MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?.

MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?.

Bwana wetu Yesu Kristo japo alikuwa ni Mungu mwenyewe katika mwili lakini hakuwa mnafiki kutokuonyesha hisia zote wanadamu wanazopitia wakiwa hapa duniani, Kama wengine walivyotazamia kuwa Mungu akiuvaa mwili, basi yeye atakuwa ni kama malaika duniani, Na ndio maana Waebrania 2:16-18 inasema:

16 Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu.

17 Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.

18 Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

Unaona? Bwana alilia palipopaswa kulia, sehemu nyingine aliomba Mungu amwepushe, na kikombe cha mateso ikiwa ni sawa sawa na mapenzi ya Baba yake, kwa namna ya kawaida tunaweza kusema hofu ya kibinadamu ya kuuawa ilimwingia.

Vile vile Japo siku zote alifahamu Baba yake yupo pamoja naye, hawezi kumwacha, na alishamweleza kitu kuhusu maisha yake, na mwisho wake utakavyokuwa, na yatakayotokea baada ya hapo, lakini kuna saa huzuni ilikuwa inamwingia….Halikadhalika Bwana akiwa pale msalabani alijua kabisa siku zisizodi tatu atakuwa utukufuni, akijua kabisa safari yake imeshakwisha kikamilifu, amebakisha dakika chache tu aondoke duniani lakini katika hatua ile ile ya mwisho, tunaona anamwambia baba yake maneno haya:

Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Fahamu kuwa alikuwa hazungumzi maneno haya ili kujifanya, ni kweli kabisa ndani ya moyo wake, hakuwa anaona uwepo wowote wa ki-Mungu, ndani yake hakukuwa na chochote, alikuwa hana tofauti na wale wezi aliosulibiwa nao, ni kama vile kaachwa Solemba, alikuwa kama mtu ambaye Mungu hajawahi kuzungumza naye kabisa, ndivyo alivyojiona ndani yake..

Tukitafsiri kwa lugha ya leo tunaweza kusema, Ee! Mungu mbona katika siku za raha ulikuwa pamoja nami, ulikuwa unatembea nami, wala hakukuwa na shida yoyote, iweje leo katika shida zangu, umejitenga mbali nami?. Mungu wangu, Mungu wangu, upo wapi mbona umeniacha?.

Hali kama hii hii ilimkuta Daudi wakati anakimbizwa na Sauli, wakati anapitia shida nyingi mapangoni, wakati yupo katika kukataliwa, na dhiki, akaona kama vile Mungu hajihusishi tena, kamwacha peke yake, tunasoma:

Zaburi 10:1 “Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?”.

Zaburi 13: 1 Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?

2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?

3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.

Nawe pia Wakati mwingine unaweza ukawa unapitia hali ngumu, magonjwa ya kutisha ambayo madaktari wamekuambia hakuna matumaini hapa, watu wanakutisha na kukupa shuhuda za waliokufa kwa magonjwa ya namna hiyo, unaumwa Kansa, unaumwa Ukimwi, Presha, Kisukari na magonjwa yote ya ajabu yaliyo duniani siku hizi. Umeombewa sana, ila hali bado ipo vilevile.

Na kweli ndani ya moyo wako unajua kabisa Mungu wako hawezi kukuacha, lakini bado unahisi kama vile hakuoni katika hali unayopitia sasa, unahisi kama vile, amekaa kimya, hachukui hatua yoyote kwa hilo tatizo ulilonalo kwa muda mrefu..

Nataka nikutie moyo, Biblia inasema Mungu hakuwahi kulidharau teso la mteswa. Na maneno hayo yafaraja tunayapata katika Kitabu cha Zaburi, kitabu kile kile ambacho Bwana YESU alikinukuu akiwa pale msalabani, ndicho hicho hicho Mungu alimpa majibu ya maneno yake…

Tusome:

ZABURI 22

1 Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?

2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.

3 Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.

4 Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.

5 Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.

6 Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.

7 Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;

8 Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.

9 Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.

10 Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.

11 Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.

12 Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;

13 Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.

14 Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.

15 Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti

16 Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.

17 Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.

18 Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.

19 Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.

20 Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.

21 Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.

22 Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.

23 Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.

24 MAANA HAKULIDHARAU TESO LA MTESWA, WALA HAKUCHUKIZWA NALO; WALA HAKUMFICHA USO WAKE, BALI ALIPOMLILIA AKAMSIKIA.

25 Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.

26 Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.

27 Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.

28 Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.

29 Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,

30 Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,

31 Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.


Ukisoma ule mstari wa 24, anasema: 24 MAANA HAKULIDHARAU TESO LA MTESWA, WALA HAKUCHUKIZWA NALO; WALA HAKUMFICHA USO WAKE, BALI ALIPOMLILIA AKAMSIKIA.

Na wewe vile vile ambaye umeokoka, umepitia hali ya shida kwa muda mrefu, bila kuona dalili yoyote ya kuponywa au kutoka katika mahali ulipo, fahamu kuwa Mungu hajalidharau teso lako, wala hachukizwi nawe, wala hajauficha uso wake kwako, bali siku ile ya kwanza ulipomlilia alishakusikia, hivyo hutakufa. Kwahiyo kaa katika matumaini ya kuipokea muujiza wako, wakati aliokuandalia utaufurahia wema wake, ulio mwingi. Ilikuwa ni lazima Mungu aruhusu Bwana Yesu ayapitie yale ili alete faida kubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni ndio maana Mungu alikaa kimya kwa wakati ule, lakini alipomaliza kazi yake, mateso yale yamekuwa sababu ya mimi na wewe kuupata wokovu. Vivyo hivyo na wewe usitishwe na kitu chochote, maadamu yupo pamoja na wewe sikuzote. Atakupigania.

Songa mbele na Bwana Yesu Kristo atakuonekania.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine. Na Mungu atakubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

MNGOJEE BWANA

MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU:

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.


Rudi Nyumbani

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Pascal michael
Pascal michael
1 year ago

Niweke kama muhuri moyon mwako, kama muhuri katika mkono wako; kwa maana upendo ni kama kifo; wivu ni dhulumu kama kaburi; makaa yake ni makaa ya moto ambayo ina moto mwingi wa moto.

Pascal michael
Pascal michael
1 year ago

Ee mungu wangu na kuomba unibariki katika kazi yangu na maisha yangu katika jina lako