KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?

by Admin | 3 December 2019 08:46 pm12

SWALI: Krisimasi ni nini, Je! ni kweli Yesu alizaliwa tarehe 25 disemba, Je ni sahihi kwa mkristo kusheherekea Krisimasi?


Krisimasi au kwa lugha ya kigeni Christmas, Ni neno lenye muunganiko wa maneno mawili: Kristo na masi/misa na hivyo  kuunda neno Kristo-masi, au misa ya Kristo, inayomaanisha  pia ibada ya Kristo.

Ni siku ambayo mabilioni ya wakristo duniani kote wanaisheherekea kama siku ya kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristo, ambayo inadhaniwa kuwa ilikuwa ni tarehe 25 ya mwezi Disemba. Hivyo kila mwaka siku kama hii na tarehe kama hii wakristo wengi sana wanaienzi kama siku ya kuzaliwa kwa shujaa wa wokovu wetu YESU KRISTO.

Lakini Je! kimaandiko Yesu alizaliwa tarehe 25 Disemba?

Hakuna mahali popote katika biblia inatoa tarehe au mwezi wa kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa kutathimini tu majira na mazingira yaliyokuwa yanaendelea siku ya kuzaliwa kwake ndiyo iliyopelekea kuzaliwa siku  na miezi tofauti tofauti kama hiyo.

Sasa kutokana na kuwa na mitazamo mingi tofauti tofauti, makundi mengi yamezaliwa na kila moja linadai mwezi wake na tarehe yake. Mengine yanaamini Kristo alizaliwa mwezi Aprili, mengine yanaamini Kristo alizaliwa mwezi Agosti… na mengi septemba na mengine octoba na mengine Disemba n.k.. Lakini lililopata umaarufu mkubwa ni hilo la mwezi Disemba..Lakini Je! Kristo alizaliwa kweli mwezi huo?

Zipo Sababu kadhaa kwenye maandiko zinazothibitisha kuwa Yesu hakuzaliwa mwezi Disemba.

kama tukisoma kitabu cha Luka tunaweza kupata kiashirio kimojawapo… tunaona kuwa malaika Gabrieli alimtokea Zakaria kuhani (babaye Yohana mbatizaji) siku fulani maalumu ambayo tayari ilikuwa imeshapangwa na mbingu, nayo tunasoma ilikuwa ni siku ya zamu za ukuhani wa ABIYA.

Luka 1: 5 “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa ZAMU YA ABIYA, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.

6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.

8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,

9 KAMA ILIVYOKUWA DESTURI YA UKUHANI, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba”.

Ahaa! Tusoma Kumbe katika siku za zamu za Abiya.. ambazo alikuwa anafanya kazi za kikuhani ndizo Zekaria alizotokewa na malaika Gabrieli. Sasa ili kufahamu zamu ya Abiya ilikuwa inaangukia katika miezi ipi turudi katika agano la kale tusome ndipo tutakapopata majibu ya majira ya ambayo Zekaria alitokewa na Malaika Gabrieli.

Na kama tunavyosoma katika 1Nyakati 24. Inasema:

1Nyakati 24: 7 “Kura ya kwanza ikamtokea Yehoiaribu, na ya pili Yedaya;

8 ya tatu Harimu, ya nne Seorimu;

9 ya tano Malkia, ya sita Miyamini;

10 YA SABA HAKOSI, YA NANE ABIA;

11 ya kenda Yeshua, ya kumi Shekania;

12 ya kumi na moja Eliashibu, ya kumi na mbili Yakimu;

13 ya kumi na tatu Hupa, ya kumi na nne Yeshebeabu;

14 ya kumi na tano Bilga, ya kumi na sita Imeri;

15 ya kumi na saba Heziri, ya kumi na nane Hapisesi;

16 ya kumi na kenda Pethahia, ya ishirini Ezekieli;

17 ya ishirini na moja Yakini, ya ishirini na mbili Gamuli;

18 ya ishirini na tatu Delaya, ya ishirini na nne Maazia”.

Kwahiyo hapo tunaweza kuona zamu ya Abiya ilikuwa ni ya NANE katika ufanyaji wa kazi za kikuhani. Na kazi hizo zilikuwa zinafanyika sabato mpaka sabato yaani wiki mpaka wiki,.. hivyo zama ya Abiya iliangukia wiki ya 8 katika utendaji kazi wa kikuhani. Na tunajua kuwa mwaka wa kiyahudi hauanzi kama huu wa kwetu huku, januari hapana bali huwa unaanza mwanzoni mwa mwezi april,.. na hivyo ukihesabu hapo majuma mawili utaona zamu hiyo inadondokea katikati ya mwezi wa 6.

Kwahiyo mpaka hapo tunaweza kusema sasa Zekaria kumbe alitokewa majira ya mwezi wa 6 na muda mfupi baada ya hapo pengine mwezi wa 6 mwishoni au wa 7 mwanzoni mkewe Elizabethi alipata mimba, na biblia inatuambia pia miezi 6 baada ya kupata mimba kwake Elizabethi Malaika Gabrieli alimwendea Bikiria Mariamu na kumpasha habari za yeye kupata mimba ya Bwana Yesu (Luka 1:26).

Hivyo mpaka hapo tunaona itakuwa imeshafika mwezi wa 12 katikati, au mwezi wa kwanza mwanzoni, ndipo mimba ya Bwana wetu YESU ilipotungishwa. Na tunajua kuwa baada ya miezi 9 mtoto huwa ndio anazaliwa, sasa ukipiga hesabu utaona kuwa uwezekano mkubwa wa kuzaliwa kwa Bwana wetu YESU KRISTO unaweza angukia katikati ya mwezi wa 9 au mwanzoni mwa mwezi wa 10, kwa kalenda yetu sisi. Na ndio maana utaona pia Bwana Yesu alianza kuhubiri akiwa na miaka 30 na akamaliza  kuhubiri akiwa na miaka 33 na nusu, na siku aliposulibiwa wote tunajua  ilikuwa ni Mwezi wa nne (April). Kwahiyo ukihesabu vizuri hapo utagundua alianza kuhubiri kati ya mwezi wa 9 hadi wa 10, ambao ndio mwezi aliozaliwa, ili kutumizia jumla ya miaka mitatu na nusu ya huduma yake.

Zipo pia thibitisho nyingine zinaonyesha kuwa Kristo alizaliwa majira hayo lakini hatuwezi kuziandika zote hapa. Kwahiyo Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Disemba..

Je! Chimbuko la Kristo kuzaliwa tarehe 25 Disemba limetoka wapi?

Kwa kufuata na kuzaliwa kwa mungu ya kirumi TAMUZ ndipo tarehe hii ikageuzwa na kuwa ndio siku ya kuzaliwa kwa Bwana wetu YESU KRISTO.

Lakini je! wanaodhimisha siku hiyo tarehe 25 Disemba (Krisimasi) wanafanya makosa?.

 Jibu ni hapana biblia haijatoa amri juu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu (krisimasi) mahali popote, kwamba ifanyike au isifanyike, na hivyo yeyote anayefanya hivyo ikiwa ni kwa lengo lake binafsi kwamba anaona umuhimu wa kuunda siku yake inayoweza kukaribiana na siku ya kuzaliwa kwa Yesu ili amtukuze na kumfurahia Mungu, Iwe ni Aprili, iwe ni Agosti, iwe ni Septemba, Iwe ni Octoba, Iwe ni Disemba iwe ni siku yoyote ile hatendi dhambi maadamu kaiweka wakfu kwa Mungu wake, ili kumwabudu na kumshukuru kwa kupewa zawadi ya wokovu duniani.

Hivyo kama unaiadhimisha siku maadamu unaidhamisha kwa Bwana wako na si kwa mungu mwingine mgeni, ni vizuri zaidi na itakuwa ni ya Baraka kwako hata kama ni tarehe 25 Disemba, siku ya Krisimasi kama utaifanya kuwa ni siku ya kumsifu Mungu na kumshukuru Mungu itakuwa ya Baraka kwako.lakini kama utaifanya hiyo kuwa ni siku yako ya kuabudu sanamu au kwenda kufanya uzinzi, au kunywa pombe, au kwenda disko, au kwenda kwenye anasa ni heri usingeihadhamisha kabisa kwasababu jambo unalolifanya ni machukizo makubwa..Unamsulibisha Kristo mara ya pili.

Fanya uamuzi sahihi;

Je! Umeokoka? Unafahamu kuwa hizi ni siku za mwisho na KRISTO yupo mlangoni sana kurudi?..  Dalili zote zinaonyesha kuwa hichi kizazi tunachoishi mimi na wewe kinaweza kushuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Kristo..Unaongojea nini?

Tubu dhambi zako leo, ukabatizwe kwa JINA LA YESU KRISTO upate ondoleo la dhambi zako, Kisha Bwana atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu kukulinda mpaka siku ile ya UNYAKUO.

Bwana akubariki.

Nikutakie Krisimasi Njema, Na heri ya mwaka mpya ujao!

Kwa mafundisho zaidi ya Neno la Mungu/maombezi/wokovu/ushauri wasiliana nasi kwa namba hizi +255693036618/ +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

Je! ni sahihi kwa Mkristo kusherekea siku yake ya kuzaliwa.[Birth day]?

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/03/krisimasi-christmas-ni-nini-je-ipo-katika-biblia/