua kabisa hatuwezi kumtumikia Mungu katika hali hiyo ya utumwa wa Kesho itakuwaje! Kwasababu hiyo basi ni lazima ampitishe katika kipindi fulani cha madarasa, kuipunguza hiyo hofu ndani ya Mtu ili aweze kuishi kwa furaha akiwa ndani ya Yesu.

Hebu fikiria mwanao, anakaa nyumbani mwako, halafu anakwenda shule huku anamashaka kwamba Kesho anaweza asipate chakula nyumbani, au akiwa na mashaka kwamba atakosa ada! Je! Huyo mtoto atasoma kweli, au atafanya vizuri darasani? Ni wazi kuwa hatasoma bali atakuwa ni mtu tu wa mawazo siku zote! Na itamsababishia kufeli, na hivyo hivyo Mawazo ya Maisha haya na mawazo ya Kesho itakuwaje! Itatusababishia tusimwelewe Mungu na kutusababisha tufeli mitihani mingi ya Maisha yetu ya kikristo.

Kulitatua hilo Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake masomo kadhaa, ya kutohofia Kesho, na hivyo kwa masomo hayo pia anatufundisha na sisi…Embu tusome tukio hili moja..

Mathayo 16:5 “Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate.

6 Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

7 Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.

8 Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate?

9 Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?

10 Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?

11 Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

12 Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo”

Somo hilo Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi baada ya Wanafunzi wake kusahau kubeba mikate ya safari yao..Hivyo walipofika njiani, Bwana Yesu akawaambia wajihadhari na chachu ya mafarisayo, wenyewe wakadhani anawashutumu kwanini hawakubeba mikate katika safari yao..na hivyo hawana kitu cha kula, kwamba Bwana kawakataza wasile chachu ya mafarisayo…(kumbuka chachu ni hamira, na chachu ilikuwa inawekwa kwenye mikate, hivyo mtu akizungumzia chachu ilikuwa inajulikana kwamba anazungumzia mikate yenye Hamira)..

Hivyo wanafunzi wakahuzunika sana, kwasababu watakwenda kukaa na njaa bila chakula huko wanakokwenda…Lakini Bwana Yesu aliwakemea na kuwaambia wana Imani chache…kwasababu wameshasahau jinsi gani Bwana alifanya miujiza ya kutokeza maelfu ya mikate kutoka katika mitano tu na maelfu ya watu wakala na kusaza na kukusanya mabaki mengi tena mara mbili… kama Mungu aliweza kufanya hivyo huko nyuma kwanini asiwafanyie tena hivyo huko mnakokwenda?? Huo ndio ulikuwa ujumbe wa Bwana! Wasianze kutafakari tafakari Kesho wakula nini? Kesho kutwa watavaa nini…wao kazi yao ni kuangalia mbele kuitenda kazi ya Mungu na hayo mengine watazidishiwa…

Tunaona tena mahali pengine Bwana Yesu alizidi kulitilia mkazo jambo hilo katika Mathayo Mlango wa 6

Mathayo 6: 24 “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.

25 Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

26 Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

27 Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?

28 Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti

29 nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.

30 Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?

31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?

32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.

33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake”

Unaona! Bwana anatufundisha ni jinsi gani, Kesho yetu ipo mikononi mwake, kwamba haijalishi leo sina chochote lakini Kesho nitakuwa na kitu..Bwana hawezi kutupungukia kabisa ikiwa tu tupo katika kusudi lake, anasema hivyo katika Neno lake (Waebrania 13:5), anajua tuna haja ya chakula, mavazi, malazi, makazi n.k lakini anachotutaka ni sisi kumtafuta kwanza yeye..Tusiwe na hofu ya Kesho..Kwasababu Hofu ni utumwa, hakuna mtu yeyote mwenye hofu, akapiga hatua yoyote mbele, hakuna.

Tatizo lililopo tunataka pindi tu tunapomkaribisha Yesu Maishani mwetu, basi atupe ratiba ya leo, Kesho na miaka mitano au kumi mbele itakuwaje! Tunataka tuone Kesho tutakuwa na shilingi ngapi mifukoni mwetu, uhakika wa kila kitu…Mungu si wakati wote anatenda kazi hivyo, wakati mwingine unaweza kukupitisha katika ukame leo, na huku hujui Kesho utakuwaje na ghafla ukashangaa kafungua mlango Kesho ukapata unayohitaji tena na zaidi ya matarajio yako…

Hivyo yeye anataka tu tumwamini kwamba hatatuacha kabisa! Anafahamu tunayohitaji!

Kama unafanya shughuli yoyote ambayo inakupatia kipato, na ikatokea ukapungukiwa kabisa, anatakiwa umwamini kuwa hajakuacha, na wala hana mpango wa kukuacha!..kumbuka wakati fulani nyuma ambapo ulipitia kupungukiwa na akakufungulia mlango kimiujiza…ukumbuke huo muujiza, na usikie sauti yake leo moyoni mwako ikikuambia…HUJAFAHAMU TU?..Haujafahamu bado?..Siku ile ulipopungukiwa na akakufungulia mlango kimiujiza?..Yatafakari matendo yake ya nyuma kisha Uinyanyue Imani yako kwake..na siku zote utaishi Maisha ya furaha na yasiyo na hofu, ukijua kuwa Baba yako wa Mbinguni, sio Baba wa kambo, ni Baba wa damu kabisa ambaye hapendi kuona utakufa njaa wala kuteseka.

Maombolezo 3:36 “Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa”.

Bwana akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP



Mada nyinginezo:

CHAKULA CHA ROHONI.

USITAFUTE FAIDA YAKO MWENYEWE BALI YA WENGINE.

YAKUMBUKE YA NYUMA.

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?.

LAANA YA YERIKO.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/16/hamjafahamu-bado/