KWANINI NI LAZIMA TUFE KWA HABARI YA DHAMBI?.

by Admin | 29 June 2020 08:46 pm06

Tunapaswa tufe kwa habari ya dhambi kwasababu kitendo hicho ni kitendo  kinacholazimisha UHAI wetu kuhamishwa toka pale ulipokuwa kwanza na kwenda sehemu nyingine..

Kama vile tunavyojua siku zote kitu pekee kinachoweza kuuhamisha uhai wa mtu ni Kifo. Ukifa leo hii  Moja kwa moja uhai wako unatoka na kwenda kwingine.., Na hiyo inapelekea watu kutokutujua mahali ulipoelekea, haijalishi watakutafuta vipi kamwe hawatakaa wajue mahali ulipo isipokuwa Mungu peke yake.

Na ndivyo ilivyo pale mtu anapokufa kwa habari ya dhambi, kwa kuzaliwa mara ya pili, Uhai wake unahamishwa na kwenda kuficha na Mungu mwenyewe, mbali na shetani au kitu kingine chochote, kiasi kwamba hata ibilisi akutafuteje rohoni  hawezi kukupata kamwe…

Biblia inasema..

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu”.

Unaona, pale tunapokufa ndipo uhai wetu unapofichwa.  Ikiwa tutasema tumeokoka, lakini bado tunaendelea kuyaishi maisha yale yale ya kale, tuwe na uhakika kuwa Mungu hata hana shughuli na uhai wetu..Ikiwa hatutakuwa tayari kuacha uzinzi wetu, uasherati, disko, fashion, matusi, ulevi, ambayo tunafanya mara kwa mara n.k. basi tujue bado shetani anayo mamlaka makubwa sana juu ya uhai wetu..

Anao uwezo wa kututumia vyovyote apendavyo, anao uwezo wa kuyashinda maamuzi yetu, anao uwezo wa kutuletea majaribu ya ajabu ajabu, ikiwemo vifo visivyo vya wakati, anao uwezo wa kuyazuia maombi yetu, anauwezo wa kutufanya tusiyaelewe maandiko. Na zaidi ya yote anakuwa na uwezo wa kuyaingilia maisha yetu kwa viwango kikubwa sana kwa kwa kutumia majeshi ya mapepo yake.

Na ndio hapo utaona, mtu anasema siwezi kushinda dhambi Fulani, siwezi kuacha kuishi maisha Fulani ya dhambi, siwezi kuacha kujichua , Ni kwasababu hakukubali kufa kwanza ili uhai wake uchukuliwe na kwenda kufichwa kwenye moyo wa Mungu.

Mtu aliyefichwa uhai wake, shetani anakuwa haelewi chochote Mungu alichokipanga juu yake, shetani anachofanya ni ku-kisia kisia tu, pengine kesho yake itakuwa hivi au itakuwa vile, lakini haelewi chochote uhai wake unaendelea kuwa moyoni mwa Mungu mbinguni daima, umefichwa huko, ukisubiria wakati maalumu wa kufichuliwa tena.. Kwasababu kitu kinachofichwa ni sharti siku moja kifichuliwe/kifunuliwe.

Na utafunuliwa lini? Biblia inaendelea kusema..

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.

4 Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”.

Ipo siku ambayo, watu wote wa Mungu watafahamu kusudi halisi la Mungu kuwaumba ni nini?.. siku watakapoona mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, siku ambayo watakavikwa miili mipya isiyoharibika na kutawala na Kristo kama wafalme na makuhani milele.. Ni siku isiyokuwa na mfano, Hatupaswi kuikosa hata mmoja wetu.

Na ndio maana biblia inazidi kutuambia..katika

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”.

Lakini kama utausoma  tu ujumbe huu au mwingine wowote mfano wa huu, kwa desturi na mazoea ya kila siku, kujitimizia tu ratiba yako, na huku hutaki kufanya badiliko lolote ndani yako, uhai wako bado hauuthamini  upo mikononi mwa ibilisi, ufahamu kuwa kila unalolisikia shetani naye analihesabu na kuliandika,  ili siku ile utakapojikuta katika mitego yake ya hatari ya kukumaliza, awe na hoja za kutosha za kumwambia Mungu ni kwanini hupaswi kupewa msaada.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! shetani anaweza kuyajua Mawazo ya mtu ,hata kama mtu huyo hatayatamka?

JIWE LA KUKWAZA

KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA,

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/29/kwanini-ni-lazima-tufe-kwa-habari-ya-dhambi/