TUNAMHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUYAELEWA MAANDIKO.

by Admin | 22 October 2019 08:46 pm10

Katika biblia nzima hakuna mahali utaona pametabiriwa kwa wazi kuwa Kristo atakaa kaburini siku tatu, na baada ya siku ya tatu atafufuka. Hakuna mahali popote kwenye Biblia palipoandikwa ufunuo huo…Tunaona unabii wa Kristo kuzaliwa na Bikira uliandikwa wazi katika Isaya 7:14 kwamba atazaliwa na Bikira, kadhalika unabii wa Kristo kuzaliwa Bethlehemu ya Uyahudi ulitabiriwa wazi katika kitabu cha Mika.

Mika 5: 2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”…

Kadhalika unabii wa Bwana Yesu kuteswa kwa ajili ya dhambi zetu uliandikwa wazi katika Isaya

Isaya 53:4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

Na Nabii nyingine Nyingi zimuhusuzo Yesu ziliandikwa wazi hata za kuja kwake mara ya pili…Lakini katika unabii wa kukaa kaburini siku tatu, huo haukuandikwa wazi..Uliihitaji Ufunuo wa kipekee wa Roho ili kuujua…Kwasababu Yesu mwenyewe alisema ilipaswa yote yatimie yaliyoandikwa na Manabii, Torati na Zaburi. Na pia ulipaswa utimie unabii alioandikiwa yeye kuhusu kukaa kaburini siku tatu.

Luka 24:44 “ Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika TORATI YA MUSA, NA KATIKA MANABII NA ZABURI.

45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.

46 Akawaambia, NDIVYO ILIVYOANDIKWA, KWAMBA KRISTO ATATESWA NA KUFUFUKA SIKU YA TATU;”

Sasa ni wapi palipotabiriwa kuwa Kristo atakaa kaburini siku tatu?

Pasipo ufunuo wa Roho hakuna mtu angejua kuwa Yesu Kristo alitabiriwa hayo, hata Wanafunzi wa Yesu walikuwa hawajui, si Zaidi Mafarisayo..Lakini tunaona Roho Mtakatifu mwenyewe alifichua fumbo hilo na kutuonesha sisi katika maandiko kuwa ni wapi Kristo alitabiriwa kukaa siku tatu kaburini…tunasoma katika..

Mathayo 12:39 “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.

40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi”

Unaona? Kumbe Maisha ya Yona yalikuwa ni UFUNUO WA YESU KRISTO kukaa kaburini siku tatu?? Nani alikuwa analijua hilo?? Hata Yona mwenyewe alikuwa halijui.

Sasa kama Maisha ya Yona yalikuwa yamebeba siri nzito namna ile, inayomhusu Yesu….ya Yusufu yatakuaje? Ya Musa yatakuaje?, ya Ayubu na Danieli yatakuwaje?..Tunamhitaji Roho Mtakatifu atufunulie maandiko tuweze kumwelewa. Hakika pasipo yeye hatutaelewa chochote katika maandiko.

Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia”.

Ukisoma tena katika maandiko utaona Bwana YESU alikuwa yupo tayari kutueleza pia mambo ya mbinguni, lakini kwa kutokuamini kwetu, hakutueleza(Yohana 3:12),.. Lakini Kristo mwenyewe aliahidi kuwa huyo Roho Mtakatifu atakapokuja atayatwaa yaliyo yake na kutupasha sisi habari,(Yohana 16:14).

Umeona umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu sasa?, Swali ni Je! Umempata?..Na hata kama unaye je! amejaa kwa wingi ndani yako? Bwana atusaidie!

Kama hujampa Yesu Kristo Maisha yako, mlango wa Neema bado upo wazi, lakini hautakuwa hivyo siku zote.Tubu kwa kumaanisha kuacha dhambi kama hujatubu, na zingatia kutafuta ubatizo sahihi, wa kuzama mwili wote majini na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38. Na yeye mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu bure kama alivyoahidi katika Neno lake kwa wale wote waaminio.

Maran atha!

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

UMUHIMU WA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUZAA MATUNDA.

JE! HIZI ROHO SABA ZA MUNGU NI ZIPI? NA JE ZINATOFAUTIANA NA ROHO MTAKATIFU?

DHAMBI YA KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU NI IPI?

UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

JE! BIKIRA MARIA NI MALKIA WA MBINGUNI?


 

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/22/tunamhitaji-sana-roho-mtakatifu-katika-kuyaelewa-maandiko/